5/5/16

Wizara ya Maliasili na Utalii Yalidhia TANAPA Kuwa Jeshi USU la Uhifadhi Wanyama Pori.


Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akikagua gwaride maalum la wahitimu wa Mafunzo ya Mabadiliko ya Mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa Jeshi Usu kwa Wahifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyofanyika kambi ya mafunzo Mlele mkoani Katavi juzi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akitunuku vyeti kwa wahitimu wa Mafunzo ya Mabadiliko ya Mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa Jeshi Usu kwa Wahifadhi za Taifa(TANAPA) yaliyofanyika kambi ya mafunzo Mlele mkoani Katavi juzi.
 Maofisa wa Jeshi Usu la hifadhi wanyamapori la TANAPA wakiwa katika sherehe hizo.
Mhifadhi Sekela Mwangota akisoma risala  ya Wahitimu wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa mgeni rasmi ,Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudance Milanzi (hayupo pichani) wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwa wahifadhi na askari waaajiriwa wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyofanyika kwenye kambi ya Mafunzo Mlele mkoani Katavi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipongezana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi mara baada ya kufunga Mafunzo ya Mabadiliko ya Mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na askari waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa yaliyofanyika kambi ya Mafunzo Mlele mkoani Katavi.
*************
Na Mwandishi Wetu,Katavi.
WIZARA ya Maliasili na Utalii  imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa jeshi usu (Paramilitary) ili kukabiliana  na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori ,misitu, na rasilimali nyingine za nchi.
Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi, wa shirika hilo Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya shirika hilo kutaka kubadilishwa na kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni ya msingi katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori.
Ufungaji wa mafunzo hayo ulifanyika  juzi katika kambi Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo katika mkoa mpya wa Katavi Magharibi mwa Tanzania ambapo jumla askari 101 na wahifadhi 26  walihitimu mafunzo ya kijeshi ya miezi 3 na 6 kwa pamoja.
“Kwa sasa uhifadhi unakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili,hususan Tembo na Farukuporomoka kwa maadili ya askari na uingizaji wa mifugo hifadhini”alisema.
Aliongeza:“Maombi yenu yamekuja kwa wakati muafaka hivyo tutawasilisha katika mamlaka nyingine za juu za kiserikali, ili yatungiwe sheria na hatimaye kuwasilishwa bungeni ili  yajadiliwe na kupitishwa kuwa sheria”.
Hata hivyo  aliwataka askari hao pamoja na menejimenti ya ya TANAPA kufanya maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa  baadhi ya mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kwa ilivyo kwa majeshi mengine nchini.
“Katika mambo ya msingi  mabadiliko hayo yatakapofanyika, ni pamoja na kuzingatia suala nidhamu kwa askari,uwajibikaji na kuepuka kujihusisha na masuala ya vyama vya wafanyakazi na pia kuhukumiwa  au kuadhibiwea katika mahakama  maalamu ya kijeshi (Court martial) pale askari atakapokiuka taratibu za kijeshi”aliongeza Meja Jenerali Milanzi.
Awali akiwasilisha maombi hayo Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijazi alisema shirika lake baada ya kutafakari kwa kina wakitumia wataalamu wa ndani ya shirika walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za kijeshi kutokana na changamoto ya sasa ya katika masuala ya uhifadhi.
“Askari wetu wanapewa  mafunzo  ya kivita  na pia silaha za kivita katika doria ili kukabiliana na majangili, lakini wanapotimiza wajibu wao wamekuwa  wakikabiliwa na changamoto ya kutotambuliwa na sheria za nchi na mara nyingi wamejikuta katika matatizo”alisema Kijazi.
Akitoa mfano alisema mara nyingi yanapotokea mapambano ya kati askari wetu na majangili  ndani ya hifadhi, na yakajitokeza madhara sheria zilizopo haziwalindi askari pale matumizi ya silaha zilizotumika zinavyoanishwa kisheria.
“Itambulike kuwa kwa sasa majangili hasa wanaoua Tembo wanatumia silaha za kisasa, teknolojia ya kisasa pamoja na mitandao ya kupashana habari hivyo bila kubadilisha mbinu si rahisi kukabiliana nao”alisema Mkurugenzi huyo.
  
Alisema lengo la mafunzo hayo ya kijeshi kufanyika ni pamoja na kuwajengea uwezo askari kuwa wakakamavu na kufikia maeneo hatarishi ndani ya hifadhi wakati wakiwa doria na pia kukabiliana na majangili  kwa mbinu za kisasa za kijeshi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo ambayo ni ya tatu kufanyika yataendelea kwa watumishi wa idara zote za shirika hilo wakiwemo maafisa wajuu ili kila moja awajibike  na kwenda na kasi ya serikali ya awamu tano ambayo inasisistiza  watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na uaminifu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael  Muhuga  alielezea umuhimu wa kutunza maeneo yaliyohifadhiwa nchini huku akionya kuwa makundi ya wafugaji yanayovamia maeneo hayo lazima yaondolewe haraka.
“Mkoani kwangu Katavi tumefanya tathamini na kugundua kuwa kuna mifugo 800,000  imevamia mapori ya akiba na hifadhi ya Taifa ya Katavi hivyo  tatafanya opresheni maalumu ya kuwaondoa ndani ya muda mfupi ujao”alionnya Mkuu huyo wa Mkoa.
Aliongeza:”Tutawatumia askari hawa hawa   waliohitimu kufanya kazi hiyo, na operesheni hii itakuwa ya kudumu,  na katika hili hatutavumilia  wanasiasa kutuingilia katika utendaji  na utekelezaji wa  majukumu ya kiserikali,”  
Mafunzo hayo ya kijeshi  ni ya tatu kwa askari na watumishi wa shirika hilo ambalo linasimamia  hifadhi 16 katika maeneo mbalimbali nchini.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts