8/1/16

Dalili Za Kwanza Za Donald Trump Kukimbia Mdahalo Na Hillary Clinton Zaanza KujitokezaDonald Trump-Mgombea Urais nchini Marekani kwa tiketi ya Republicans

Mbio za Urais nchini Marekani zinazidi kunoga. Baada ya makongamano ya vyama viwili vikubwa vya Republicans na Democrats kumalizika, macho na masikio huelekezwa kwenye kampeni na hususani midahalo (Debates). Midahalo ni sehemu muhimu ya zoezi la uchaguzi nchini Marekani. Ni muda muafaka wa wagombea kufafanua sera na mipango yao endapo watachaguliwa.

Sasa kwa muda kumekuwepo na tetesi kwamba mgombea wa Chama Cha Republicans, mfanyabiashara Donald Trump anapanga “kukacha au kukimbia” midahalo hiyo.

Tetesi zinasema ni ngumu kwa Trump kuingia kwenye mdahalo na mgombea wa Democrats, Hillary Clinton kwani Waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa serikali ya Obama na Seneta wa zamani wa New York ana uzoefu mkubwa sana katika midahalo na uelewa wa mambo mbalimbali kitu ambacho Donald Trump ameonekana wazi kutokuwa nacho. Republicans wanahofia kwamba midahalo itamuacha uchi mgombea wao. Trump mwenyewe ameshasema mara kadhaa kwamba hapendi midahalo. Kisingizio chake ni kwamba yeye sio mwanasiasa.

Katika kile ambacho kinaonekana ni dalili za awali za Donald Trump kuingia mitini, bilionea huyo ameshaanza kulalamika kwamba tarehe ya mdahalo wa kwanza sio nzuri. Anasema siku hiyo kuna michezo ya NFL (mpira wa miguu wa ki-Marekani). Anasema watu wengi hawatotizama debate wakati yeye anataka watu waone!

Midahalo ya wagombea Urais nchini Marekani huandaliwa na Tume huru isiyofungamana na chama chochote. Tume hiyo tayari imetoa maelezo kwamba tarehe hiyo imeandaliwa zaidi ya miezi 18 iliyopita na hawawezi kuibadili.

Mbali ya kwamba tarehe hiyo imeandaliwa mapema, wanasema kwa vyovyote vile hata siku zingine zingeingiliana na matukio mengine aidha ya kimichezo au mengineyo. Hata midahalo ya miaka iliyopita iliwahi kuingiliana na matukio ya michezo. Tume hiyo pia inasema hata kama watu hawatoangalia “Live” Wanaweza kurekodi na kuangalia baadae au ku-stream moja kwa moja hata wakiwa kwenye michezo. Kwa maneno mengine wanasema sababu au wasiwasi anaoutoa Trump hauna msingi.

Upande wa kambi ya mgombea wa Democrats, Hillary Clinton, wao wanasema wapo tayari na hawana tatizo na tarehe iliyopangwa.

Mdahalo wa kwanza umepangwa kufanyia tarehe 26 Septemba katika Chuo Kikuu Cha Hofstra kilichopo Hempstead New York. Mdahalo wa pili umepangwa kufanyika tarehe 9 Oktoba huko St.Loius na wa tatu na wa mwisho umepangwa kufanyika tarehe 19 Oktoba jijini Las Vegas.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts