6/28/16

Tujifunze kuvunjwa kwa bodi ya TCU
Mwezi uliopita, Serikali kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ilivunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ( TCU) na kuwasimamisha watendaji wake kadhaa.


Serikali iliwasimamisha watendaji hao baada ya kubaini kuwa Chuo Kikuu cha St Joseph kilidahili wanafunzi 486 katika kampasi za Arusha na Songea wasio na sifa kusoma shahada, huku wakipata mkopo wa Serikali.


Profesa Ndalichako alisema kuna wanafunzi katika vyuo wasio na sifa ambao wanasoma kwa mikopo ya Serikali na kwamba itawasaka popote walipo.


Baada ya uamuzi huo wa Serikali, swali kuu lilibuka, je, bodi ya TCU na watendaji wake walikosea au mfumo mzima wa elimu nchini ndiyo wenye matatizo?


Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Catherine Sekwao anasema hatua iliyochukuliwa na Serikali ya kuivunja bodi ilikuwa sahihi baada ya mambo kuharibika.


Anasema wanasiasa ndiyo wameifikisha elimu hapo ilipo kwa kufanya maamuzi yenye kuwashinikiza wataalamu, lakini mambo yanapoharibika wanawawajibisha.


Anasema kulikuwa na kila sababu ya bodi ya TCU kuvunjwa kwa sababu wao ndiyo wasimamizi wa ubora wa vyuo hivyo.


“Tume ya TCU ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia, kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa vyuo vikuu hapa nchini, hapo hata kama ulishinikizwa na mwanasiasa, mtaalamu ndiye unayewajibishwa,” anasema.


Sekwao anasema ili kusoma shahada inajulikana wazi kwamba lazima uwe umefika kidato cha sita na kufaulu.


Kwa mwanafunzi anayemaliza kidato cha nne na kufaulu anatakiwa kusoma stashahada na kufanya vizuri.


“Huwezi kumaliza kidato cha nne na kuanza kusomea shahada,” anasema.


Hata hivyo, anasema aliyefika kidato cha nne na kufaulu vizuri anaweza kusoma stashahada na baadaye shahada. Anasema ndivyo mfumo unavyoonyesha na ndiyo maana Serikali imeivunja tume hiyo kwa kutosimamia hilo.


Anasema wanafunzi walisimamishwa masomo hawana makosa kwa sababu walidahiliwa na kupewa mikopo. “Ni nani anaweza kuikataa fursa hiyo, wamedahiliwa na wakakaribishwa vyuoni kusoma,” anasema.


Anasema wakati umefika kwa wanasiasa kuwatumia wataalamu kupata ushauri kuhusu masuala mbalimbali na wataalamu wasiogope kuwaeleza ukweli viongozi.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa wa Kitila Mkumbo anasema mtu anaweza kusomea shahada hata kama amefika darasa la saba lakini akaonyesha umahiri katika eneo fulani.


Akitoa mfano, anasema mwanamuziki akionekana ni mahiri katika eneo hilo, seneti ya chuo inaweza kukaa na kujadili ikamruhusu kusoma chuo kikuu.


“Kwa mfano wanamuziki kama Diamond akionekana amefanya vizuri katika muziki anaweza kusoma na akapata shahada,” anasema na kuongeza kuwa si mara nyingi utaratibu huo kutumika.


Hata hivyo, anasema vyuo vikuu vilivyokutwa na wanafunzi wasio na sifa ndivyo vinavyotakiwa kulaumiwa kwa sababu ndivyo vyenye mamlaka ya kusimamia udahili wanafunzi.


“Vyuo hivi vina seneti na menejimenti yake, iweje vichukue wanafunzi wasio na sifa, vinajiendesha kiujanjaujanja ili kupata ada,” anasema.


Anasema ni kweli TCU inatakiwa kusimamia viwango lakini suala la udahili linatakiwa kusimamiwa kikamilifu na vyuo vyenyewe.


Anasema kwa mfumo ambao Rais John Magufuli anataka ufuatwe, baadhi ya vyuo binafsi vitafungwa kwa kukosa wanafunzi wenye sifa.


“Ujanjaujanja huu ukidhibitiwa watafunga vyuo kwa sababu wanafunzi wenye sifa ni wachache,” anasema.


Anawataka viongozi wa vyuo vikuu nchini kutoingiliwa na viongozi wa Serikali katika shughuli zao hasa za kitaaluma.


“Maprofesa acheni kuingiliwa na viongozi wa Serikali, mna sheria zenu kanuni na vyombo vya maamuzi mkiruhusu hali hiyo iendelee kukitokea makosa ndio wa kulaumiwa,” anasema.


Mtazamo tofauti


Mchambuzi wa masuala ya elimu, Philip Mwakibinga anasema wanafunzi hao wamehukumiwa kwa makosa yasiyowahusu na kuiomba Serikali kuwarudisha vyuoni.


“Kama kumetokea matatizo wanafunzi siyo wa kulaumiwa, wameshapoteza muda wao kinachotakiwa ni kuwaacha waendelee na udhibiti uanze lakini ya kuwafukuza,” anasema.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala anasema ngazi za elimu zinatakiwa kufuatwa na siyo kupita njia za mkato.


Anasema tangu enzi za utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ngazi za elimu zinajulikana kwa watu wengi.


Anasema ukimaliza kidato cha nne na kushindwa kufaulu vizuri unasomea astashahada, kisha stashahada na baada ya kufaulu na ndipo unasomea shahada.


Anasema vyuo vinavyotoa ngazi hizo za elimu vipo vingi lakini siku hizi vinakosa wanafunzi kwani wengi wanataka kusomea shahada.


“Nadhani Rais wetu anataka kurudisha heshima ya elimu ambayo ilikuwepo tangu wa Serikali ya awamu ya kwanza,” anasema.


Anasema hakuna njia ya mkato katika kutafuta elimu bali kufuata ngazi zilizowekwa kisheria.


Anaungana na wenzake kusema mfumo wa elimu uliopo ni mzuri, isipokuwa usimamiaji ndiyo wenye matatizo.


Mtemi Zombwe ambaye ni mchambuzi wa masuala ya elimu anasema TCU imekuwa mwathirika wa siasa kwa sababu wasomi hawashauri hata kama wanaujua ukweli.


“Wasomi wetu wananywea hata kama wanaujua ukweli,” anasema.


Anasema kuna baadhi ya watu waliohitimu shahada ya uzamili ambao wakiitwa kwenye usaili inashangaza kama wamepitia ngazi zote za elimu kwa sababu wanashindwa hata kujieleza wao wenyewe.


Anachokifanya Rais Magufuli ni mapinduzi katika elimu, hivyo inabidi asaidiwe na wenye nia safi.


“Ni lazima tusafishe huu mtindo wa mtu amefika kidato cha nne na kufeli masomo, lakini baada ya miezi michache unamkuta kwenye darasa la mafunzo ya shahada,” anasema.


Anashauri wasomi kuacha kusikiliza matamko ya wanasiasa wenye kutaka idadi kubwa ya vyuo lakini visivyokuwa na ubora.


“Wanasiasa wanataka idadi kubwa ya shule na vyuo, wasomi ni lazima tusimame tuwaambie hili hapana,’’ anasema.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts