6/12/16

UVCCM - Arusha waishukia Chadema tuhuma udikteta

Umeibuka na kuibua shutuma dhidi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kudai kuwa hawataki mageuzi ya kweli yanayoendelea kuletwa na Serikali ya awamu ya tano kwa sababu ya madai yao kuwa serikali ina dalili za kufanya maamuzi ya kidikteta.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai Ole Sabaya, ndiye aliyesema hayo juzi mjini Arusha, akidai kuwa kitendo cha Chadema kudai kuwa serikali inaendeshwa kidikteta na kwamba inaminya demokrasia ni dalili za wazi kuwa chama hicho (Chadema) hakina nia ya dhati ya kuona taifa linapata mageuzi ya kweli kupitia jitihada zinazoendelea kufanywa chini ya Rais John Magufuli.

Sabaya alidai kuwa Chadema na wote wanaotoa madai hayo ni watu wanaotaka kudhoofisha mapambano dhidi ya ufisadi na pia kukwaza mageuzi ya kweli, hasa katika uchumi na nidhamu ya kazi serikalini.

Sabaya alisema kuwa inavyoonekana, kuna viongozi wa Chadema wanakerwa na vita iliyoanzishwa na serikali ya Rais Magufuli katika kutokomeza rushwa na ufisadi kwa sababu chama hicho kimeanza kutoa kauli zenye dalili za kuwatetea wezi na mafisadi.

"Ikiwa Rais Dk. Magufuli anatafsirika kuminya demokrasia kwa kupambana na wezi, mafisadi na kupinga wonevu, ni heri ifahamike anakandamiza demokrasia… lakini kama anawakomesha wala rushwa, wabadhirifu , wezi na wakwepa kodi halafu wao wanadai ni dikteta kwa kuchukua hatua hizo, ni ruksa aitwe dikteta," alisema Sabaya.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema hadi sasa hajafahamu kama Chadema ina malengo gani kwa sababu hawaonyeshi kuwa na mwelekeo maalum na badala yake hutoa matamko yanayoashiria kuwa wao ni kama popo ambao huwa na baadhi ya sifa zinazofanana na kundi la ndege na wanyama kwa wakati mmoja.

"Ni nani anayewapa Chadema ujasiri wa kupingana na utakatifu wa Mungu? Kupigania haki, kutetea wanyonge, kukomesha rushwa na wezi ni kazi ya kumtumikia Mungu… ieleweke kuwa Dk. Magufuli ni chaguo la Mungu," alieleza Sabaya.

Katika hatua nyingine, Sabaya alisema umoja wao unalaani hatua ya Chadema ya kutaka kuitisha mikutano ya hadhara bila kufuata utaratibu kwa sababu kufanya hivyo ni kutotii sheria za nchi na pia ni dalili ya kufilisika kwa hoja.

"Tunamtaka Rais Magufuli aendelee na dhamira yake ya kuisafisha nchi yetu, awakabili mafisadi na wasaliti walioko ndani na nje ya serikali yake," alisema Sabaya.

Hivi karibuni, Chadema, kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani vikiwamo vya ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (CUF), wamekuwa wakilalamikia baadhi ya maamuzi ya serikali kwa kudai kuwa ni ya kibabe na pia yana ishara ya udikteta.

Chadema na washirika wao wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamekuwa pia wakilalamikia maamuzi ya Naibu Spika Dk. Tulia Ackson wanayedai huwabana ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria kwa minajili ya kuibeba serikali na kwa sababu hiyo, hivi sasa wamekuwa wakitoka nje ya Bunge katika vikao vyote vinavyoongozwa na kiongozi huyo (Dk. Tulia).
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts