7/3/16

Wassira, Membe vinara sura zilizofutika ghafla


UTEUZI wa nafasi za wakuu wa Wilaya uliotangazwa katikati ya wiki na Rais John Magufuli.
Stephen Wasira kulia na bernard membe kushoto wakizungumza katika viwanja vya bunge wanaowasikiliza ni Ismail Jussa na january makamba.picha maktaba

Unaelekea kuhitimisha uwezekano wa kurejea ulingoni kwa wanasiasa kadhaa waliokuwa na majina makubwa katika safu ya uongozi wa Serikali iliyopita ya Rais Jakaya Kikwete wakiwamo mawaziri wa zamani, Stephen Wasira na Bernard Membe.

Katikati ya wiki, Rais Magufuli aliendelea kukamilisha safu ya uongozi katika Serikiali yake ya awamu ya tano kwa kuwateua wakuu wa wilaya 139, miongoni mwao wakiwamo wapya 78.

Aidha, tayari Rais Magufuli ameshawateua wakuu wa taasisi na mashirika kadhaa ya Serikali, mawaziri na pia wakuu wa mikoa.

Baadhi ya mabalozi wameshateuliwa pia na hivyo, ni dhahiri kuwa kuna uwezekano mdogo kwa baadhi ya vigogo katika serikali iliyopita ya Rais Kikwete kuendelea kufutika jumla walau katika kipindi hiki cha mwaka wa kwanza wa utawala wa Serikali ya awamu ya tano baada ya majina yao kutoonekana kokote.

Mbali na Wasira na Membe ambao walitikisa pia wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Chama Cha Mapinduz (CCM) kabla ya kutimuliwa vumbi na Magufuli aliyekuja kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, yapo pia majina ya vigogo kadhaa ambao sasa hawasikiki tena kutokana na ama kushinbdwa katika uchaguzi, kutogombea kabisa uongozi au kutokumbukwa katika nafasi za uteuzi za Rais Magufuli.

Katika orodha hiyo ndefu, majina yanayoonekana kuwahi kuwa makubwa zaidi katika Serikali iliyopita ni pamoja na aliyekuwa Waziri asiye na Wizara Maalum, Prof. Mark Mwandosya, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya kuachia ngazi kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, Dk. Emmanuel Nchimbi na aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia aliponzwa na Operesheni Tokomeza, Balozi Khamis Kagasheki.

Kadhalika, orodha ya vigogo waliokuwa na majina makubwa enzi za utawala wa Kikwete na sasa hawasikiki tena baada ya kukosekana bungeni na pia katika teuzi za Rais Magufuli ni aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Samuel Sitta na pia aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa.

Sitta hakuwamo katika orodha ya majina matano ya mwisho ya CCM wakati wa mbio za urais ndani ya chama hicho tawala. Baada ya hapo akajitosa tena katika harakati za kuwania uspika bila mafanikio kabla ya kuripotiwa kuwa amestaafu rasmi siasa.

Silaa alipoteza nafasi ya kurejea tena kwenye safu ya uongozi baada ya kushindwa katika mbio za kuwania ubunge wa Jimbo la Ukonga na hadi sasa hajabahatika kuwamo katika orodha ya wateule wa Magufuli.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya siasa aliiambia Nipashe kuwa majina yaliyokuwa yakitikisa katika utawala uliopita wa Rais Kikwete lakini sasa yamefutika ghafla katika kipindi kifupi cha kuanzia Oktoba 25 mwaka jana ni mengi, lakini vinara miongoni mwao ni pamoja na Wasira, Membe, Sitta na Prof. Mwandosya.

“Hawa walikuwa na majina makubwa zaidi. Katika kipindi chote cha utawala wa Rais Kikwete walikuwa wakisikika lakini sasa ni kama wamefutika kabisa,” alisema mchambuzi huyo.

“Wengine kama aliyekuwa Spika Anna Makinda wanatambulika wazi kwamba hawakuwa na uwezekano wa kurudi kwenye uongozi kwa sababu walishatangaza kung’atuka kabla hata ya uchaguzi mkuu. Wengine hawakugombea pia lakini wanaonekana bado ni vijana na hivyo walitarajiwa kuendelea kung’ara na mfano ni Nchimbi au Silaa aliyejaribu kuwania ubunge Ukonga bila mafanikio,” alisema na kuongeza:

”Wasira, Membe, Sitta na vigogo wengine kadhaa katika uongozi wa Kikwete wanaendelea kufutika kila uchao kwa sababu hivi sasa siyo wabunge, siyo wakuu wa mikoa, siyo wakuu wa wilaya, siyo mabalozi na wala siyo miongoni mwa wakuu wa taasisi nyeti za umma.”

Katika kundi la vigogo enzi za Kikwete wamo baadhi yao ambao wamepenya na sasa wanaendelea kuwa sehemu ya majina makubwa yanayoendelea kutamba katika uongozi kutokana na ama kuendelea kuwa wabunge au kuamniwa na Rais Magufuli kushika nafasi mbalimbali zikiwamo za uwaziri na ubalozi.

“Hawa wasiosikika kabisa ni wale ambao licha ya kutokuwa wabunge, lakini pia hawajakumbukwa hadi sasa kwa nafasi za uteuzi za Rais. Wengi wao hivi sasa sidhani kama bado wana matumaini ya kukumbukwa na Rais Magufuli… baadhi wanasubiri uteuzi wa safu mpya ya uongozi CCM Julai 23 ambayo sasa ndiyo karata pekee iliyobaki,” chanzo kiliongeza.

Dk. Harrison Mwakyembe, Mwigulu Nchemba na William Lukuvi ni miongoni mwa mawaziri waliokuwa na majina makubwa enzi za utawala wa Kikwete na sasa wanendelea kung;ara baada ya kuteuliwa kuwa mawaziri, kama ilivyo kwa Dk. Asha-Rose Migiro ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza.

MATUMAINI YABAKI SAFU MPYA CCM
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kuwa baada ya Rais Magufuli kuwafungia vioo baadhi ya vigogo wa serikali ya awamu iliyopita, sasa matumaini pekee ya baadhi yao ni kusubiri uteuzi wa safu mpya ya uongozi ndani ya CCM wakati Rais Magufuli atakapotwaa kijiti cha uenyekiti wa CCM Julai 23, kutoka kwa mwenyekiti wa sasa, Rais mstaafu Kikwete.

Imeelezwa kuwa kwa baadhi ya vigogo wasiosikika sasa, uteuzi huo wa watu wa kushika nafasi mbalimbali katika safu mpya ya uongozi CCM ndiyo tumaini pekee lililobaki kwa baadhi yao.

Msemaji wa sasa wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alipewa nafasi hiyo baada ya kuanguka ubunge kwenye Jimbo la Simanjiro wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita kwa kuzidiwa kete na James Ole Millya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, aliiambia Nipashe kuwa kwa kawaida, Kamati Kuu (CC) ya CCM hudumu hadi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa kawaida wa chama ambao kwa mujibu wa ratiba unapaswa kuwa mwaka 2017.

Hata hivyo, Luhwavi alisema kuwa mwenyekiti mpya akiona Kamati Kuu imepoteza sifa anaweza kuomba ridhaa ya Halmashauri Kuu (NEC) ili kuivunja.

Luhwavi alisema Mwenyekiti pia anaweza pia kutumia njia ya mkato kwa kuwaomba wajumbe wa CC wajiuzulu wenyewe ili wampe nafasi ya kupanga safu mpya kama ataona kuna hana haja ya kuendelea na Kamati Kuu iliyopo sasa.

“Wakati mwingine inaweza kutokea hata isipoombwa, Kamati Kuu yenyewe inaweza kujiuzulu ili kumpa nafasi Mwenyekiti mpya aisuke kwa anavyotaka yeye… na wakati huohuo ,Mwenyekiti akitaka anaweza kusuka upya pia Sekretarieti yake,” alisema Luhwavi.

Alisema kikatiba Mwenyekiti anapotaka kuunda CC mpya huteua majina 14 kutoka Tanzania Bara na majina 14 kutoka Tanzania Visiwani. Baadaye, majina hayo hupelekwa kwenye kikao cha NEC kupigiwa kura ili kupata wajumbe saba wa Bara na saba kutoka visiwani.

Luhwavi alisema ingawa hiyo haitokei mara nyingi, iliwahi kutokea mwishoni mwa mwaka 2011 baada ya Mwenyekiti wa sasa, Kikwete, kukosa imani na CC na kuishauri Halmashauiri Kuu kuivunja.

Alisema mwenyekiti mpya ana mamlaka ya moja kwa moja pia ya kubadili sekretarieti aliyoikuta akiwamo Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Visiwani, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Katibu wa Fedha na Uchumi, Katibu wa Oganaizesheni na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ambao kwa nafasi zao nao wanakuwa wajumbe wa CC.

MUHTASARI VINARA WASIOSIKIKA
Membe alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimatataifa kwenye serikali ya Kikwete tangu mwaka 2007, alipochukua nafasi ya Dk. Migiro.

Dk. Migoro ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Banki Moon kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo Jan, 5, 2007.

Awali, Membe alikuwa akichukuliwa kama mtu anayeandaliwa kumrithi Kikwete mara baada ya kuachia madaraka mwaka 2015. Ingawa Membe alifanikiwa kuingia tano bora, lakini bado kura zake hazikutosha na hivyo safari yake iliishia hatua hiyo.

Membe hakuwania ubunge kwenye jimbo alilokuwa akiliongoza la Mtama mkoani Lindi na alishatangaza mapema kwamba atawania nafasi ya juu zaidi, akimaanisha urais.

Prof. Mwandosya alikuwa Waziri asiye na Wizara Maalum hadi mwishoni mwa utawala wa Kikwete na alijitosa kuwania urais kupitia chama hicho, ingawa jina lake liliishia kwenye Kamati ya Maadili iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.

Prof. Mwandosya alikuwa Mbunge wa Rungwe (CCM) na alishatangaza mapema kuwa asingewania ubunge tena.

Mwandosya ambaye sasa amerudi kijijini, ameamua kujiweka pembeni na masuala ya siasa.

Kuna wakati alinukuliwa akimlalamikia Rais mstaafu Kikwete kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuiburuza Kamati Kuu na Kamati ya Maadili ya CCM, akidai kuwa alikwenda kwenye vikao hivyo akiwa na majina yake mfukoni.

Wasira aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, ni miongoni mwa viongozi waliokuwa maarufu katika Serikali ya awamu ya nne. Alijitosa katika mbio za urais ndani ya CCM, lakini jina lake liliishia kwenye Kamati ya Maadili.

Baada ya kuanguka kwenye urais, Wasira alijitosa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini lakini akaishia kugonga mwamba baada ya kuangushwa na Ester Bulaya wa Chadema.

Kabla ya kuangushwa kwake na sasa kubaki bila ya kuwa na cheo chochote kisiasa, Wasira alikuwa Mbunge wa Mwibara tangu mwaka 1970 na baadaye Mbunge wa Bunda hadi mwaka jana.

Sitta alisifika kwa jina la ‘mzee kasi na viwango’ alipokuwa Spika wa Bunge, lakini aliangushwa kwenye kinyang’anyiro kilichompa ushindi Anne Makinda katika nafasi ya uspika wa Bunge la 10 mwaka 2010.

Aliposhinda ubunge, Rais Kikwete alimpa uwaziri wa Afrika Mashariki na hadi mwishoni mwa utawala wa awamu iliyopita alikuwa akishikilia nafasi ya uwaziri wa Uchukuzi.

Sitta ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliochukua fomu ya urais ya kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana lakini jina lake lilikatwa kwenye Kamati ya Maadili.

Hakuchukua fomu ya kuwania ubunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na badala yake jimbo hilo alilokuwa akiliongoza alimuachia nafasi mkewe, Magreth Sitta ambaye ndiye mbunge wa sasa.

Tangu wakati huo, Sitta alitangaza kustaafu siasa na anaendelea na shughuli zake binafsi.

Mizengo Pinda, alikuwa Waziri Mkuu wa Kikwete tangu mwaka 2008, akichukua nafasi ya Edward Lowassa, aliyejiuzulu kwa kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richomond.

Pinda alikuwa maarufu kama mtoto wa mkulima alikuwa miongoni mwa waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, lakini kama wenzake, naye alikatwa na Kamati ya Maadili.

Tangu mwanzoni mwaka mwaka 2015, Pinda alishatangaza kwamba asingewania ubunge kwenye jimbo lake la Katavi, hivyo baada ya kuanguka kwenye mbio za urais aliamua kustaafu siasa.

Pinda kwa sasa anaendelea na maisha yake ya kilimo na ufugaji kijijini kwake Kibaoni wanakoishi pia wazazi wake.

Christopher Chiza ambaye alikuwa Mbunge wa Buyungu (CCM), alikuwa Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji mwishoni mwa serikali ya JK lakini licha ya kupitishwa na chama chake kuwania ubunge, aliangushwa na Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Dk. Nchimbi aliwahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo mwanzoni mwa utawala wa JK na baadaye alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2012.

Nchimbi ni miongoni mwa mawaziri walioangushwa kwa kashfa ya Operesheni Tokomeza, alitangaza kutowania tena ubunge kwenye Jimbo lake la Songea Mjini ambalo kwa sasa linashikiliwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lawrance Gama.

Hadi sasaa, Nchimbi ni Mjumbe wa Kamati Kuu lakini kubaki kwake au kuondolewa kutategemea matakwa ya Mwenyekiti mpya wa chama hicho, yaani Rais Magufuli.

Balozi Kagasheki, kama ilivyokuwa kwa Nchimbi, naye aling’olewa katika kashfa ya Operesheni Tokomeza.

Alifanikiwa kupenya kwenye kundi la walioomba kuteuliwa na CCM kuwania ubunge Bukoba Mjini, lakini aliangushwa na mpinzani wake wa siku nyingi, Wilfred Lwakatare wa (Chadema) kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

David Mathayo alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wakati kashfa ya Operesheni Tokomeza ilipotokea na ni miongoni mwa mawaziri waliong’olewa kufuatia shinikizo la Bunge.

Mathayo alipitishwa na CCM kuwania ubunge Jimbo la Same Magharibi, lakini naye aliangushwa Chadema kwenye wimbi la mageuzi la Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.

Adam Malima alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini hadi mwishoni mwa utawala wa Kikwete, lakini naye alipoomba kuteuliwa na chama chake kutetea nafasi yake katika Jimbo la Mkuranga, aliangushwa na Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo, Abdalah Ulega na sasa hasikiki tena.

Nyota ya Silaa aliyekuwa Meya wa Ilala jijini Dar es Salaam iling’aa katika medani za uongozi wakati wa utawala wa Rais Kikwete kuanzia 2010-2015. Wakati Kikwete aliposuka upya CC ya CCM mwaka 2012, Silaa alikuwa miongoni mwa sura mpya zilizochomoza. Hata hivyo, sasa hasikiki tena tangu aangushwe katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Ukonga na pia kutoteuliwa katika nafasi yoyote na Rais Magufuli.

Inaelezwa kuwa kiumri, Silaa bado ni kijana hivyo kutokumbukwa kwake na Rais Magufuli kwenye nafasi walau ya ukuu wa wilaya waliotangazwa hivi karibuni hakuashirii dalili njema kwake kisiasa. Sasa, kubaki kwake katika CC kunategemea huruma ya Magufuli katika mkutano mkuu maalum wa CCM utakaofanyika Julai 23.

Dk. Mohamed Ghalib Bilal alikuwa Makamu wa Rais wa JK 2010-2015. Naye ni miongoni mwa waliochukua fomu ya kuwania kupeperusha bendera ya urais kwa tiketi ya CCM lakini jina lake lilikatwa mapema na Kamati ya Maadili.

Yeye alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho kwa wadhifa wake, hivyo naye kubaki au kuondolewa kwake kutategemea matakwa ya Rais Magufuli pindi atakapoukwaa uenyekiti CCM kwa sababu sasa siyo Makamu wa Rais.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts