5/13/16

Wanaodhalilisha Wabunge Wanawake Wapo Juu ya Sheria?

 

Agost 2012 aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga Mrisho Gambo, alitoa kauli ya kidhalilishaji kwa aliyekuwa Mwanasheria wa Halmashauri hiyo Najum Tekka, kuhusu uhalali wa shahada aliyonayo huku akiihusisha shahada hiyo na vitendo vya ngono.

Kauli za kidhalilishaji dhidi ya viongozi wanawake zimeendelea kuota mizizi  kutokana na wanaofanya vitendo hivi kutochukuliwa hatua kali za kisheria; hali inayochangia kijirudiarudia huku wanaofanya vitendo hivi wakijiona wapo juu ya sheria kwani Aprili 24, 2013 aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Uzini, Mohammed Seif Khatib (CCM) aliwahi kusema wabunge wa Viti Maalumu wa Chadema wamepata nafasi hizo kwa kuwa ni wake, wapenzi na wachumba wa viongozi wa chama taifa.

Sambamba na hilo pia Mbunge wa Jimbo la  Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) aliwahi kutoa kauli ya kidhalilishaji dhidi ya wabunge wanawake kwamba baadhi yao wanapata mimba zisizotarajiwa.

Kutokana na kukithiri kwa vitendo hivi ndani ya ukumbi wa bunge unawafanya Wabunge wanawake 53 wa Kambi ya Upinzani kutoka Vyama vya CUF na Chadema kujitoa kwenye Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG) kutokana na kauli aliyoitoa Mbunge la Ulanga, Godluck Mlinga (CCM) Mei 5 mwaka huu katika kikao cha Bunge la 11 alipokuwa akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017 na kusema wabunge hao kutoka Chadema walipata ubunge kwa njia ya mapenzi huku akikataa kuomba radhi baada ya kutoa kauli hiyo ya kidhalilishaji.

Mlinga alisema wabunge wanawake ndani ya Chadema, walipata nafasi hiyo baada ya kuwa ‘baby’ wa watu huku akiongeza kwamba ndani ya chama hicho wamo pia wenye uhusiano wa jinsia moja licha ya kutotaja majina ya wabunge hao, akasema “Kila mwanamke ndani ya Chadema kaingia ubunge kwa sifa yake lakini sifa kubwa ni lazima uwe baby (mpenzi) wa mtu.Ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja,”.

Katika barua yao ya kujitoa  iliyosainiwa na Mbunge wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee kwa niaba ya wabunge wenzake wa Kambi ya Upinzani na nakala kupewa Spika, Job Ndugai, ilieleza kuwa kauli ya Mlinga inadhalilisha wabunge hao, utu na heshima ya mwanamke.

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts