7/3/16

Mwanza yaongoza kwa saratani za watoto


TATIZO la saratani kwa watoto linaongezeka nchini tofauti na miaka iliyopita, lakini chanzo cha ugonjwa huu bado hakijafahamika.
jiji la mwanza
Hata hivyo inahofiwa kuwa mtoto anapozaliwa na saratani, kuna asilimia kubwa ya wazazi wote kuwa na vinasaba vya maradhi hayo.
Dokta Levin Mumburi, bingwa wa saratani kwa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, alisema wakati wa mahojiano na Nipashe na kuongeza kuwa mkoa wa Mwanza unaoongoza kwa idadi kubwa ya watoto walioathirika, hata hivyo hakuwa na takwimu.
Alifafanua zaidi kuwa saratani zinazofikishwa hospitalini hapo ni za aina nyingi ikiwamo ya shingo, figo, tumbo, ya jicho, mdomo na kichwa.
“ Baada ya watoto kufanyiwa vipimo uchunguzi unaonyesha kuwa asilimia kubwa wanaugua saratani ya damu”alisema Dk.Mumburi.
Aliongeza kuwa ugonjwa huu kwa kuwa haujulikani chanzo chake imekuwa ni tatizo hata kwa madaktari katika hospitali za humu nchini na kwingineko, mtoto anapokuwa na uvimbe madaktari wanajitahidi kuutibu baada ya kuona hakuna matumaini ya kutibika ndipo wanapowaleta Muhimbili wakiwa na hali mbaya na gharama za kutibiwa zinakuwa kubwa.
Dk. Mumburi alieleza kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ndiyo pekee yenye kitengo cha saratani kwa watoto. Bila kujali umri,watoto wanaoingia katika hospitali hiyo kwa mwezi anasema ni 400 hadi 500 hao ni wale wanaotoka mikoa yote nchini ingawa Mwanza unaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi zaidi.
DALILI
Alifafanua kuwa wazazi na walezi wa watoto wanatakiwa kuwa makini wanapoona dalili kama kadhaa kuwa kuna uwezekano wa kuwa na saratani.
Mojawapo ni pamoja na kutoka damu puani, kulala kwa muda mrefu, kuwa na uvimbe usiokuwa na maumivu makali.
Wazazi wanatakiwa kuwa makini maana ugonjwa huu kwa watoto hauna umri wa wala hautokani na mazingira tunayoishi kama kuvuta sigara, matumizi ya dawa au vyakula.
CHANGAMOTO
Akizungumzia changamoto alisema ni gharama kubwa ya matibabu hasa vipimo na utafiti akitaja kuwa inagarimu Dola 3,000 au karibu sawa na Shilingi milioni 6.6 vipimo na utafiti . Aliongeza kuwa serikali na wadau mbalimbali ndiyo wanaochangia na kwamba wafadhili huchangia kwa kiwango kikubwa na kama watakapojitoa maisha ya wagonwa yanakuwa hatarini.
Daktari Mumburi alieleza kuwa kitengo hicho ndicho pekee nchini cha saratani kwa watoto na kwamba kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa madaktari bingwa wa saratani kwa watoto, na kwamba bingwa ni mmoja,jambo ambalo ni hatari maana endapo atapata matatizo ya kiafya tiba kwa watoto itakuwa changooto nyingine.
Aliiomba serikali kuongeza bajeti ya madaktari kwa ajili ya kujifunza saratani kwa watoto angalau kila mkoa apatikane mmoja ili kunusuru maisha ya watoto wanaokufa bila kufika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Changamoto nyingine kwa mujibu wa maelezo yake ni pamoja na kukosekana kwa vifaa tiba na fedha za kufanya utafiti hali inayochangia kutokuwa na takwimu sahihi za miaka iliyopita.

chanzo: NIPASHE
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm