6/24/16

Ulimwengu aionya YangaMSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Thomas Ulimwengu, amesema hukumu ya kifungo aliyopewa mmiliki wa timu hiyo, bilionea Moise Katumbi haitaathiri ushiriki wao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.Mazembe wanatarajia kutua nchini Jumapili wiki hii tayari kwa mchezo dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 28.

Akizungumza Nipashe jana kwa simu kutoka Lubumbashi, Ulimwengu alidai kuwa hukumu hiyo yenye mrengo wa kisiasa, haina nguvu ya aina yoyote kuathiri ushiriki wao kwenye mashindano na kwamba wamejiandaa vizuri kupata ushindi dhidi ya Yanga.

Straika anayecheza timu ya Taifa - Taifa Stars, alisema pamoja na hali ya kisiasa nchini humo kutotulia, lakini bado waliweza kutwaa Taji la Ligi Kuu.

"Hukumu yake sisi haituathiri kabisa. Bosi wetu bado yuko karibu na timu na hata jana (juzi), katika mechi ya kutangaza ubingwa tulizungumza naye na alitupa pongezi," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Moro United.

Alisema kama Yanga wanadhani hukumu hiyo inaweza kuwafaidisha katika mechi inayofuata, basi wajiandae na kipigo.

Kuhusu mchezo huo, Ulimwengu alisema wamejiandaa vizuri na hakuna mchezaji yeyote wanayemhofia kutoka Yanga.

"Sitaki kuzungumzia mchezaji mmoja mmoja. Naamini kila mchezaji ana madhara yake uwanjani kutegemeana na uwezo wake, lakini kwetu TP Mazembe hatujaona mchezaji wa kutunyima usingizi Yanga. Tunakuja kucheza kwa lengo moja tu la kusaka ushindi," alisema Ulimwengu.

TP Mazembe ndio inaongoza Kundi A ikifuatiwa na Mo Bejaia, Yanga na Medeama.

Bilionea Katumbi alihukumiwa na Mahakama ya Lubumbashi kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini Sh. bilioni 12 baada ya kupatikana na hatia ya kuuza ardhi iliyokuwa ikimilikiwa na raia wa kigeni.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts