7/21/16

Watumishi wapewa siku 12 kuhamia NHC

 
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga wanaoishi jijini Tanga, wamepewa siku 12 kuhamia katika nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zilizojengwa katika eneo la Kasera.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Anjelina Mabula baada ya kukagua nyumba 40 zilizojengwa na NHC katika eneo hilo yalipo makao makuu ya halmashauri hiyo.
Mabula alilazimika kutoa agizo hilo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Yona Maki kumwambia kuwa baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wanaishi jijini humo ambako ni umbali wa kilomita 35 kutokana na ukosefu wa nyumba za kuishi.
Katika maelezo ya ujenzi wa nyumba hizo yaliyotolewa na Meneja wa NHC Mkoa wa Tanga, Isaya Mshamba, nyumba 10 kati ya hizo zina vyumba viwili na majiko ya nje, 10 zina vyumba vitatu na majiko ya nje wakati 20 zina vyumba vitatu na majiko ya ndani.
Mshamba alisema NHC ipo katika hatua za mwisho za kuiuzia halmashauri hiyo nyumba hizo ili iwapangishe watumishi wake ambao hawana makazi.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Maziba alitaja sababu ya baadhi ya watumishi kuishi jijini Tanga kuwa ni ukosefu wa nyumba na kwamba, ana imani zitakaponunuliwa watahamia Mkinga.
Baada ya kupokea maelezo hayo, Mabula alisema anataka ifikapo Agosti Mosi watumishi hao wawe wamehamia kwenye nyumba hizo.
Naibu waziri huyo alisema angependa watumishi hao wahamie kwenye nyumba hizo haraka kwa sababu wakiendelea kusuasua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakapotembelea Tanga na kukuta wakiishi jijini humo, itawagharimu.
Mabula alisema hataki kuwaona watumishi hao wakiwajibishwa kwa vitu ambavyo vinaweza kuepukika.
Mradi wa ujenzi wa nyumba hizo ulianza Januari 2013 na kukamilika Machi 2014, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alifungua rasmi matumizi ya nyumba hizo
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm