6/12/16

Wasomi kuichambua Bajeti leo

KIONGOZI wa Chama Cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, leo atawaongoza wasomi na wachambuzi mbali mbali wa masuala ya uchumi na wananchi wa kawaida katika kongamano maalum la wazi la mapitio ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017.

Kongamano hilo linalosimamiwa na ACT-Wazalendo, linafanyika ikiwa ni siku chache zimepita tangu serikali kuwasilisha bungeni bajeti yake ya Sh. trilioni 29.5. Sh. trilioni 17.719 zimeelekezwa katika matumizi ya kawaida.

Tayari maoni mbali mbali yameshatolewa, huku baadhi wapinzani wakiita kuwa ni bajeti hewa kutokana na kuainisha uhalisia wa kitabu cha mapato ya serikali kinachoonyesha jumla ya mapato ya serikali ni Sh. trilioni 22.063.

Kwa mujibu wa afisa habari wa Chama cha ACT-Wazalendo, Abdallah Khamis, kongamano hilo litafanyika katika Ukumbi wa Millenium Towers, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, kuanzia saa saba mchana.

Mbali na Zitto, wachangiaji wengine watakuwa ni pamoja na Godfrey Mwang’onda, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar esSalaam, Profesa Kitila Mkumbo na Mwenyekiti wa Chama hicho Mama Anna Mghwira.

Khamis alieleza kuwa wachambuzi katika kongamano hilo watachambua bajeti iliyowasilishwa na serikali bungeni pamoja na kuainisha njia mbadala za kuhakikisha Bajeti hiyo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi shirikishi na ustawi wa jamii, kwa kuzingatia misingi ya usawa, uwajibikaji demokrasia na uongozi bora.

“Dhama kuu itakayoongoza uchambuzi ni ujenzi wa taifa lenye kujitegemea kwa kuzingatia misingi ya Ujamaa wa Kidemokrasia ambayo ndiyo itikadi ya chama chetu,” alisema Khamis.

Wakati huo huo, Khamis alisema wamemuandikia barua Mwenyekiti wa Kituo cha Demokria Tanzania (TCD) ili aingilie kati ukandamizwaji unaofanywa na serikali ya awamu ya tano kupitia mwavuli wa Jeshi la Polisi.

“TCD inapaswa ionyeshe nafasi yake katika hili, isiwe ya kukutanisha vyama katika sherehe huku matatizo yakijitokeza yenyewe inakaa kimya,” alisema.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts