6/27/16

Saruji kuuzwa bei nafuu Julai
KAMPUNI ya kuzalisha saruji ya Dangote ya Mtwara imesisitiza azma yake ya kuuza saruji kwa gharama nafuu, kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu ujenzi wa makazi bora.

Akizungumza katika maonesho ya bidhaa za Kiafrika “ARSO Made in Africa Expo” yaliyofanyika jijini Arusha hivi karibuni, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Sadaladan Baki alisema kampuni ya Dangote tayari imeshaingiza saruji yake yenye ubora wa kimataifa na inayouzwa kwa gharama nafuu sokoni.

Alisema, kuanza uzalishaji kwa kiwanda cha Dangote kumeleta matumaini mapya kwa wananchi wa kipato cha chini na kusisitiza kuwa uwekezaji mkubwa wa Dola za Marekani milioni 600 uliofanywa kwenye kiwanda hicho, utawezesha kupatikana kwa saruji bora na ya gharama nafuu.

Mkurugenzi huyo alisema saruji aina ya 32.R ya ujazo wa kilo 50 inauzwa kwa Sh 10,000 kwa bei ya rejareja, wakati saruji aina ya 42.5R ya ujazo huo huo inauzwa Sh 10,500.

Takwimu zinaonesha kuwa, sekta ya ujenzi imekuwa kwa asilimia 12.5 kutokana na mahitaji ya saruji kuongezeka pamoja na wananchi kuhamasika kujenga nyumba bora, suala ambalo pia limechangia kuongezeka kwa mahitaji ya saruji.

Alisema mahitaji ya saruji kwa sasa nchini yanakadiriwa kufikia tani milioni tatu kwa mwaka wakati viwanda vya ndani vikiwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts