Rage Aionya Yanga | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

6/28/16

Rage Aionya Yanga
WAKATI mashabiki wa Yanga leo wakisubiri kwa hamu kuwaona nyota wake waliosajiliwa hivi karibuni, kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC) dhidi ya TP Mazembe, timu hiyo imetahadharishwa kutowatumia wachezaji wapya waliotoka Ligi Kuu Tanzania bara.

Mwenyekiti wa zamani wa Simba Ismail Rage aliliambia gazeti hili jana kuwa wachezaji wanne ambao ni Hassan Kessy, Juma Mahadhi, Ben Kakolanya na Vicent Andrew hawana leseni ya kuwaruhusu kucheza michuano hiyo.

Kwa mujibu wa Rage, Sheria ya usajili ya michuano ya Kombe ya Shirikisho namba nne na tano inaonesha wazi kuwa wachezaji hao hawaruhusiwi kucheza kama hawajapewa leseni na Kamati ya sheria na usajili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“Kwa mujibu wa sheria hizo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) suala la usajili lina sehemu mbili. Wachezaji wanatakiwa kusajiliwa kabla ya Januari 15 au kabla ya Agosti 10, ndipo waruhusiwe,”alisema.

Rage alifafanua kuwa Yanga baada ya kufuzu michuano hiyo mapema, TFF kama ilikuwa inataka kuwasaidia wawakilishi hao wa Tanzania, Rais wake (Jamal Malinzi) alitakiwa kuitisha kikao cha dharura kufanya marekebisho ya kanuni za usajili kuisaidia timu hiyo kupata leseni za wachezaji wake mapema.

Lakini kwa vile walishindwa kufanya hivyo, alisema sheria zinaeleza kuwa ili wachezaji hao waruhusiwe kucheza ni lazima wapitishwe na kamati hiyo ya TFF.

Alisema hadi sasa kamati hiyo haijakaa kwani utaratibu wao uliopo ni hadi kusubuiri dirisha la usajili lifungwe kisha ikae na kupitia majina ambayo hayana pingamizi na ndipo iwaruhusu wachezaji hao.

Rage ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa FAT, (Sasa TFF) alisema sehemu ya pili ya kifungu cha usajili ya CAF inataka timu ifanye usajili wa wachezaji saba, na Yanga ina wachezaji 23 pekee, tayari imesajili wanne bado watatu na kuhoji je, itawapata wapi?.

Licha ya Rage ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais chini ya uongozi wa Leodegar Tenga mwaka 2004 alisema: “Ni lazima wawe makini kwenye hilo wasipoangalia inaweza kuwagharimu”.

Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa tayari TFF imempatia leseni Kessy kumruhusu kucheza huku kukiwa hakuna taarifa za kamati hiyo kukutana.

Mdau huyo wa soka alisema Kessy na wenzake wanaweza kuruhusiwa kucheza na CAF, lakini iwapo kutakuwa na matatizo baadaye kutoka kwenye klabu zao, Shirikisho hilo la soka la Afrika halitaweza kuwasaidia. Mchezaji anayeruhusiwa kucheza ni Mzambia Obrey Chirwa.

google+

linkedin