Maofisa wa Uhamiaji ‘wamtwanga’ diwani | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/20/16

Maofisa wa Uhamiaji ‘wamtwanga’ diwaniMAOFISA tisa wa Idara ya Uhamiaji katika ofisi zao mkoa wa Kigoma wanatuhumiwa kumpiga na kumjeruhi Diwani wa kata ya Kidahwe, Halmashauri ya wilaya Kigoma, Henry Kigufa.

Akizungumza mjini Kigoma diwani huyo alisema kuwa amekumbwa na dhahama hiyo ndani ya ofisi za uhamiaji ofisi ya mkoa Kigoma alipokuwa akifuatilia shauri la kukamatwa kwa ndugu yake Henry Kiaga ambaye anadaiwa kuwa na utata katika uraia wake.

Diwani huyo alisema kuwa alishangazwa na kitendo cha maofisa hao wa uhamiaji kumpiga na baadaye kumfunga pingu licha ya kujitambulisha mapema alipokuwa akiingia kwenye ofisi hizo kwamba yeye ni nani na kwamba tayari ameshafungua kesi kituo kikuu cha polisi mjini Kigoma akilalamikia kushambuliwa mwili na udhalilishaji.

Akieleza mazingira ya kupigwa kwake alisema kuwa anashangazwa na kitendo cha watendaji waandamizi wa serikali kufanya mambo kama watu wa mtaani na kuhoji kuwa kama yeye diwani ambaye ni kiongozi anafanyiwa hivyo wananchi wengine wasio na nyadhifa mahali popote wanafanyiwaje?

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Ferdinand Mtui amethibitisha kutokea kwa tukio na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea na kwamba hakuna mtu ambaye ameshakamatwa akihusishwa na tukio hilo.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Kigoma, Maurus Kitinusa alikanusha maofisa wake kumpiga diwani huyo na badala yake alisema kuwa walimtoa nje kwa nguvu baada ya kutaka ndugu yake apewe dhamana huku mahojiano kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili mtuhumiwa yakiwa hayajafanyika.

google+

linkedin