6/12/16

Maamuzi kwa Wanafunzi 6 wa Shule ya Msingi Waliooana Haya Hapa


WANAFUNZI sita waliooana wakiwa shuleni ni miongoni mwa jumla ya wanafunzi 20 walioachishwa masomo shule ya msingi visiwani Zanzibar katika muhula wa 2015/2016 kutokana na kujiingiza kwenye maisha ya ndoa badala ya kujiendeleza kielimu, imefahamika.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Juma Pembe ndiye aliyefichua taarifa hizo wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017, mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Akieleza zaidi kuhusu tatizo hilo linalochangia kukwaza maendeleo ya elimu visiwani Zanzibar, Waziri Riziki alisema wanafunzi hao 20 walitimuliwa kutokana na kubainika kufunga ndoa kabla ya kuhitimu masomo yao wakiwamo waliooana.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya elimu namba 6 ya mwaka 1982 kifungu cha 20(3), wanafunzi hawaruhusiwi kuingia katika maisha ya unyumba kabla ya kumaliza masomo na ndiyo sababu ya kutimuliwa kwa wanafunzi hao 20 wa shule mbalimbali za msingi.
Aidha, Waziri Riziiki alisema kuwa kesi nane za kupata ujauzito zimejadiliwa kati ya takribani 20 zilizoripotiwa na wanafunzi waliojadiliwa wameruhusiwa kuendelea na masomo baada ya kukidhi matakwa ya sheria namba nne ya kuwalinda watoto.
UKATA WATIKISA BODI YA MIKOPO
Awali, Waziri Riziki alisema kuwa idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu Zanzibar imeshuka kwa asilimia 13 katika mwaka wa fedha wa 2015/2016.
Waziri huyo alisema idadi kamili ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo imeshuka kutoka wanafunzi 3,499 hadi 3,046 kutokana na uhaba wa fedha.
Aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2015/2016, Bodi ya Mikopo ilitarajia kutumia Sh. bilioni 8.2 kama ruzuku ya Serikali ya kuwakopesha wanafunzi lakini wamekwama kupata fedha hizo kama zilivyokuwa zimeidhinishwa.
“Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia Mei 31, 2016, jumla ya Sh. bilioni 3.6 zilipatikana ikiwa ni sawa na asilimia 44.3 kama ruzuku ya serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa fedha 2016/2017, fedha kwa ajili ya mfuko wa elimu ya juu imeshuka hadi kufikia Sh. bilioni 6.1 kutoka Sh. bilioni 8.
Alisema kuwa idadi ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaopokea mikopo kupitia SMZ imefikia 3,046, wakiwamo wanafunzi wapya 575 pamoja na wale wanaoendelea na masomo 2,471 katika vyuo vikuu vya ndani na nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, waziri huyo alisema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu Zanzibar imeongeza nguvu katika ukusanyaji wa madeni baada ya idadi ya wahitimu wanaolipa kufikia 1,016 kutoka 744 na hivyo kufanikiwa kukusanya Sh. milioni 660 kutoka Sh. milioni 360 kwa mwaka.
Waziri huyo alisema kwa msingi huo, Wizara ya Elimu katika mwaka ujao wa fedha imepanga vipaumbele viwili vikiwamo vya kuongeza upatikanaji wa fursa sawa za elimu kwa wanafunzi wa ngazi zote za elimu za mafunzo ya amali, pamoja na kuinua ubora wa elimu na kujenga stadi katika ngazi zote za elimu na mafunzo.
Katika bajeti hiyo, Waziri Riziki alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopo katika sekta ya elimu, bado kuna matatizo ya upatikanaji wa fedha katika kufanikisha miradi na programu zinazopangwa kila mwaka.
Alisema kuwa programu ya elimu mbadala na watu wazima ilipangiwa kupata mgawo kutoka serikalini wa Sh. milioni 500 lakini hadi mwishoni mwa Mei, ni Sh. milioni 260.4 tu ndizo zilizopatikana (asilimia 33) wakati Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ikichangia Sh. milioni 946.4, sawa na asilimia 5.2 ya matarajio yake.
Aidha, alisema kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha kilitengewa Sh. milioni 60 kufanikisha programu ya elimu mjumuisho na stadi za maisha kwa watu wenye mahitaji malumu wakiwamo walemavu, lakini hadi Mei 31 mwaka huu, zilipatikana Sh. milioni 800 tu, sawa na asilimia 1.3 ya bajeti yake.
Aliongeza kuwa vifaa maalum vya kufundishia na kujifunzia kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa macho na viziwi vilipatikana kutoka Jumuya ya watu wasioona Zanzibar (ZANAB) na pia kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Zantel.
Waziri Riziki aliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha matumizi ya Sh. bilioni 140.1, kati ya hizo Sh. bilioni 92.9 ni kwa kazi za kawaida na Sh. bilioni 47.2 kwa kazi za maendeleo.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts