8/12/16

Kucha 261 za Simba zamtia hatiani Mvietnam

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa Kilimanjaro, imemtia hatiani raia wa Vietnam, Hoang Trung (50),  kwa kosa la kusafirisha meno 60 na kucha 261 za simba zenye thamani ya Sh300 milioni kwenda nchini Qatar.
Hata hivyo, Mahakama hiyo imelipeleka jalada la kesi hiyo Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Moshi ili iweze kutoa adhabu baada ya mshitakiwa kuomba apewe adhabu ndogo kutokana na kuwa ni mgonjwa.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Joachim Tiganga, mbele ya wakili wa Serikali, Ignas Mwinuka baada ya Mahakama kumtia hatiani raia huyo wa Vietnam kwa makosa manne ya uhujumu uchumi.
Kucha hizo zilikuwa na thamani ya Dola 68,600 za Marekani sawa na Sh151.7 milioni za Tanzania wakati meno hayo ya Simba yalikuwa na thamani sawa na kucha hizo, na yalikuwa yakisafirishwa kwenda Jiji la Doha.
Awali upande wa upande wa mashitaka ulidai kuwa mshitakiwa alitenda makosa hayo Desemba 15 mwaka jana, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), wakati akijiandaa kusafiri kwenda Doha.
Katika shitaka la kwanza, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, ulidai siku hiyo, mshitakiwa alisafirisha kucha 261 kwenda Doha wakati shitaka la pili lilihusu kusafirisha meno 60.

Wakili Chavula, alidai mshitakiwa alisafirisha nyara hizo za Serikali pasipokuwa na kibali cha CITES, kosa linaloangukia katika sheria ya uhujumu uchumi na ya uhifadhi wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009.

Katika shitaka la tatu na la nne, mshitakiwa huyo alikabiliwa na mashitaka ya kupatikana na nyara za Serikali ambazo ni kucha 216 na meno 60 ya Simba, kinyume cha sheria ya uhifadhi wanyapori ya mwaka 2009 na Uhujumu uchumi.
Tangu alipofikishwa Mahakamani kwa mara kwanza Aprili 15 mwaka jana, mshitakiwa huyo aliyekuwa akitetewa na wakili Gwakisa Sambo, alikuwa akikanusha mashitaka hayo hadi alipotiwa hatiani na mahakama hiyo jana.
Katika hatua ya kama washitakiwa wana kesi ya kujibu ama la, mahakama ilimuona hana kesi ya kujibu, aliyekuwa mshitakiwa wa pili, Honest Mkojera (35) aliyekuwa Afisa Usalama wa kampuni inayoendesha Kia ya Kadco.
Akitoa uamuzi huo jana, Hakimu Tiganga alisema mashahidi watano wa upande wa mashitaka, wameweza kuithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka kuwa raia huyo wa Vietnam alitenda makosa hayo.
Katika maombolezo yake kupitia kwa wakili wake, Raia huyo aliomba apunguziwe adhabu kwa vile ni mgonjwa na amekaa muda mrefu gerezani, lakini katika uamuzi wake Hakimu alisema mahakama kuu ndio yenye uwezo huo.
Kutokana na Mahakama hiyo kupeleka jalada la kesi hiyo Mahakama kuu ili iweze kutoa adhabu kwa mshitakiwa, adhabu hiyo imepangwa kutolewa Agosti 16 mwaka huu.

mwananchi
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts