Kasembe abwagwa, Cecil mbunge halali Jimbo la Ndanda | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

7/1/16

Kasembe abwagwa, Cecil mbunge halali Jimbo la NdandaMahakama Kuu Kanda ya Mtwara, imemthibitisha Cecil Mwambe (Chadema) kuwa ndiye mbunge halali wa Jimbo la Ndanda wilayani Mtwara na kutupilia mbali madai yaliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa CCM, Mariam Kasembe.


Katika hukumu hiyo iliyotolewa jana na Jaji, Winfrida Kossoro awali alianza kwa kurudia kusoma madai na kupitia ushahidi uliotolewa na mpeleka maombi na upande wa wajibu maombi.


Katika kesi hiyo Kasembe alipeleka madai matatu mahakamani hapo ya kuitaka itengue ubunge wa Mwambe kwa madai kuwa uchaguzi haukuwa wa huru na haki. Pia, zihesabu upya kura na tatu alikuwa anadai Mwambe alikuwa akitoa lugha za matusi wakati wa kampeni.


Akisoma hukumu hiyo, Jaji Kassoro alisema mpeleka maombi ameshindwa kuithibitishia Mahakama madai yake.


Akizungumza baada ya kutolewa hukumu hiyo, Mwambe aliwaomba wafuasi wa chama chake na wakazi wa Jimbo la Ndanda kuwa watulivu na sasa wageukie shughuli za maendeleo, huku akiwashukuru kwa kumpatia ushindi uliothibitishwa na mahakama.


Akizungumzia gharama za kesi, alisema bado anatafakari nini cha kufanya, licha ya Mahakama kuamuru alipwe fidia.


Alipotakiwa kuelezea hukumu hiyo, Wakili wa Kasembe, Elphace Rweshabura aligoma kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwapo mahakamani hapo.


Wananchi waliofika mahakamani hapo walisema, hukumu hiyo imetolewa kwa wakati bila kupoteza muda kama zilivyokuwa kesi za kupinga matokea katika miaka ya nyuma.


Mfuasi wa Chadema, Sophia Joram alisema, “Nina furaha, mahakama imetoa hukumu kwa haki na Jaji ameweza kutusomea kesi nzima na tumebaini upungufu ulikuwa wapi. Hivyo ni busara kwa kila mtu kukubaliana na uamuzi huo.”


Issa Chimae alisema, “Kesi ilikuja mahakamani ili haki ipatikane na imepatikana, sisi hatuna la kuzungumza.”
 
chanzo: Mwananchi

google+

linkedin