7/7/16

Afya: Toka Jasho Angalau Dakika 30 Kila SikuKUISHI ni jambo moja na kuishi maisha yenye afya njema ni kitu kingine. Hakuna anayeweza kueleza ukweli wa hilo zaidi ya waliopata athari za magonjwa yasiyoambukiza.

Wananchi wengi wenye umri mkubwa na watoto ni waathirika wanaoteseka kwa sababu ya magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa yasiyoambukiza hayasambai kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusu magonjwa hayo. Magonjwa hayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kisukari, figo, saratani, kifua sugu, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi ukiwemo ugonjwa wa selimundu.

Kwa bahati mbaya, licha ya mipango mikakati ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza nchini, Watanzania wengi bado wanaathirika na wengine kupoteza maisha. Daktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, Profesa Andrew Swai anasema, takwimu za kidunia za mwaka 2012 zinaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza yalisababisha vifo milioni 56.

Daktari huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania, anasema, kati ya vifo hivyo, milioni 38 ambavyo ni asilimia 68 vilitokana na magonjwa yasiyoambukiza na vingine milioni 16.9 sawa na asilimia 40 ni vya mapema. Anasema watu milioni 28 ambao ni asilimia 75 ya vifo hivyo wameaga dunia katika nchi zinazoendelea. Asilimia 82 ya vifo vya mapema vimetokea nchi hizo. Magonjwa yaliyochangia vifo hivyo ni moyo (asilimia 48), saratani (asilimia 21), magonjwa ya kudumu ya upumuaji (asilimia 12) na kisukari asilimia 3.5.

“Theluthi mbili ya kansa zilizoua katika nchi zinazoendelea na masikini ni ya mapafu, matiti, utumbo na ini huku asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari wanaishi nchi masikini. “Idadi ya watu wanaokufa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza imekuwa ikiongezeka mara mbili ukilingnisha na vifo vya magonjwa yanayoambukiza ikijumuisha HIV/ AIDS, kifua kikuu na malaria,” anasema Profesa Swai.

“Tatizo la magonjwa yasiyoambukiza linakuwa kwa kasi katika nchi zinazoendelea kama Tanzania. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 magonjwa haya yatasababisha asilimia 73 ya vifo vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani,” anasema. Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Tatizo Waane anasema Watanzania kwa sasa wanakabiliwa na mzigo mara mbili wa magonjwa yakiwemo ya kuambukiza na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.

Anasema kasi ya magonjwa yasiyoambukiza imeongezeka. Waane anasema, kuna ongezeko la kasi la magonjwa na vifo hata miongoni mwa vijana vinavyohusishwa na matatizo kadhaa kwenye kundi hilo. Anasema, magonjwa yasiyoambukiza yanakaribia kuyapita yale ya kuambukiza kama vile malaria, HIV na TB hasa kutokana na uratibu, udhibiti na uzuiaji vinavyohitaji rasilimali nyingi hasa fedha.

Waane anatoa mfano wa gharama za matibabu kwa matumizi ya huduma za afya kwa mgonjwa ya kisukari kuwa ilikuwa ni wastani wa dola za Marekani bilioni 465 kwa mwaka 2011 wakati mgonjwa alipotumia dola za Marekani 1,274. Anasema mwaka 1991, asilimia 9 ya bajeti yote ya afya ilikuwa ikihitajika kutumika kuwahudumia wagonjwa wa kisukari pekee. Kwa mujibu wa Waane, mambo yanayochangia kuongezeka magonjwa hayo ni mabadiliko ya taratibu za kimaisha ikiwa ni pamoja na kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, unywaji pombe, matumizi ya tumbaku, dawa za kulevya na msongo wa mawazo.

“ Watu kukaa darasani, ofisini kuangalia runinga, kutumia lifti, kupanda magari hata eneo la umbali mfupi, zinafanya mwili usichome chakula kilicholiwa hivyo kuenda kuweka mafuta mwilini ambayo yanachangia ongezeko nishati isiyotumika mwilini,” anasema. Waane anatoa mfano wa utafiti wa mwaka 2003 katika shule nchini, unaoonesha kuwa wanafunzi mijini walikuwa na uzito mkubwa ukilinganisha na wa vijijini kwa sababu ya taratibu za maisha.

Anasema magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kuwepo bila dalili zozote kwa miaka kadhaa lakini mwili utakuwa umeathirika. “Mtu anaweza kuishi miaka mingi na shinikizo kubwa la damu bila dalili zozote hadi pale anapopata kiharusi, moyo unaposhindwa kufanya kazi au figo zinapokuwa zimeharibika kwa sababu ya huo msukumu wa damu,” anasema. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 nchini na kushirikisha watu wenye umri wa miaka 25 na kuendelea, ulionesha kuwa kati ya watu 14 waliokutwa na shinikizo la damu ni mmoja tu ndiye aliyekuwa tayari amegunduliwa.

Pia kwa upande wa ugonjwa wa kisukari chini ya nusu ya watu wote waliokutwa na ugonjwa ndio waliokuwa wamegunduliwa mapema. “Hivyo watu wanashauriwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kugundua kuwepo kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” anasema. Waane anasema jambo litakalosaidia kupunguza ukuaji wa kasi wa magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha.Ulaji unaofaa ni pamoja na kula chakula mchanganyiko, cha kukutosha kukua na kuwa na uzito wa kawaida na chenye virutubishi vyote kwa uwiano unaotakiwa.

“Jamii inatakiwa kujua kuwa mwili si eneo la kuweka chakula cha ziada. Hivyo watu wanatakiwa kula matunda angalau mara mbili kwa siku na kula mboga kwa wiki. Tumia mafuta kiasi kidogo hususani yale yatokanayo na mimea na sukari na chumvi pia inatakiwa kutumiwa kidogo sambamba na kutokunywa pombe kupita kiasi,” anasema Waane.

Kwa upande wa mtindo bora wa maisha, Waane anasema ni kwa jamii kutakiwa kufanya mazoezi ili kuihusisha misuli na kusababisha kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kazi ya kupumua. Kiwango cha mazoezi kinachotakiwa ni dakika 30 kwa siku angalau siku tano kwa wiki. “Imeandikwa kila mtu atakula kwa jaso lake, hivyo hakikisha unatoka jasho angalau dakika 150 kwa wiki,” anasema Waane.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts