6/24/16

Simu kuokoa maisha ya mama, mtoto Dar
Kamati ya afya mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na Hospitali ya CCBRT imedhamiria kuboresha huduma za rufaa kwa kutumia mawasiliano ya simu za viganjani katika vituo vya afya kwa lengo la kuokoa maisha ya mama na mtoto.


Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa, Raymond Mushi alisema ubunifu huo ambao ni mpya utasaidia kwa kiasi kikubwa changamoto za msongamano wa wajawazito katika hospitali za rufaa, ambao wangeweza kutibiwa katika vituo vya maeneo yao, jambo ambalo limekuwa likidhoofisha utoaji wa huduma.


Alisema Dar es Salaam ina wakazi wengi, jambo ambalo linaongeza ukubwa wa tatizo la vifo vya mama na mtoto na endapo hakutakuwepo na jitihada za makusudi, tatizo hilo litakuwa sugu.


“Wabunifu wa huduma hii ya mawasiliano kutoka kituo kimoja na kingine wamefanya jambo zuri ambalo licha ya idadi kubwa ya watu jijini (Dar) wametuhakikishia kuwa huduma za mama na mtoto zitakuwa imara zaidi kwa siku zijazo,” alisema Mushi ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Ilala.


Meneja mradi wa CCBRT, Dk Brenda D’mello alisema huduma hiyo itapambana na tatizo la mawasiliano hafifu kati ya zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuondoa rufaa za wagonjwa zisizokuwa na mipangilio ambazo husababisha kucheleweshwa kwa huduma za matibabu kwa wagonjwa.


Alisema mfumo huu utatumia teknolojia ya simu ya mkononi na na mfumo maalum wa watumiaji (closed user group) ambapo vituo 23 na magari saba ya wagonjwa ofisi za waganga wakuu wa wilaya na mkoa wataunganishwa katika mfumo huo ili kuweka mawasiliano ya karibu na kuboresha huduma ya mama na mtoto.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts