6/12/16

"CHURA" ya SNURA sasa yahamia kwa Wanafunzi wa Shule ya Msingi, Waunda kundi

 
KIZAAZAA kimeibuka katika shule ya Msingi Mbande, kata ya Chamazi nje ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya baadhi ya wanafunzi kuunda kundi linalojiita chura ambalo kazi yake ni kukata viuno hadharani wakati wenzao wakiwa darasani.
Staili ya wanawake kucheza muziki wa kimwambao kwa kukata viuno hatari, ya chura, imekuwa maarufu tangu video ya wimbo wa 'Chura' ya msanii Snura Mushi ipigwe marufuku na Baraza la Sanaa (Basata) Aprili.
Mbali na wanaokata viuno hadharani wakati wa masomo shuleni hapo, wanafunzi wengine wameunda kundi jingine hatari linalofanya wizi.
Wanafunzi hao ni wa darasa la sita na la saba ambao wameunda makundi hayo na kuyapa majina ya 'Chura' kwa wanenguaji na 'Dadaz' na 'Nyodoz' ambayo kazi yake ni ugomvi.
Makundi mengine ni 'Mtaa wa Kongo' na 'Chizi' ambayo yanajihusisha na wizi ndani na nje ya shule.
Tayari Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema ameliangiza Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika na kuwafungulia mashtaka ili iwe fundisho kwa wengine.
Mjema alitoa agiza hilo jana shuleni hapo wakati akipokea mifuko 600 ya saruji iliyotolewa na taasisi ya GSM kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule hiyo. Mfuko mmoja wa saruji kwa sasa unaanzia Sh. 10,000 kwa Dar es Salaam.
Taasisi hiyo licha ya kukabidhi mifuko hiyo, imeahidi kutoa madawati 400 ili kukabiliana na tatizo la wanafunzi kukaa chini kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi walioandikishwa mwaka huu baada ya serikali kuagiza elimu bure kwa shule za msingi na sekondari.
Akizungumza na Nipashe, msichana mmoja anayesoma darasa la 7C, ambaye yuko katika kundi la 'Dadaz, alisema waliliunda kundi hilo baada ya kuwa na ugomvi na wanafunzi wenzao.
Mwanafunzi huyo alimtaja aliyebuni jina la kundi hilo ambalo linapambana na kundi la 'Nyodoz'.
“Kiukweli nilijikuta nimeingia tu kwenye mkumbo huu kwa sababu marafiki zangu walikuwemo humo, ila walimu walituita ofisini wakatuonya na kutaka makundi hayo yasambaratishwe, yapo lakini hayana nguvu kwa sasa,” alisema.
Alisema kundi la 'Chura' ni la wanafunzi wa darasa la sita ambalo hukatika viuno na kufunua nguo mbele ya wanaume hata nyakati za masomo.
Mwalimu Brigita Kuluwia anayefundisha darasa la saba alisema kinachowasumbua wanafunzi hao ni kuwa katika kipindi cha kukua kimwili.
“Suala hili liliibuka mwanzoni mwa mwaka huu na wiki iliyopita Mwalimu Mkuu, Dauden Mwakyambiki alitoa adhabu ya viboko vitano kwa wanafunzi hao na kupewa ushauri nasaha,” alisema.
“Tuliwashirikisha wazazi wao walipokuja kuchukua ripoti zao ili wakati huu wakiwa nao majumbani watusaidie kuwarekebisha tabia zao.”
Suala hilo liliibuliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Shule hiyo, Martine Jairo ambaye alieleza kuwa moja ya changamoto inayokabili shule hiyo ni kukosekana kwa uzio hivyo kusababisha wanafunzi kujihusisha na mambo yasiyofaa ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi hivyo.
Mwanaidi Omari, mmoja wa wazazi wenye watoto shuleni hapo, alisema kinachochangia tatizo hilo ni tabia ya watoto kupenda kuiga mambo yasiyofaa.
Mwalimu Mkuu Mwakyambiki alisema shule hiyo ina wanafunzi 5,815 ambapo wasichana ni 3,030 na wavulana ni 2,785 huku vyumba vya madarasa vikiwa ni 16 tu.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts