7/17/16

Saa 120 za panga la Magufuli CCM


HUKU zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya kufikia Julai 23, sawa na saa 120, kabla Rais John Magufuli atwae rasmi uenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kuna taarifa kuwa hofu kubwa imetanda kuhusiana na uwezekano wa kupitishwa kwa panga kali katika safu ya juu ya uongozi wa chama hicho tawala.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kupitia mahojiano na wanachama kadhaa wakiwamo viongozi wa chama hicho, umebaini kuwa hofu iliyotamalaki miongoni mwao ni uwezekano wa mabadiliko makubwa yanayoweza kufanywa na Rais Magufuli kwa kutumia ‘staili’ yake ile ile aliyoanza kuionyesha serikalini tangu akabidhiwe madaraka baada ya kuapishwa Novemba 5, 2015.

Aidha, uchunguzi huo umebaini kuwa wapo makada kadhaa wanaojihusisha na ‘dili’ mbalimbali za kuwaingizia fedha za kiujanja-ujanja wakitumia kivuli cha ukada wao CCM ndiyo walio katika hali mbaya zaidi huku wakitamani siku zigande ili kutoifikia siku hiyo ya kufanyika kwa mkutano mkuu maalum wa kumkabidhi kijiti cha uongozi Rais Magufuli.

“Kuna watu hawana uchungu wowote na chama lakini hujiweka kimbelembele kwa namna ya kisanii ili kufanikisha mambo yao… wapo hadi matapeli wa mjini hujifanya ni makada wakubwa wa chama chetu, lakini kiukweli hawana lolote isipokuwa ni kufanikisha dili zao za kimjini zinazowaingizia fedha nyingi kila uchao.

Wanachama wa aina hii hawana raha hata kidogo,” chanzo kimoja kiliiambia Nipashe mwishoni mwa wiki.

“Magufuli hatabiriki. Linapokuja suala la kuzingatia haki, utaratibu na sheria za nchi huwa hana msalie… na hili ameshalithibitisha kupitia kampeni yake ya kutumbua majipu ambapo vigogo kadhaa waliokuwa wakidhaniwa kuwa hawaguswi wameshashughulikiwa. Bila shaka tutaanza kushuhudia CCM mpya isiyokuwa na utitiri wa watu wenye madoa ya kifisadi,” chanzo hicho kiliongeza kwa sharti la kutoandikwa jina.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Idara ya Itikadi na Uenezi (CCM), Nape Nnauye, mkutano mkuu maalum wa chama hicho utafanyika kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Dodoma kama ulivyopangwa na maandalizi yote yameshakamilika.

Magufuli anatarajiwa kutwaa uenyekiti wa CCM ikiwa zimepita siku 262, tangu akabidhiwe kiti cha Urais Novemba 5, mwaka jana.

Nape alisema kabla ya kikao kitakachokuwa na ajenda itakayotoa nafasi kwa Magufuli kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti wa chama, kutakuwa na vikao vya Kamati ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kitakachofanyika Julai 21 na pia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kitaklacofanyika Julai 22.

HOFU ZAIDI
Mbali na hofu itokanayo na kiapo cha Magufuli kusafisha mafisadi nchini, yapo pia mambo mengine kadhaa yaliyowajaza hofu baadhi ya makada wa chama hicho. Kwa mujibu wa chanzo chetu, mambo mengine yanayowapasua kichwa baadhi ya makada kuhusiana na ujio wa Magufuli ni pamoja na ahadi yake ya kushughulikia wasaliti ndani ya chama na pia mpango wake wa kutanguliza vijana katika uteuzi wa nafasi mbalimbali kutokana na imani yake kubwa kwao, huku mfano ukidhihirishwa na uteuzi wake wa nafasi za ukuu wa mkoa, ukuu wa wilaya, makatibu tawala, wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmshauri za wilaya.

“Hili la kuwashughulikia wanachama wanaojifanya kuwa wao ni CCM wakati ni mamluki wasiokuwa na uchungu na chama alishalisemea mara nyingi sana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu,” chanzo kilieleza.

“Pia mapenzi yake kwa vijana yameongezeka kutokana na utendaji mzuri ambao tayari umeshaonyeshwa na wale aliowaamini katika nafasi mbalimbali hadi sasa, watu kama Paul Makonda, Anthony Mavunde na vijana wengine wengi ndani ya Serikali wanaweza kuwa sababu ya Rais Maagufuli kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya uongozi ndani ya CCM mpya. Hili liko wazi na kinachosubiriwa ni kwa siku hiyo tu kufikiwa na Magufuli kuanza mambo yake,” chanzo kingine kilidai.

Wakati wa mchakato wa uteuzi wa jina la mgombea urais wa CCM uliohusisha makada 38 kabla Magufuli kuibuka kidedea, ushindani mkali uliibuka miongoni mwa wanachama huku ikielezwa kuwa baadhi ya wale waliozidiwa kete katika uteuzi huo walibaki na vinyongo na kushiriki katika kampeni za chinichini kukwamisha safari yak Magufuli kuelekea Ikulu.

Inaelezwa zaidi kuwa kutokana na kushitukia kwake jambo hilo, ndipo Rais Magufuli alipoahidi mbele ya hadhara kuwa pindi atakapotwaa kijiti cha uongozi wa CCM, kazi mojawapo atakayofanya ni kuhakikisha kuwa ‘wanafiki’ wote wanasafishwa na kubaki na wanacham watiifu, hata kama ni wachache kiasi gani; lengo likiwa ni kuwa na CCM imara, isiyoyumbishwa kwa namna yoyote ile na wanachama wasaliti.

Aidha, inakumbukwa kuwa baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 baada ya kupata 58.46 ya kura zilizopigwa na mwishowe kukabidhiwa cheti cha uteuzi huo, Rais Magufuli alikwenda katika hafla maalum ya chama iliyofanyika jijini Dar es Salaam, kwenye ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba.

Alilakiwa na maelfu ya wanachama wenzake walioongozwa na Mwenyekiti (Kikwete) na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

Wakati wa hafla hiyo, Rais Magufuli alipata fursa ya kutoa shukrani zake kwa wana CCM wenzake waliomuamini na kumpa jukumu la kupeperusha bendera yao katika uchaguzi.

Ni hapo ndipo Magufuli alipozungumzia kile kinachowapandisha ‘presha’ baadhi ya makada wapiga ‘dili’ na wenye kutuhumiwa kuwa wasaliti wa chama. Moja ya mambo aliyoyazungumza ni kumuomba mwenyekiti, Rais mstaafu Kikwete, kuhakikisha anawaondoa wanafiki wote ndani ya chama kabla yeye hajatwaa kijiti cha uongozi.

Alisema ni heri kuwa na wanachama wachache wenye umoja na mshikamano kuliko kuwa na wanachama wengi ambao ni wanafiki.

“Nitakuwa sijautendea haki moyo wangu kama nitashindwa kuyaeleza haya. Na kama mnavyofahamu, msema kweli ni mpenzi wa Mungu… tumefika hapa kwa sababu ya wanafiki waliopo ndani ya chama chetu,” alisema Rais Magufuli, akizungumzia ugumu wa kampeni ambazo mwishowe zilimuwezesha mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Lowassa aliyehama CCM baada ya uteuzi wa Magufuli, aliweka historia tangu kurejeshwa chaguzi za vyama vingi nchini baada ya kupata zaidi ya asilimia 39 ya kura halili zilizopigwa, akiwakilisha Chadema, Chama cha Wananchi (CUF),

NCCR-Mageuzi na NLD.
Akifafanua zaidi katika hafla hiyo ya ushindi wake kwenye ofisi za Lumumba, Magufuli alisema wanafiki wote ndani ya CCM wanapaswa kuondoka wenyewe kabla ya kuondolewa kwa sababu wanakihujumu chama hicho, wakijifanya kuishabikia CCM nyakati za mchana huku usiku wakiwatumikia wapinzani.

Alikiri kuwa licha ya kushinda, kampeni zilikuwa ngumu na chanzo cha yote ni kundi la baadhi ya wanachama wenzao waliokuwa wakiongozana nao kwa kudhani ni wenzao kumbe ni wanafiki.

“Kabla hujanikabidhi chama Rais Kikwete, naomba uwasafishe wanasifiki wote walioko ndani ya chama,” alisema Magufuli kwa msisitizo na kuibua shangwe kubwa.

Alisisitiza kuwa anawatambua wanafiki wote ambao walikihujumu chama wakati wote wa kampeni na kusababisha kazi hiyo kuwa ngumu na hivyo, kamwe hatawavumilia.

Aidha, kama hiyo haitoshi, Rais Magufuli alirudia tena kauli kama hiyo ya kusafisha CCM siku ya Aprili 21, 2016 wakati wa mkutano wa kuwashukuru wenyeviti na makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini kutokana na kazi kubwa waliyoifanya ya kuhakikisha kuwa chama chao kinaendelea kubaki madarakani.

Rais Magufuli, alimueleza Katibu Mkuu wa CCM, Kinana kuwa, anatumai kuwa, kama serikalini kuna watumishi hewa, ni wazi kuwa na kwenye chama hawawezi kukosekana.

Kwa sababu hiyo, Magufuli alimuagiza Kinana kuhakikisha kuwa anawaondoa watumishi wote hewa ndani ya chama.

WAJUMBE KAMATI KUU
Mbali na mabadiuliko mbalimbali yanayotarajiwa kuiweka CCM mbali na watuhumiwa wa ufisadi, upo pia uwezekano wa kuwapo kwa mabadiliko makubwa katika nafasi mbalimbali za ndani ya chama, ikiwamo wajumbe wa kamati kuu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajabu Luhwavi, aliwahi kuiambia Nipashe hivi karibuni kuwa kwa nafasi yake, baada ya kukabidhiwa uenyekiti, Magufuli anaruhusiwa kikatiba kufanya mabadiliko kadhaa ya uongozi kwa kuzingatia taratibu mbalimbali zilizomo ndani ya katiba yao.

Inaelezwa kuwa wanaoweza kuguswa katika mabadiliko ya Magufuli ni pamoja na viongozi wa sekretarieti ya chama hicho na pia wajumbe wa kamati kuu, mbali na wale wanaoingia kutokana na nafasi zao.

Hivi sasa, baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM (CC), wengine wakiipata nafasi hiyo kutokana na nyadhifa zao, ni Dk. Ali Mohamed Shein, Phillip Mangula, Kinana, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, Mizengo Pinda, Balozi Seif Ali Iddi, Anna Makinda, Pandu Kificho, Rajab Luhwavi, Vuai Ali Vuai na Nape Nnauye.

Wengine ni Mohammed Seif Khatib, Zakhia Meghji, Asha- Rose Migiro, Sophia Simba, Sadifa Juma Khamis, Abdallah Bulembo, Jenister Mhagama, William Lukuvi, Steven Wasira, Dk. Emmanuel Nchimbi, Pindi Chana, Jerry Silaa, Adam Kimbisa, Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Ally Mwinyi, Dk. Maua Daftari, Samia Suluhu, Dk. Salim Ahmed Salim, Prof. Makame Mbarawa na Hadija Abood.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts