Kumekua na taarifa nyingi kutoka nchini India kuhusu mtoto wa mwaka mmoja anayeitwa Akash. Taarifa za mtoto huyo zimevuma sana kwa kuwa ana tofauti kubwa na watoto wengine wa mwaka mmoja. Mtoto Akash ameanza kuonyesha dalili zote za kubalehe. Kwa kawaida ulimwenguni kote tunatambua kuwa mwanadamu hubalehe na kuvunja ungo akiwa na umri wa kati ya miaka 10 mpaka 13.mtoto aliyebalehe mapema india
Kwa mujibu wa taarifa hizo mtoto Akash ambaye ana mwaka mmoja anaonyesha mabadiliko yote yanayoonekana kwa mvulana aliyebalehe. Wazazi wake walipompeleka hospitali mtoto huyo alipimwa na kukutwa na kiasi kikubwa cha homoni za kiume kinacholingana na kiasi kile kinachokutwa kwa kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 25. Ingawa habari ya mtoto huyo imevutia watu wengi kwa kuwa ni moja ya matukio yasiyo ya kawaida kuwahi kutokea duniani ninapenda kuchukua fursa hii kukutaarifu kuwa yeye sio mtoto wa kwanza kubalehe mapema na wala hatokua wa mwisho. Hali iliyomtokea mtoto huyu inatambulika kama balehe iliyowahi au kwa kitaalam precocious puberty.
BALEHE ILIYOWAHI (PRECOCIOUS PUBERTY) NI NINI 
balehe iliyotanguliaKi-baiolijia binadamu huzaliwa wakiwa hawana uwezo wa kuzalisha wala kuzaa. Kwa wengi uwezo huo hupatikana wanapofika umri wa miaka kuanzia 10 mpaka 13. Inapotokea binadamu wa kike (msichana) akavunja ungo (kuanza kutoa mayai yaliyo tayari kuchavushwa na kutengeneza mtoto) akiwa na umri wa chini ya miaka nane (8) huwekwa kwenye kundi la waliowahi kuvunja ungo. Inapotokea binadamu wa kiume (mvulana) akabalehe (akaanza kuwa na uwezo wa kutoa mbegu ambazo zinaweza kuchavusha yai la kike na kutengeneza mtoto) kabla ya kufika umri wa miaka tisa (9) nao huwekwa kwenye kundi la waliowahi kubalehe. Balehe iliyowahi au balehe ya mapema au kwa kitaalam precocious puberty ni balehe iliyotokea kabla ya umri wa miaka 8 kwa wasichana na miaka 9 kwa wavulana.
Hali hii si kawaida kutokea na kwa wengi ambao hubalehe mapema huwa wana sababu iliyosababisha wakawahi kubalehe.
BALEHE HUTOKEA VIPI
Mabadiliko ya mwili wakati wa balehe hutokea chini ya muongozo wa ubongo na homoni maalum za jinsia (sex hormones).
mtiririkoBinadamu anapofikisha umri wa kubalehe ubongo hutoa homoni inayoitwa Gonadotropin-releasing Hormone (Gn-RH) ambayo hufanya kazi ya kuamrisha tezi ya Pituitary iliyo kwenye ubongo ili tezi hiyo izalishe homoni za jinsia (sex hormones). Tezi za Pituitary huanza kutoa homoni mbili ambazo ni Luteinizing hormone (LH) na Follicle Stimulating hormone (FSH). Homoni hizo ndio huhusika na uhamasishaji wa uzalishaji wa homoni za kike (Estrogen) kwa wasichana na za kiume (Testosterone) kwa wavulana.
Homoni za kike yaani Estrogen husimamia mabadiliko ya kike kwa wasichana na homoni za kiume Testosterone husimamia mabadiliko ya kiume kwa wavulana.
MABADILIKO YA MWILI WAKATI WA BALEHE
Mabadiliko yafuatayo hutokea wakati wa balehe (kuvunja ungo kwa wasichana)
balehe kwa wote
WAVULANA
Homoni za kiume
 • Mwili kurefuka kwa kasi
 • Sauti kuwa nzito
 • Kuanza kuota ndevu, nywele za kwapani na nywele za sehemu za siri
 • Kukua kwa maumbile ya kiume
 • Kifua kutanuka
 • Kubadilika harufu ya mwili
 • Kutoka chunusi
 • Kupata hamu ya kufanya ngono
Mtoto Akasha ambaye ni mvulana ameonyesha mabadiliko niliyoorodhesha hapo juu akiwa na umri wa mwaka mmoja ndio maana ameushangaza ulimwengu.
WASICHANA (HUVUNJA UNGO)
 • EstrogenKuanza kuona damu ya hedhi
 • Mwili kurefuka kwa kasi
 • Sauti kuwa laini (ya kike)
 • Matiti kuanza kukua kwa kasi
 • Kuota chunusi
 • Kuanza kuota nywele za kwapani na nywele za sehemu za siri
 • Kubadilika harufu ya mwili
 • Kuwa na muonekano wa kike
 • Kupata hamu ya kufanya ngono
NINI HUSABABISHA BALEHE IKATOKEA KABLA YA WAKATI (PRECOCIOUS PUBERTY)
Kwa wengi ambao hali hii hutokea huwa ni vigumu kutambua sababu hasa iliyopelekea wakabalehe mapema lakini kwa ujumla sababu zimewekwa kwenye makundi makubwa mawili.
SABABU ZA KATI (CENTRAL PRECOCIOUS PUBERTY)
mabadiliko ya homoni
mtiririko wa utoaji wa homoni za jinsia
Hizi ni sababu za kwenye ubongo, uti wa mgongo au tezi zinazohusika na uzalishaji wa homoni za jinsia (sex hormone). Sababu hizo ni kama zifuatazo;
 • Uvimbe kwenye ubongo au uti wa mgongo
 • Mapungufu ya kuzaliwa nayo (mfano kichwa kikubwa yaani hydrocephalus)
 • Mtoto kupigwa na mionzi yenye sumu kwenye ubongo au uti wa mgongo
 • Ajali ya ubongo au uti wa mgongo
 • Maradhi ya kurithi ya tezi za adrenal
 • Maradhi ya tezi ya shingo (thyroid gland)
SABABU ZA PEMBENI (PERIPHERAL PRECOCIOUS PUBERTY)
SababuHizi ni sababu zinazohusiana na homoni za jinsia moja kwa moja yaani Estrogen kwa wasichana na Testosterone kwa wavulana.
Kwenye kundi hili la mara nyingi homoni kutoka kwenye ubongo huwa ziko katika kiwango cha kawaida tu. Tatizo hutokea kwenye maeneo homoni za jinsia zinapozalishwa au kutengenezwa.
Tatizo hutokana na hitilafu kwenye tezi za kike (Ovaries kwa wasichana), korodani (kwa wavulana), tezi za Adrenal na tezi za Pituitary.
Sababu huwa ni kama zifuatazo;
 • Uvimbe kwenye tezi za Adrenal au Pituitary ambazo huzalisha homoni za kike (Estrogen) na kiume (Testosterone).
 • Kuongezewa homoni za kiume (Testosterone) au za kike (Estrogen) kutoka nje kupitia vitu kama mafuta ya kupaka au dawa mbali mbali zenye homoni hizi.
 • Kwa wasichana pekee: Uvimbe kwenye tezi ya uzazi (Ovarian tumor)
 • Kwa wavulana: Uvimbe kwenye chembe hai zinazotengeneza mbegu (Germ cells) au kwenye chembe hai zinazotengeza homoni za kiume (Testosterone).
 • Matatizo ya kijenetiki ya kuzaliwa nayo. Haya ni matatizo ya kijenetiki ambayo hutokea wakati wa uumbaji wa mtoto akiwa tumboni kwa mama yake. Matatizo ya namna hii husababisha balehe itokee mapema zaidi kati ya mwaka mmoja (1) mpaka minne (4) baada ya kuzaliwa.
KINA NANI WAKO HATARINI ZAIDI KUBALEHE MAPEMA
 • Wasichana
 • Watoto wenye uzito mkubwa kupindukia
 • Watoto wanaopakwa mafuta yenye homoni za kike au za kiume
 • Watoto wenye maradhi mbali mbali hususani yanayohusu tezi za pituitary, adrenal pamoja na thyroid (tezi ya shingo).
 • Watoto wanaotibiwa saratani kwa njia ya mionzi
MADHARA YA BALEHE YA AINA HII
Watoto ambao wanapitia balehe mapema yaani precocious puberty hupata changamoto mbili kuu
 1. balehe ya mapemaKuwa wafupi wa kimo (kutorefuka sana): Kutokana na kubalehe mapema kabla ya umri sahihi watoto hawa hurefuka wakati huo wa balehe mpaka kufikia kimo kifupi zaidi ya kile cha wale ambao walibalehe muda sahihi wa miaka kuanzia 10. Kutokana na kubalehe akiwa na umri mdogo mhusika hurefuka kwa kasi na baada ya kumaliza kipindi cha balehe uwezekano wa kurefuka kwa kiwango kikubwa hupungua sana kutokana na kukokamaa kwa mifupa.  Watoto wengi wanaobalehe mapema huishia urefu wa chini ya futi 4.
 2. Athari za kisaikolojia: Kutokana na kupitia hali hii kabla ya watoto wengine wa rika lake, watoto wengi hupata athari za kisaikolojia. Athari hizi huweza kuonekana kwa muda mrefu na wengi huhitaji matibabu ya kisaikojolia ili waweze kukubaliana na kilichotokea na kuweza kuishi maisha yao ya kawaida bila kuwaza hali yao yakubalehe mapema.
TATIZO HUGUNDULIKA VIPI
Zaidi ya kuonekana akibadilika na kuonyesha dalili za kubalehe watoto wanaopitia hali hii hutakiwa kupelekwa hospitalini ambako wataonwa na daktari bingwa ambaye atasikiliza historia ya mabadiliko hayo ya mtoto pamoja na kumfanyia vipimo vya kawaida na baadae ataratibu ufanyaji wa vipimo muhimu kuangalia wingi wa homoni za jinsia kwenye miili ya watoto hao.
Kipimo cha wingi wa homoni za jinsia ni kipimo kitakachothibitisha kuwa mabadiliko yanayomtokea mtoto ni balehe.
Pia vipimo vingine vyenye lengo la kugundua sababu hasa ya balehe kutokea mapema ni lazima vifanyike. Vipimo hivi vitasaidia kujua namna ya kukabiliana na mabadiliko yatakayokua yanamtokea mtoto.
MATIBABU
 1. mtoto aliyebalehe mapemaMatibabu yanayolenga kuondoa chanzo cha tatizo: Matibabu haya yanalenga kutibu chanzo cha tatizo (kwa mfano kama chanzo ni uvimbe kwenye tezi za adrenal basi matibabu yatahusisha kuondoa uvimbe huo).
 2. Matibabu ya kupunguza kasi ya mabadiliko ya balehe: Matibabu haya yanalenga kupunguza kasi ya mabadiliko yanayoonekana wakati wa balehe. Matibabu haya huhusisha upunguzaji wa nguvu ya homoni za jinsia.
KUHUSU MTOTO AKASH
Homoni za kiume betterMtoto huyu amefanyiwa vipimo na sababu ya tatizo mpaka sasa haijafahamika hivyo matibabu anayopewa sasa yako kwenye kundi la pili na yanalenga kupunguza nguvu ya homoni za kiume na hivyo kupunguza kasi ya mabadiliko ya mwili yanayotokea kutokana na uwepo homoni hizo (mabadiliko ya wakati wa balehe).


HITIMISHO
Hali hii ya balehe ya mapema hutokea kwa watoto wengi hapa nchini kwetu na ni vyema kama wazazi, walezi wa majirani tujitahidi kuwapunguzia matatizo ya kisaikolojia watoto hawa kwa kukaa nao karibu na kuwahakikishia kuwa hakuna jambo baya ambalo litawatokea. Watakua vizuri tu na wataweza kuendesha maisha yao kama kawaida.
Watoto hawa pia ni vyema itambulike kuwa wanaweza kupata watoto kama ilivyo kwa watu waliopata balehe wakiwa na umri sahihi wa balehe. Hii ina maanisha ni vyema kuwapa elimu ya uzazi na kuhakikisha wanatambua kuwa wao wako tofauti na watoto wengine.
balehe mapema cover
MWISHO