8/13/16

Dk Magufuli ataja majipu CCMLicha ya kupokelewa na umati mkubwa wa wana-CCM na kusindikizwa na msafara mrefu hadi ofisi ndogo za CCM, Rais John Magufuli ametaja majipu yaliyopo ndani ya chama hicho akitaka wanachama na viongozi kumvumilia katika kipindi ambacho anataka kurejesha heshima, imani na maadili yaliyopotea.

Magufuli alikuwa mgombea pekee kwenye uchaguzi maalumu wa mwenyekiti wa CCM uliofanyika Julai 23 mjini Dodoma alioshinda kwa kupata kura 2,398 na tangu wakati huo alikuwa kwenye makao hayo makuu ya nchi hadi alipokwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa kushukuru wananchi kwa kumchagua kuwa Rais.


Mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na vikundi vya ngoma, matarumbeta na mamia ya wanachama, msafara wa magari madogo na mabasi ulielekea ofisi hizo ndogo za CCM zilizoko Lumumba ambako Rais Magufuli alitoa hotuba fupi iliyotaja baadhi ya majipu ndani ya CCM.


“Mahali nitakapoamua kunyosha nitanyooshea hapo hapo,” amesema Magufuli katika hotuba yake iliyochukua takribani dakika 50. “Inawezekana ujio wangu ndani ya CCM usiwafurahishe baadhi ya watu, lakini nina uhakika wanachama wetu zaidi ya milioni nane watafurahi. Nimeamua kufanya kazi kwa uwazi ili kila pato la chama lionekane.”


Rais Magufuli alisema CCM ilianza kupoteza dira na kuwa ya matajiri na kwamba anataka kukifanya kiwe cha aina yake.


Akizungumza baada ya viongozi wa CCM kuhutubia wakipiga vijembe vyama vya upinzani, Rais alisema hata vigogo wa chama hicho watakaokwenda kinyume na taratibu, watang’oka.


Akitaja baadhi ya majipu ndani ya CCM, Magufuli alisema jijini Dar es Salaam chama hicho kina viwanja zaidi ya 410 na kuhoji fedha zinazopatikana kutokana na mali hizo zinakwenda wapi.


“Kulikuwa na (Shirika la Uchumi na Kilimo la CCM)Sukita. Fedha za Sukita zinakwenda wapi? Kuna jengo la ghorofa la vijana wa CCM, naambiwa baadhi ya viongozi wa chama wamejigawia vyumba,” alisema huku akionyesha kwa kidole lilipo jengo hilo huku sauti ikitoka kwa wanachama ikisema “wengine umekaa nao hapo mbele, tunao ushahidi tutakuletea”.


“Hizi fedha zinakwenda kwenye mfuko wa nani? Haya ndio nitayachambua kituo kwa kituo, koma kwa koma, nukta kwa nukta mpaka kieleweke.”


Alisema hata Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na Jumuiya ya Wazazi wana majengo na vitega uchumi vingi, lakini fedha hazionekani.


“Viwanja vya mpira vya CCM navyo; kipo cha Mwanza, Songea; kuna viwanja sijui wapi na kila kiwanja kimezungushiwa maduka,” alisema.


“Mchezo uliopo; kila kibanda kwenye viwanja wanasema wanalipwa Sh30,000 lakini ukweli walikuwa wanalipwa Sh500,000 au milioni moja. Zile tofauti walikuwepo watu wakubwa ndani ya chama wanazimega. Hao n’talala nao mbele.”


Amesema kuwa anataka CCM yenye lengo la kutawala na si kubembeleza kutawala.


“Haiwezekani kila ukikaribia uchaguzi, tunakwenda kuombaomba kwa wafanyabiashara. UVCCM wenye maghorofa unakwenda kuomba; UWT nao hivyo hivyo na wakati mwingine mnawaomba hata waliohama CCM. Hawa UWT wanawafuata kwa kuvaa baibui usiku, yaani asubuhi ni CCM na usiku ni Chadema. Nasema uongo UWT?” alihoji na kuitikiwa “kweliii”.


“Hivi kwanini Redio Uhuru haina fedha na haipati matangazo? Kwanini kikundi cha TOT kina shida? Kwanini CCM haina hata televisheni? Lazima tujipange vizuri, tubadilike na kukubali changamoto. Asiyekubali kubadilika tutajitahidi kumbadilisha na asiyeweza kubadilika tutamwacha pembeni.”


Alisema katika uongozi wake anataka kuondoa kero za wananchi, huku akieleza jinsi anavyotekeleza ahadi yake ya elimu bure, kukusanya kodi, kujenga viwanda, kuimarisha miundombinu ya usafiri na kuimarisha sekta ya afya.


Kuhusu uchaguzi mkuu wa CCM utakaofanyika mwakani, Rais alisema atahakikisha wanapatikana viongozi wenye sifa na ambao hawatatoa rushwa.


“Atakayetoa fedha, jina lake halitarudi maana hata mimi nimepatikana bila rushwa,”


Amesema ilikuwa vigumu kuwania nafasi ya uongozi ndani ya CCM na kushinda akifananisha na ngamia kupenya kwenye tundu la sindano.


Katika hotuba hiyo, Rais Magufuli amesema wapo mafisadi waliosalia licha ya baadhi yao kukimbia baada ya kutoswa katika mchakato wa urais ndani ya CCM.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts