Serikali yaahidi kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

6/21/16

Serikali yaahidi kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri

SERIKALI imesema itaendelea kuwawekea vijana mazingira wezeshi ili kuwa na uwezo wa kujiajiri wenyewe pindi wamalizapo kozi mbalimbali na kuibua shughuli za kiuchumi katika maeneo yao.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya wiki mbili kwa wakufunzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa ajili ya kuwafundisha vijana wanaojiunga na jeshi hilo, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Hamis Mwinyimvua, alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha vijana wanatengenezewa mazingira bora ya kujiajiri na kwamba mafunzo hayo ni hatua ya kufikia lengo hilo.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

“Lengo kubwa la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wakufunzi hawa ili wawe na uelewa mpana wa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana wetu,” alisema Dk. Mwinyimvua.

Alisema nia ni kuhakikisha vijana wengi wanakuwa na fikra ya kujitegemea na kuondoka katika dhana ya utegemezi mara wamalizapo mafunzo katika vyuo mbalimbali hapa nchini.

“Tunataka kufuta dhana ya kufikiria ajira kwa vijana hawa,” alisema na kueleza kuwa kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji wananchi, watahakikisha vijana wengi wanafikiwa katika maeneo yao.

Naye Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, alisema mpaka sasa wakufunzi 150 kutoka katika kambi 17 za Tanzania wamepatiwa mafunzo hayo ya ujasiriamali.

“Tunategemea baada ya miaka mitano, tutakuwa tumefikia zaidi ya vijana elfu thelathini na tano kwa nchi nzima,” alisema.

Aliongeza kuwa mpango uliopo sasa ni kutoa mafunzo kwa wakuu wote wa kambi kwa nchi nzima ili waelewe mpango huo ambao ni mkakati wa serikali kuhakikisha dhana ya ujasiriamali inaenea katika majeshi.

“Mara baada ya kumalizika kwa program hii ya kutoa mafunzo kwa wakufunzi, tutageukia kwa wakuu wote wa kambi,” alisema.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa, Kanali Chacha Wanyancha, aliishikuru serikali kupitia NEEC kuwa wamefanya jambo kubwa kwa jeshi hilo.

“Niwapongeze sana, hili si jambo dogo, ni mfano wa kuigwa na taasisi nyingine hapa nchini,” alisema.

Kanali Wanyancha alisema kama juhudi hizo zitafanyika kwa vijana wengi hapa nchini, taifa litakuwa limefanya juhudi za kujikomboa kiuchumi.

“Vijana watakaozingatia haya watafaidika, hii ni fursa kubwa sana kwa vijana wetu,” aliongeza Kanali Wanyancha.

google+

linkedin