Wacharazwa viboko 15 na kulipa Sh. 50,000 kwa kwenda baa na watoto | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

6/21/16

Wacharazwa viboko 15 na kulipa Sh. 50,000 kwa kwenda baa na watoto


WANAWAKE wawili wakazi wa Kijiji cha Sanya Hoye, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wamekamatwa na kucharazwa viboko 15 na kulipa faini ya shilingi 50, 000 baada ya kukiuka sheria za serikali ya kijiji hicho inayokataza wazazi na walezi kwenda baa na watoto chini ya miaka 18.
Aidha, serikali ya kijiji hicho pia imetangaza adhabu nyingine ya viboko 10, kwa watu watakaobainika kutumia vibaya fedha za kusaidia kaya masikini zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Uamuzi wa kuwashughulikia wanaofanya anasa ikiwamo ulevi, kwa kutumia fedha hizo za kusaidia watu wasiojiweza kujikwamua kiuchumi, uliasisiwa juzi na wanufaika wenyewe wa Tasaf ambao wamejitungia sheria ndogo ya kudhibitiana ili kila mmoja aone manufaa ya kusaidiwa.

Wazazi hao (majina yamehifadhiwa), walianza kutumikia adhabu hiyo Jumamosi iliyopita walipokutwa wakiwa baa na watoto, kinyume na maazimio ya mkutano mkuu maalumu wa kijiji hicho uliopitisha utekelezaji wa adhabu ya viboko na faini.

Juzi, Nipashe wakati ikifuatilia sakata la kucharazwa viboko kwa wanawake hao wawili (majina yamehifadhiwa), ilipokea taarifa nyingine za kupitishwa kwa sheria ndogo ya kuwabana wanufaika wa Tasaf waliopo kwenye mpango huo.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Mosses Munuo alithibitisha kuwapo kwa mkakati maalumu wa kuwadhibiti watu wasiojiweza wasitumie vibaya fedha hizo kwa kunywa pombe na kufanya matumizi mengine ya anasa kwa kuwa siyo malengo ya Tasaf kwa jamii ya watanzania.

“Ni kweli hao wanufaika wametengeneza wenyewe sheria yao ya kudhibitiana ili kusaidiana na wafanye jambo la maana la kujikwamua na umasikini. Kimsingi wameweka masharti yao kwamba atakayekutwa akizinywea pombe achapwe viboko 10 kama onyo la kwanza na akirudia wanaufaika wenyewe wataishauri Tasaf kumuondoa mwenzao kwenye mradi huo,” alisema Munuo.

Nipashe limeelezwa kwamba tayari, watu watatu ambao ni wanufaika wa mradi huo wa Tasaf wanadaiwa kuzitumbua kwa kunywea pombe na kikao cha wanufaika hao kimeamua watafutwe na watumikie adhabu yao.

Alisema wanufaika wa Tasaf wanaodaiwa kupata fedha hizo na kuzinywea pombe walilipwa kati ya Sh. 35,000 hadi 40,000.

Mwezi Mei, mwaka huu kijiji hicho kilitangaza kuanza kutekelezwa kwa adhabu hiyo, kwa kile kinachodaiwa ni malezi mabaya ya wazazi au walezi, baada ya watoto kutoka shule. 
 
NIPASHE

google+

linkedin