6/24/16

Magufuli: Mafuriko ya kisiasa marufuku hadi 2020

WAKATI kukiwa na hali ya kizungumkuti juu ya vyama vya siasa kuendesha shughuli zao ikiwa ni pamoja na mikutano na makongamano,

Rais John Magufuli amesema sasa ni wakati wa kutekeleza yale aliyoahidi wananchi, hivyo hatokubali mtu yeyote kumkwamisha na kwamba muda wa kufanya siasa ni baada ya miaka mitano ijayo.

Hivi karibuni vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupinga zuio la Jeshi la Polisi kufanyika kwa mikutano ya kisiasa nchini.

Kabla ya kukimbilia mahakamani, vyama hivyo pamoja na chama cha ACT- Wazalendo vimekuwa vikipinga kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara pamoja na makongamano ya ndani huku vikidai ni kinyume cha misingi ya demokrasia.

Kwa mara ya kwanza, Rais Magufuli amezungumzia suala hilo ambalo katika siku za karibuni limekuwa likilalamikiwa na wanasiasa na wanaharakati.

Akizungumza jana wakati wa kupokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, Rais Magufuli alisema siasa kwa sasa hazina nafasi hadi baada ya miaka mitano.

“Niwaombe wanasiasa wenzangu, tufanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi, tuliyotekeleza au ambayo hatukutekeleza,” alisema.

”Ushindani wa sasa wa vyama vya siasa unaotakiwa uchukue nguvu zaidi ni kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi, kama ni kwa madiwani, wakajenge hoja kwenye baraza la madiwani, kama ni wabunge, wakazungumze kwa nguvu zote bungeni. Lakini hata kuziba midomo nayo ni demokrasia, hiyo ni demokrasia na mwelekeo wa aina yake,” alisema Rais Magufuli.

Kabla ya kutoa kauli hiyo, Rais Magufuli alisema hatamvumilia mtu yeyote atakayetaka kuchelewesha utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ambao ulimuweka madarakani.

“Kabla sijahitimisha hotuba yangu, napenda kusema jambo moja la mwisho, kama nilivyosema hapo awali, sasa uchaguzi umekwisha.

“Ni kweli katika uchaguzi uliopita kama ilivyo kawaida kwenye nchi kuna vyama vingi, watu mbalimbali kupitia vyama vyao walijitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi na baadhi yetu tuliibuka washindi," alisema Rais Magufuli.

"Kwa mtazamo wangu na bila shaka huu ndiyo mtazamo wa Watanzania walio wengi, kwenye uchaguzi huu haukuwa na Mtanzania yeyote aliyeshinda au kushindwa.

“Sisi Watanzania wote ni washindi. Na kwa sababu sisi, Watanzania wote ni washindi, ni matumaini yangu Watanzania ninaowaongoza wanataka maendeleo, wanataka kuona kero zao mbalimbali zinaondolewa," aliongeza Rais Magufuli.

Alisema hata kama ni kwa bahati mbaya, kwa sasa serikali iliyoko madarakani ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo inahitaji kupewa muda wa kutekeleza ahadi zake kwa wananchi waliyoiweka madarakani.

”Kwa sasa hivi, iwe kwa bahati nzuri au kwa bahati mbaya, serikali inayoongoza ni ya Chama cha Mapinduzi, yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano.

Nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kuyatekeleza hayo niliyoyaahidi kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano," alisema.

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema atashirikiana na vyama vyote vya upinzani na kuzifanyia kazi hoja zao kwa maslahi ya taifa.

"Lakini ninachotaka kusema nimeamua kufanya kazi, tutashirikiana na vyama vyote katika kuhakikisha tunatatua kero za wananchi, na huo ndiyo wajibu wangu, na hili nitalisimamia kwa nguvu zangu zote,” alisema.

"Kila nchi, hata nchi zenye demokrasia, zilizobobea kwa demokrasia, unapokwisha uchaguzi, mnakuwa wachapa kazi, haiwezekani mkawa kila siku ni siasa, kila siku siasa, watu watalima saa ngapi?" Alihoji.

Alisisitiza kuwa: "Kila siku ni siasa, kila siku ni siasa. ni vyema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na wananchi wanataka maendeleo.

"Lakini napenda nikuthibitishie Mwenyekiti (wa NEC), mimi niko pamoja na wanasiasa wenzangu. Tutashirikiana na kwa nguvu zote, changamoto zao zote zenye kujenga taifa hili, nitazipokea kwa mikono yangu miwili. Ushauri wao nitaupokea kwa nguvu zangu zote, maudhui yao, tutashirikiana kwa pamoja ili Mungu aibariki nchi hii.

"Lengo letu ni kuhakikisha nchi inakwenda mbele. Ninajua wezangu wamenielewa na ninawaomba wanielewe."
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts