Mwigulu katika tanuru la moto | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

6/13/16

Mwigulu katika tanuru la moto

WAKATI Mwigulu Nchemba anaapishwa leo kuwa Waziri mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wabunge, wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa wameonya kuwa anakabiliwa na mtihani mzito.
Hali hiyo inatokana na wizara hiyo mpya atakayoanza kuiongoza leo kuwa na changamoto nzito.

Rais John Magufuli alifanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri juzi, akimteua Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk. Charles Tizeba, kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi huku aliyekuwa waziri katika wizara hiyo, Mwigulu, akihamishiwa kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mwigulu na Dk. Tizeba wataapishwa leo saa 3:00 asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam.Mwigulu anarithi mikoba ya Charles Kitwanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli Mei 20, mwaka huu, kutokana na ulevi.

Waziri huyo mteule, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) anakuwa waziri wa 27 kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tangu mwaka 1961 nchi ilipopata uhuru.

Ugumu wa wizara uko wazi kwani tangu uhuru, rekodi inaonyesha ni mawaziri wanne tu waliodumu kwenye wizara hiyo kwa muda mrefu nao ni Ali Said Maswanya (1967-1973), Muhidin Kimario (1983-1989), Augustine Mrema (1990-1994) na Ali Ameir Mohamed (1995-1999).

Wabunge na wadau mbalimbali wa masuala ya ulinzi na usalama wamebainisha ‘majipu’ ambayo Mwigulu atalazimika kuyatumbua ili kuleta ufanisi wa kazi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

MAUAJI YA KUCHINJANA
Mbunge wa Bunda (CCM), Mwita Getere, alisema anaamini Mwigulu ni waziri makini anayetumia akili nyingi katika kutatua kero mbalimbali, hivyo kuna haja aanze kwa kuitafutia ufumbuzi changamoto ya mauaji ya kuchinjana iliyoibuka katika maeneo mbalimbali nchini.

“Wizara hii ndiyo msingi wa amani. Changamoto ya mauaji yaliyoibuka ni kubwa sana. Hatukuwahi kuishuhudia hali hii, hivyo tunategemea atatusaidia kumaliza tatizo hili,” alisema Getere.

Matukio makubwa ya kuchinjana yaliyotokea nchini mwezi uliopita ni pamoja na kuuawa kwa kukatwakatwa kwa watoto wanne wa familia moja katika kijiji cha Msufini, Ndungu wilayani Same, Kilimanjaro Mei 5, mwaka huu.

Mengine ni kuuawa kwa kukatwakatwa kwa mapanga watu saba wa familia moja wilayani Sengerema mkoani Mwanza Mei 11, mwaka huu, na kuvamiwa kwa msikiti katika mtaa wa Utemini ulioko Nyamagana, Mwanza na kuchinjwa kwa waamini watatu waliokuwa ndani ya msikiti huo Mei 19, mwaka huu.

Matukio mengine ya mauaji yalitokea Mei 25, mwaka huu. Katika mauaji hayo, Aneth Msuya alichinjwa na watu ambao bado hawajakamatwa Kigamboni jijini Dar es Salaam na kuuawa kikatili kwa Saidi Simba (mume) na Kadogo Ehicho (mke) katika kijiji cha Mmazami, Butiama mkoani Mara kwa kukatwakatwa kwa mapanga.

UJAMBAZI
Getere pia alisema Mwigulu anapaswa kuja na dawa ya kumaliza matukio ya ujambazi nchini, ambayo yamekuwa tatizo sugu.

“Watu wamefikia hatua ya kuteka mabasi na kupora kwa nguvu. Apambane na ujambazi huu hatari. Tuna mategemeo atamaliza matukio haya,” alisema.

Naye Mbunge wa Sikonge (CCM), George Kakunda, alisema Mwigulu anapaswa kuwa makini katika kuishughulikia changamoto hiyo kwa kuwa baadhi ya polisi wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya ujambazi.

Kakunda alishauri kuwa Mwigulu adhibiti uingizwaji holela wa silaha nchini, hasa kwenye maeneo ya mipakani mwa nchi.

UVAMIZI VITUO VYA POLISI
Mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi anayefanya kazi mkoani Mtwara, aliliambia gazeti hili jana kuwa Mwigulu anapaswa kuja na mbinu ya kudhibiti wizi wa silaha kwenye vituo vya polisi nchini.

“Mwaka jana kulikuwa na matukio ya kuvamia kwa vituo vya polisi na kuporwa kwa silaha, sasa pametulia lakini bado hatuamini kama genge hilo la wezi wa silaha limetosheka na silaha lilizopora kwa nguvu, Waziri aje na mwaroini wa ugonjwa huu,” alisema askari huyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa jeshi.

DAWA ZA KULEVYA
Dawa za Kulevya bado ni madoa yanayolichafua taifa katika medali za kimataifa. Tanzania inatajwa na taasisi mbalimbali za kimataifa kuwa miongoni mwa njia za kupitisha dawa hizo. Waziri aliyepita alisema wafanyabiashara hiyo wanafahamika.

WAHAMIAJI HARAMU
Idara ya Uhamiaji iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa Mwigulu anakabiliwa na kazi ya kuongoza idara hiyo kukabiliana na wimbi la wageni wengi wanaoingia nchini kwa njia zisizokuwa halali.

Hata hivyo, idara hiyo katika siku za karibuni imekuwa ikiendesha operesheni za kukabiliana na tatizo hilo.

RUSHWA
Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Gulamali, aliiambia Nipashe jana kuwa rushwa ni changamoto kubwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Alisema Jeshi la Polisi ndilo linalokabiliwa na changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa kutokana na baadhi ya askari wake kuomba rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

“Mwigulu inabidi aanze kwa kupambana na rushwa. Kuna tatizo la karibu asilimia 50 wa mapato yatokanayo na makosa ya barabarani kuishia mifukoni mwa maaskari wa usalama barabarani. Wanakupa 'risiti' nyeupe ukidai ile ya njano ambayo ndiyo inakaguliwa na serikali, wanakwambia uende ukaichukue kituo cha polisi,” alisema.

MIKATABA TATA
Mwigulu anarithi mikoba ya Kitwanga huku Jeshi la Polisi ambalo katika siku za karibuni limekuwa likilalamikiwa kuingia kwenye mikataba yenye utata. Jambo hilo lililalamikiwa pia na Rais Magufuli.

Bunge linachunguza mkataba wa jeshi hilo na kampuni ya Lugumi Enterprises Limited, wa zabuni ya kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini mwaka 2011/12.

Pia kuna mkataba wa ukodishaji wa eneo la polisi la Oysterbay jijini Dar es Salaam. Mikataba yote ya jeshi hilo pia imeitishwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

MADENI
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina taasisi (Jeshi la Polisi) inayotisha kwa madeni nchini. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15, inalitaja Jeshi la Polisi ya afya kuwa miongoni mwa taasisi mbili za zinazotisha kwa madeni pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa hadi Juni 30, 2015, deni lilikuwa Sh. trilioni 1.5, huku Jeshi la Polisi likiwa na deni la Sh. bilioni 385 (asilimia 27 ya deni lote).

UDHIBITI WA KISIASA
Mbunge wa Sikonge (CCM), Kakunda, alisema Mwingulu anapaswa kuwa makini katika kudhibiti mvutano wa kisiasa unaoendelea nchini ili kulinda heshima ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa ujumla.

“Lazima aangalie sana suala hili. Mambo ya uchaguzi yameshaisha. Kusiwe na watu wanaoendeleza siasa katika kipindi ambacho tunatakiwa kuwatumikia wananchi,” alisema Kakunda.

Hata hivyo, hivi karibuni Mbunge wa Ole (CUF), Juma Hamad Omar, alilitupia lawama Jeshi la Polisi kwa kutumiwa chama tawala kudidimiza demokrasia, hasa wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.

VIONGOZI WENGINE WANAMZUNGUMZIAJE
LEMA

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema katika taarifa yake jana kuwa Nchemba anapaswa kuwa makini, mwangalifu na mtulivu.

“Jambo la kwanza utakalofanya ni kutambua kuwa, wingi wa silaha za kisasa kwa askari wetu sio suluhisho la ulinzi na amani katika taifa letu bali haki na matumaini ya wananchi ndiyo msingi mathubuti wa amani na utulivu wa nchi,” alisema Lema ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani.

Aliongeza kuwa polisi na askari magereza wanaishi maisha magumu, mishahara haitoshi hivyo wanahitaji uelewa wa waziri juu ya maisha yao na kazi zao.

“Umeteuliwa wakati Serikali kupitia Jeshi la Polisi, inatumia nguvu zote kukandamiza na kuangamiza demokrasia, vyama vya Siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa sababu ambazo hazina msingi wowote, kinyume cha sheria na Katiba ya Nchi,” aliongeza Lema.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alionya kuwa wizara hiyo ni ngumu na kupewa ni sawa na kufukuzwa kazi kwa kuwa changamoto kubwa iko kwenye Jeshi la Polisi ambalo linahusika na maisha ya watu ya kila siku na limekuwa likilalamikiwa.

Alisema mambo anayopaswa kuyasimamia kwa karibu ni rushwa, ambayo imeota mizizi ndani ya jeshi hilo ambalo linalalamikiwa kuonea raia kwa kuwabambikia kesi za silaha, madawa ya kulevya ambayo wanayo.

Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema hatua ya Rais Dk. John Magufuli kumhamisha Mwigulu kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi si jambo zuri.

Alisema Wizara hizo ina milengo inayotofautiana katika utendaji wa kazi, alisema Mwigulu atapata kazi ya kujifunza kwa muda mrefu kwa sababu ni wizara iliyo na mambo mengi na changamoto kubwa.

“Mwigulu haijui sana Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, hivyo itamlazimu apate muda mwingi ajifunze, tofauti na mawaziri wengine,” alisema Mghwira.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia, Dk. Watengere Kitojo, alisema Mwigulu amewahi kuwa katika idara mbalimbali za serikali kabla hajateuliwa nafasi hiyo .

“Sina shida na Mwigulu, ni mtu anayeijua vizuri serikali, na ni mchapakazi, kikubwa apewe nafasi na muda ni imani yangu ataibadilisha Tanzania,” alisema Dk. Kitojo.

Orodha ya Mawaziri wa Ndani ya Nchi tangu uhuru

Walioingoza wizara hiyo kipindi cha Mwalimu Julius Nyerere cha Serikali ya Awamu ya Kwanza ni Sir George Kahama (1961), Oscar Kambona (1962), Lawi Sijaona (1963-1965), Job Lusinde (1966), Said Maswanya (1967-1973), Omar Muhaji (1973-1974), Ali Hassan Mwinyi (1975-1976), Hassan Nassoro Moyo (1977-1978), Salim Amour Juma (1979- 1980), Abdallah Natete (1980-1983) na Muhidin Kimario (1983-1985).

Kipindi cha uongozi wa Mwinyi, wizara hiyo iliongozwa na Kimario (1985-1989), Nalaila Kiula (1990), Augustino Mrema (1990-1994) na Ernest Nyanda (1994-1995).

Katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Benjamin Mkapa, wizara hiyo ilikuwa chini ya mawaziri Ali Ameir Mohamed (1995-1999), Muhammed Seif Khatib (2000- 2002) na Omar Ramadhani Mapuri (2003-2005).

Katika miaka 10 ya utawala wa Jakaya Kikwete, mawaziri wa wizara hiyo walikuwa John Chiligati (2006), Joseph Mungai (2006-2008), Lawrence Masha (2008-2010), Shamsi Vuai Nahodha (2010-2012), Emmanuel Nchimbi (2012-2013) na Mathias Chikawe (2014-2015).

google+

linkedin