7/9/16

CUF WATOA MASHARTI YA KUKUTANA NA CCM KUHUSU ZNZ

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema kipo tayari kufanya mazungumzo na CCM kumaliza mgogoro wa uchaguzi mkuu kama msingi wake utakuwa kutafuta haki ya wananchi waliyofanya kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, na kusimamiwa na Jumuiya za Kimataifa.

Msimamo huo umelezwa na Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Chama hicho, Salim Bimani Abdalla, kufuatia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania kuvishauri vyama vya CCM na CUF kukaa pamoja kutafuta muafaka wa kumaliza matatizo ya kisiasa Zanzibar.bendera_cufAlisema CUF ipo tayari kuingia katika mazungumzo yoyote iwe mchana au usiku, endapo yatazingatia ajenda ya kupatikana haki ya kidemokrasia kama wananchi walivyokuwa wameamua katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, alisema mazungunmzo hayo lazima yaratibiwe na kusimamiwa na Jumuiya za Kimataifa kutokana na CCM kutokuwa na nia njema katika kumaliza mgogoro huo.

“CUF tupo tayari kufanya mazungumzo iwe mchana au usiku, kama yataratibiwa na kusimamiwa na jumuiya za kimataifa, ndiyo maana tulifungua mlango wa mazungumzo mapaema, lakini CCM walishindwa kuheshimu mazungumzo hayo,”alisema Bimani.

Alisema ushauri wa Tume ya Haki za Binadamu umejaa hekima na busara, na kwamba CUF haiwezi kudharau kwa sababu ya manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.

Bimani alidai nchi imebakia vipande vipande kutokana na mgawanyiko mkubwa wa wananchi uliyojitokeza ikiwamo kubaguana katika huduma za kijamii tangu kuibuka kwa mgogoro wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar.

“Hakuna njia ya kumaliza mgogoro huu zaidi ya kuvunja serikali iliyopo madarakani na kuingia katika mazungumzo ya kutafuta muafaka wa matokeo ya Uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana,”alisema Bimani.

Aidha, alisema CUF ilitarajia Rais Dk. Ali Mohamed Shein, angetumia mkusanyiko wa Baraza la Idd-El-Fitri kutafuta njia muafaka za kumaliza mgogoro wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, lakini alionekana kuimarisha chimbuko lake baada ya kusema hakuna serikali ya mpito na uchaguzi mpaka 2020

Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts