DC awasimamisha kazi walimu watatu kwa tuhuma ya mapenzi | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/30/16

DC awasimamisha kazi walimu watatu kwa tuhuma ya mapenzi

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera, Godfrey Mheluka amewasimamisha kazi walimu watatu wa Shule ya Sekondari Kituntu kwa madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi shuleni hapo.


Pia, ameunda kamati kuchunguza tukio hilo ambayo ameipa siku 14 ikamilishe kazi hiyo.


Akitoa agizo hilo jana kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule hiyo, Mheluka alisema zipo taarifa nyingi zinazoripotiwa kwenye ofisi yake kuhusiana na vitendo hivyo.


Alisema ili kudhibiti hali hiyo, ameamua kuwasimamisha kazi walimu hao kupisha uchunguzi.


“Hatuwezi kukubali kuona mwanafunzi anageuzwa mke wakati mzazi kajinyima na kumhudumia mwanaye ili asome kwa ajili ya manufaa yake ya baadaye, na ikibainika kweli wanafanya vitendo hivyo, hatua za kisheria dhidi yao zitachukuliwa,” alisema Mheluka.


Hata hivyo, miongoni mwa walimu waliotajwa, Deodatus Lusatu alikanusha kuhusika na vitendo hivyo huku akidai kuwa anafanyiwa hila na watu wenye nia mbaya na yeye.


Alimpongeza mkuu wa wilaya kwa kuunda kamati ya uchunguzi, huku akitaka watu wote wenye ushahidi dhidi yake, wajitokeze mbele ya kamati hiyo ili ukweli ufahamike badala ya kuendelea kumpaka matope.


“Siwezi kufanya matendo ya kishetani kama haya, nina akili timami na kama ninafanya vitendo hivyo sipaswa kuendelea kuwapo chini ya jua,” alisema Lusatu.


Mkuu wa Wilaya Mheluka alisema utaratibu wote wa kiutumishi utafuatwa bila kumuonea.


Katibu wa Tume ya Nidhamu na Maadili ya Walimu (TSD) Wilaya ya Karagwe, Fredrick Kabendwe alisema, atafanya kazi sanjari na kamati atakayoiunda ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo.


Mkazi mmoja wa wilaya hiyo, Sadiki Juma alisema tuhuma hizo zinapaswa kuchunguzwa kwa makini kwani zinaweza kuwa ni chuki binafsi.


Katika hatua nyingine, Mheluka aliwataka wazazi, walezi na wananchi wa wilayani Karagwe kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kuiwezesha sekta ya elimu kufikia malengo wanayokusudia.


Pia, aliwataka kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti na kuacha kutochoma moto ovyo, yeyote atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.

google+

linkedin