6/24/16

Diwani wa CCM mbaroni kwa tuhuma za kumuua mfugaji


JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Diwani wa Kata ya Mkwatani (CCM) wilayani Kilosa, Hussein Mwinchea (38), tuhuma za mauaji ya mfugaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema tukio hilo limetokea juzi, saa 7 mchana, katika kijiji cha Kisaki wilayani Kilosa.

Kamanda huyo alisema mtuhumiwa huyo, akiwa na silaha aina ya Shotgun ikiwa na risasi 6, alifyatua moja iliyompiga Moringe Kandiri (33), mfugaji wa jamii ya Kimasai, mkazi wa Mazoka wilayani humo, ambaye alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa.

Katika hatua nyingine, Christina Nuru (36) mfugaji wa jamii ya Kimasai anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumshambulia mkulima.

Matei alisema tukio lililotokea pia juzi, saa tisa Alasiri katika kijiji cha Dihombo, wilayani Mvomero.

Alisema siku ya tukio, watu wasiofahamika wa jamii ya Kimasai wakiwa wanachunga ng’ombe wao, walingiza mifugo hiyo kwenye shamba la Peter Mdidi (26) mkazi wa Hembeti na kuchana magunia 60 ya mpunga yaliyokuwa yameandaliwa shambani hapo kwa ajili ya kupelekwa nyumbani.

Kamanda Matei alisema kutokana na tukio hilo, wakulima nao walikamata ng’ombe 250 na kuwapeleka ofisi ya kijiji cha Dihombo, hatua iliyosababisha wafugaji hao wakiwa shambani, kuanza kumpiga mkulima Anatori Kunambi (55) na kumsababishia uvimbe katika mnono wake wa kushoto.

Alisema mkulima huyo alitibiwa katika zahanati ya Dakawa na kuruhisiwa na kwamba mali iliyoharibiwa haijafahamika thamani yake.

Kamanda Matei alisema jitiada za kuwasaka watuhumiwa wengine zinaendelea.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts