7/14/16

Waziri Tizeba asimamisha vigogo watano Kilimo

 Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amewasimamisha kazi watendaji watano wa wizara hiyo, akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Ombaeli Limweli na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula, Charles Walwa.
Wengine waliosimamishwa kazi kutoka idara ya Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Huduma, Anna Ngoo; Mkurugenzi wa Masoko, Mikalu Mapunda na Meneja wa Kanda, Jeremia Mtafia.
Dk Tizeba alisema jana kuwa Limweli amesimamishwa kazi kutokana na kuendelea kutoa vibali ya kusafirisha nafaka nje ya nchi kabla ya Serikali kufanya tathmini ya mazao yaliyovunwa 2015/16 .
Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la wafanyabiashara ambao wanauza mahindi na mpunga nje ya nchi bila ya Serikali kuyafanyia tathmini. “Nimemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Eliyampa Kiranga kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula,” alisema na kuongeza:
“Namwelekeza Katibu Mkuu wa wizara, Dk Yohana Budeba amwachishe kazi Kaimu Mkurugenzi Limweli atupishe tufanye uchunguzi kwa vibali alivyotoa kuanzia Novemba mwaka 2015 hadi sasa.”
Kadhalika, Waziri Tizeba alitoa wiki mbili kwa idara husika kufanya tathimini ya mazao yaliyovunwa katika kipindi cha msimu wa mazao ya 2015/16.
Alisema vibali hivyo vilitolewa kinyume na utaratibu kabla ya tathmini kukamilika.
“Jana amekuja mtu ofisini kwangu lakini simtaji aliambiwa kuwa leo au kesho angepewa kibali cha kusafirisha tani 300,000 za mahindi apeleke nchini Malawi,” alisema
Katika hatua nyingine, Dk Tizeba amesitisha utoaji wa leseni mpya za uvuvi hadi pale zitakapotengenezwa kanuni mpya za leseni hizo.
“Mvuvi wa nje anapewa muda wa kuvua wa mwaka mzima, lakini wao wanavua na aina nyingine ya samaki,” alisema na kuitaka kurugenzi ya uvuvi kubadilisha masharti ya leseni na kuundwa kwa kanuni mpya.

-Mwananchi
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts