6/3/16

‘Tutawarudisha wote tuliowatoa mkopo’-Azam FC

KLABU ya Azam FC imewarudisha wachezaji wake wote iliowapeleka kwa mkopo katika timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kwa ajili ya kuangaliwa na kocha mpya, Mhispania Zeben Hernandes kwa tathmini ya mwisho kabla ya kuuzwa kabisa.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Katibu Mkuu wa Azam, Idrissa Nassoro, alisema wachezaji hao, Bryson Raphael aliyekuwa Ndanda FC, Kelvin Friday aliyekuwa Mtibwa Sugar, Ismail Gambo aliyekuwa Mwadui na Joseph Kimwaga aliyekuwa Simba tayari wamesharudi.

Alisema licha ya timu hizo kuonesha nia ya kutaka kubaki nao kwa ajili ya msimu ujao, wameona warudi kwanza na kushiriki na wenzao kwenye mazoezi yatakayoanza rasmi Julai mwaka huu kwa tathmini ya kocha mpya kuona kama wabaki au wauzwe.

“Tumewarudisha kwanza ili wafanye mazoezi na kocha kisha atawaangalia tena kwa tathmini yake kama wabaki Azam au waendelee na timu nyingine,” alisema Nassoro.

Alisema pia, kuna idadi kubwa ya wachezaji watakaopunguzwa na wengine wa kusajiliwa tayari wamepatikana na kwamba watawekwa wazi kuanzia Julai.

Katika hatua nyingine, klabu hiyo ilisema inatarajia kuwapandisha wachezaji wanne vijana kucheza timu kubwa msimu ujao baada ya kuonekana kufanya vyema katika michuano mbalimbali.

Kocha Mkuu wa timu ya vijana Tom Leg aliwataja wachezaji waliopendekezwa kupandishwa kuwa ni Shaban Idd, Masoud Abdallah, Prosper Mushi na Optatus Lupekenye.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts