7/3/16

Dawa rasmi za nguvu za kiume Bongo ni hizi


WAKATI kasi ya kuibuka kwa waganga wa tiba za asili wanaojitangaza kuuza dawa za kuongeza nguvu za kiume ikionekana kuongezeka kila uchao,Hatimaye Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imeibuka na kueleza wazi kuwa dawa pekee zinazofaa ni zile zilizothibitishwa kitaalamu kuwa zinafaa kwa matibabu hayo na siyo vinginevyo.

Nipashe ilifanya uchunguzi kwa siku kadhaa kuhusiana na kuwapo kwa utitiri wa matangazo holela ya dawa za nguvu za kiume, hasa katika maeneo ya mijini ikiwamo jijini Dar es Salaam na ndipo ilipobaini kuwa dawa rasmi zilizothibitishwa na TFDA hazizidi tano.

Nyingine nyingi hazijathibitishwa na hivyo kuwa na uwezekano wa kutotimiza matarajio ya watumiaji au kuwahatarisha na madhara mbalimbali yakiwamo ya kupasuka kwa mishipa ya damu iliyopo kwenye moyo.

Afisa Uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza, aliiambia Nipashe kuwa ni kweli kuna dawa nyingi zinazotangazwa na watu mbalimbali kuwa zinatibu tatizo la nguvu za kiume, lakini zilizo rasmi ni pamoja na Viagra, Erecto, Cialis na Suagra.

Simwanza alisema dawa hizo ndizo wanazozitambua kuwa zinaweza kutumiwa na watu waliopungukiwa au kuishiwa kabisa nguvu za kiume kwa sababu zimepitishwa baada ya kukidhi vigezo vya kitaalamu.

Hata hivyo, Simwanza alisema dawa hizo siyo za kutumiwa kiholela bali wenye shida nazo ni lazima wafuate maelekezo ya madaktari ili kujiepusha na madhara yake pindi zikitumika kiholela.

“Kuna dawa nyingi ambazo sisi tunazitambua na tumezipitisha zitumike…lakini mtu asizitumie hadi pale atakapopewa ushauri wa daktari. Hizi zina nguvu sana na zinaweza kufanya mishipa ya moyo kupasuka ama kuathiri mfumo wa damu kwa watu wanaozitumia bila kufuata maelekezo ya madaktari,” alisema Simwanza.

Alipoulizwa kuhusu dawa za asili za kuongeza nguvu za kiume zikiwamo maarufu za kizizi cha mkuyati na zile zinazofahamika kama vumbi la Kongo, zikihusisha orodha ya dawa mbalimbali za aina hiyo kutoka Kongo zikiwamo za kasongo na mundende, Simwanza alisema TFDA hawawezi kuzizungumzia hizo na badala yake waulizwe wataalamu wa kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala cha Wizara ya Afya.

Dawa nyingine maarufu za kiasili ambazo huuzwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam hutambulishwa kwa majina ya mkongoraa, sheki na oljanilolo inayopatikana zaidi kwa morani wa Kimasai.

Alipoulizwa kuhusu dawa hizo za asili kwa ajili ya kushughulikia tatizo la nguvu za kiume, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Paul Mhame, alisema hivi sasa Wizara ya Afya iko katika utaratibu wa kusajili dawa za asili zikiwamo hizo (kizizi cha Mkuyati na jamii ya vumbi la Kongo) ikiwa zitathibitika kuwa zinafaa na hazina madhara kwa watumiaji.

Akieleza zaidi, Dk. Mhame alisema kuwa hadi sasa hakuna dawa ya asili yoyote ambayo imesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kwamba, kwa sababu hiyo, hakuna dawa ya kiasili ambayo Wizara inaweza kuizungumzia kwa uwazi kuwa imethibitishwa kuwa inaongeza nguvu za kiume pasi na kwua na madhara yoyote kwa watumiaji.

Dl. Mhame aliongeza kuwa kwa sababu hiyo ya kutokuwapo kwa usajili rasmi kwa dawa za asili hadi kufikia sasa, ni vyema watumiaji wakawa waangalifu kutumia dawa za namna ya kizizi cha Mkuyati na vumbi la Kongo zinazouzwa kiholela mitaani kwa sababu zinaweza kuwasababishia madhara makubwa kiafya kwa vile ni dawa ambazo hazina vipimo sahihi vya matumizi yake.

Hata hivyo, Dk.Mhame alikiri kuwa Tanzania ina miti mingi ya asili ambayo inaweza kutumika kutibu masuala ya tendo la ndoa baina ya wapendanao, lakini ni muhimu kutambua kuwa tiba inapotangazwa kwa sura ya kibiashara inatia shaka na hivyo watumiaji wanapaswa kuwa macho.

“Kwa mfano, kuna watu wanauziwa kile wanachoelezwa kuwa ni supu ya pweza mitaani kuboresha afya zao hasa kuhusu nguvu za kiume… lakini ni muhimu kuwa waangalifu ili kujiridhisha kuwa kweli kinachouzwa na watu kunywa ni supu ya pweza au ni maji tu ya kawaida,” alitahadharisha Dk. Mhame.

Aliongeza kuwa zipo dawa kadhaa za tiba asili ambazo baraza wanazitambua kuwa husaidia kutatua tatizo la nguvu za kiume, lakini nyingi hazifanyi kazi za papo kwa papo kama watu wanavyoaminishwa, bali nyingi humlazimu mhusika atumie dawa hizo kwa siku akdhaa ili mwili urudi katika hali yake ya awali na kupata jawabu ya kile kinachotarajiwa.

Alisema kuwa ipo mimea imethibitika pia kutatua tatizo la nguvu za kiume kama mahama au mapama, ubuyu na majani ya mlonge, lakini zote hizo humsaidia mtu aliyepungukiwa na nguvu za kiume kurudisha mwili wake katika hali ya kawaida baada ya kutumiwa kwa siku kadhaa na siyo papo kwa papo kama inavyoelezwa kuhusu kizizi cha mkuyati na vumbi la Kongo.

Alisema ili dawa ya tiba asili ifanye kazi papo kwa papo, ni lazima ikamuliwe na kuondolewa viambata vingine ndipo itafanya kazi papo kwa papo kama ilivyo kwa dawa aina ya Viagra, lakini muhimu ni kufuata maelekezo ya daktari.

MADAKTARI WAONYA
Katika hatua nyingine, madaktari kadhaa waliozungumza na Nipashe wameonya kuwa kwa yeyote anayetumia dawa za kuongeza nguvu zilizotihibitishwa kama viagra, ni vyema atumie dozi yake baada ya kushauriwa kitaalamu na pia awe karibu na mwenza wake kwa sababu vinginevyo anaweza kujipa mateso makali ya mwili.

“Watu wenye matatizo ya nguvu za kiume wanapaswa kuonana na daktari… hizo dawa za asili kiukweli zina nguvu sana na mtu akitumia asipopata mwenza kwa wakati huwa ni hatari,” alisema Dk. Simon Madatura wa Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Dk. Madatura alisema mtu yeyote anayetumia dawa za kuongeza nguvu za kiume zikiwamo zile za asili, ajue kuwa anapaswa kuwa mwangalifu kwa sababu kinyume chake anaweza pia kusababisha mfumo wake wa vichocheo kufa.

Alisema utumiaji holela wa dawa hizo unaweza kusababisha mtumiaji kuwa tegemezi wa dawa hizo anapokaribia kushiriki tendo la ndoa mwishowe husababisha mhusika kushindwa kufanya kazi kabisa hadi hapo atakapokuwa na dawa hizo.

Alisema baadhi ya dawa hizo khusababisha mtumiaji kushiriki tendo la ndoa kwa muda mrefu na hatari nyingine inayoweza kumkumba mhusika ni mishipa ya moyo wake kupasuka kutokana na msukumo mkubwa wa damu.

Alisema dawa kama Kizizi cha Mkuyati na Vumbi la kongo siyo dawa rasmi zilizothibitishwa na wataalamu na hivyo siyo vyema kutumiwa hovyo.

Akitolea mfano juu ya madhara zaidi ya kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume bila kufuata ushauri, Dk. Madatura alisema yapo matukio ya watu wanaotumia viagra kiholela kupoteza maisha baada ya dawa hizo kuwazidi nguvu.

Daktari huyo aliwataja baadhi ya watu ambao wako katika matatizo ya kutokuwa na nguvu za kiume kuwa ni wale wenye magonjwa kama ya kisukari, msongo wa mawazo, shinikizo la damu, tezi dume, watumiaji wa dawa za kulevya na na pia wavuta sigara.

Alisema njia sahihi ya kuondokana na matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume ni kufanya mazoezi, kula vyakula kwa kuzingatia lishe bora na pia wapenzi kuwa wapendao kwa dhati.

Daktari wa masuala ya uzazi kutoka Hospitali binafsi ya Mico jijini Dar es Salaam, Makene Ndaro, alisema wao hupokea vijana wengi wenye matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume na baadhi yao huwa ni matokeo ya kutumia kiholela dawa hizo.

“Tunapokea vijana 10 hadi 20 kwa mwezi ambao huwa na matatizo ya nguvu za kiume. Wengi ni vijana wa umri kati ya miaka 25 hadi 35. Matumizi ya dawa za nguvu za kiume zisizothibitishwa kitaalamu huchangia pia kuwapo kwa matatizo haya,” alisema Dk. Ndaro

Alisema athari mbaya ambazo mtu anayetumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kiholela huwa ni pamoja na misuli ya via vyake vya uzazi kusinyaa, kushindwa kabisa kushiriki tendo la ndoa, kupata upofu kutokana na mishipa ya macho kushindwa kuhimili kasi ya damu itakayokuwa inazunguka kwa kasi kutokana na nguvu ya dawa hizo.

“Mishipa ya macho ni midogo sana. Sasa mtumiaji holela wa dawa za kuongeza nguvu za kiume akiwa anashiriki tendo la ndoa, anakuwa anatumia nguvu sana na atachelewa kufika kileleni, hivyo kusabisha mzunguko wa damu kuwa mkubwa na kumsababishia upofu baada ya misihpa hiyo kushindwa kuhimili msukumo uliopo,” alisema Dk.Ndaro na kutaja matatizo mengine ambayo yanaweza kumpata mtumiaji wa dawa hizo kiholela kuwa ni pamoja na kuahribika kwa ini na figo.

WATUMIAJI WANASEMAJE
Mmoja wa watumiaji wakubwa wa dawa hizo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema hutumia dawa hizo kwa dhumuni la kuibuka kidedea pindi anapokutana na mpenzi wake na mara hufanikisha lengo lake hilo.

Mtumiaji mwingine alisema hujiona kama amepungukiwa kitu Fulani asipotumia dawa za kuongeza nguvu kabla ya kukutana na mwenza wake na hilo anaamini ni tatizo kubwa kwake kwa sasa.

Alisema kilichomuingiza katika matumizi ya dawa hizo, ni kukerwa na hali aliyokuwa nayo hapo kabla ya kufika kileleni mapema lakini atumiapo dawa hizo huchelewa na kupata raha kwa muda mrefu wa saa tatu hadi saa nne.

Kijana mwingine alisema kuwa yeye hutumia dawa za kuongeza nguvu ili kumridhisha zaidi mpenzi wake ambaye ni mama mwenye umri mkubwa kuliko yeye na kwa kufanya hivyo, hulipwa fedha nzuri hadi kufikia Sh. 200,000.

MUUZAJI ASIMULIA
Nipashe lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa vijana aliyewahi kuuza dawa hizo aliyejitambulisha kwa jina la Hassan ‘Beka’, ambaye alisema alikuwa akitoa dawa hizo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alisema madereva wanaoendesha magari kwenda nchini Kongo ndiyo hufanya biashara hiyo zaidi, wakichukua dawa za ‘vumbi la Kongo’ na kuzileta nchini ambako siku hizi wateja wake siyo wazee tu bali vijana.

Alisema dawa mojawapo iitwayo sheki, ambayo huweza kuchanganwa na soda, huuzwa kwa kati ya Sh. 5,000 hadi Sh. 20,000 kutegemeana na ujazo wake.

“Hiyo sheki , kichupa cha maji kidogo kikijaa unauziwa Sh. 20,000, inayoitwa Kasongo ndiyo balaa kwa sababu yenyewe unauziwa kama dawa za kulevya… kidogo sana kwenye ukucha huuzwa Sh. 5,000,” alisema Beka.

Alisema baadhi ya maeneo zinakotoka dawa hizo ni nchini Kongo ni katika migodi ya Mutanda, ambako ndiko dawa za aina hiyo inapatikana kwa wingi. Alisema baadhi ya dawa hizo huwa ni za kunywa na nyingine hutumiwa kwa kupaka.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts