8/15/16

Muhimbili yainuka kimapato, yakusanya bilioni 5 kwa mwezi


HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili ya jijini Dar es Salaam, katika kukabiliana na changamoto za ufinyu wa bajeti zinazotolewa na hazina, imeamua kuacha utegemezi na kuweka mikakati inayopunguza matumizi na kuiongezea mapato taasisi hiyo ya matibabu.

Takwimu za Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha hospitali hiyo zinaonyesha kuwa, kibubu cha Muhimbili sasa kinapasuka, zamani kilikuwa kikikusanya Shilingi bilioni 2.3 kwa mwezi lakini sasa makusanyo yamefikia bilioni 4.8.
Je, ni namna gani ilivyoongeza mapato yake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma hospitalini hapo, Aminiel Aligaesha, anaelezea zaidi katika makala hii, akitaja, kuachana na matumizi ya karatasi na kutumia kompyuta, hospitali kuagiza dawa kutoka nje kuwa ni moja ya mambo yaliyoleta mafanikio.
Anaongeza kuwa imebana matumizi ya gharama za uendeshaji kwa kupunguza uchapishaji wa nyaraka za wagonjwa kwa kutumia makaratasi na sasa kazi hiyo hufanywa kwa kutumia mtandao wa kompyuta.
Anafahamisha kuwa hospitali imeanzisha utaratibu wa kutumia kompyuta ili kuweka na kutunza rekodi za wagonjwa badala ya matumizi ya mafaili ambao ni mfumo wa kizamani na wenye gharama.
"Hii imepunguza gharama za steshenari hasa karatasi , majalada na peni hivyo fedha hizo zinatumika katika matumizi mengine hasa kuboresha huduma za hospitali. Mfano maabara tulikuwa tunanunua mabunda 100 ya karatasi kwa mwezi kuandika taarifa za matokeo ya vipimo kwa wagonjwa, kwa sasa majibu yote yanapatikana kwenye kompyuta hakuna gharama za karatasi,"anasema.
Aligaesha anabainisha kuwa aidha uwepo wa huduma bora na kuongezeka mapato umetokana ununuzi wa dawa kutoka nje . Mathalani, baada ya kupata kibali kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), hospitali imenunua dawa zinazotumiwa na wagonjwa wanaopandikiziwa viungo kwa mfano figo ziitwazo ‘immunosuppressant’ ili kuzuia mwili usikikatae kiungo kigeni.
Dawa hizo ziliagizwa kutoka India kwa gharama ya Shilingi milioni 226 wakati ununuzi huo kama ungefanyika nchini zingegharimu milioni 500, anaongeza.
Pia anasema kwa mkakati huo hospitali imeagiza nyuzi za kushonea wagonjwa waliofanyiwa upasuaji kutoka kiwanda cha Ethicon kwa gharama ya Shilingi milioni 321 wakati zingeagizwa na kampuni nyingine zingefikia Shilingi milioni 668.
"Tumeweza kupunguza gharama za uchujaji wa damu (dialysis) kutoka wastani wa Shilingi 250,000 kwa kila zamu na kufikia 171,000 matibabu ya kijumuisha dawa ya ‘heparin’ inayozuia damu kuganda na huduma nyingine. Hivyo hospitali imewahudumia wagonjwa 31 ambao hawawezi kulipia gharama hizi. Hii ni hatua kubwa," alisisitiza.
Pia anaeleza kuwa hospitali imeunganisha mashine za CT Scan, X Ray na MRI katika mtandao wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehema) ili kuhakikisha picha zote zinazofanyika katika idara hiyo zinaonekana na kupata idadi ya wagonjwa waliofanya vipimo na kulinganisha kiasi cha mapato kilichokusanywa kama kinaendana na picha zilizofanyika kwenye mashine hizo.
"Katika mpango huu tumeunganisha wodi zote kuweza kuangalia majibu ya picha za CT scan, X ray na MRI kupitia kompyuta zilizopo wodini na kliniki,"anasema.
Anasema kuwa tiba ya figo imeimarika na kwamba kuna mashine 17 za kuchuja damu na pia kuboreshwa kwa huduma ya tiba kwa magonjwa ya tumbo na ini.
Aidha, anasema Muhimbili imeanza kufanya upasuaji kwa njia ya hadubini (Laparascopic Surgery) hususani kwa magonjwa ya masikio, pua na koo na katika eneo hilo, idara ya tiba hizo inaongoza katika matumizi ya teknolojia hiyo mpya.
“Si hivyo tu tumeanza upasuaji wa macho kwa kutumia vifaa vya kisasa , kuimarisha huduma za uuguzi na pia kwenye tiba na afya ya akili" anabainisha.
Huduma nyingine zilizoboreshwa anazitaja kuwa ni kupanua Idara ya Kinywa na kwa upande wa maabara vimewekwa vifaa vipya vya kisasa katika kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ubora wa hali wa ya juu.
"Tuna mashine mpya iitwayo ‘Architect Analyzer C4100’, mashine moja inaweza kupima vipimo zaidi ya 1,200 kwa saa moja ili kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri muda mrefu ili kupata majibu ya ya uchunguzi," anasema na kuongeza:
"Uwepo wa famasi mbili zinazofanya kazi kwa saa 24 na kuhakikisha idara zote 18 za tiba zina watalaamu bingwa ni miongoni mwa mafanikio yetu.”
Akielezea zaidi kuhusu mapato na matumizi, anasema hadi Septemba mwaka jana hospitali ilikuwa ikijiendesha kwa hasara kwa sababu mapato waliyokuwa wakikusanya yalikuwa ni Sh. bilioni 2.3 wakati matumizi yalikuwa bilioni 4.8.
Aligaesha anasema Muhimbili kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za uendeshaji na katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa zinazosababishwa na upungufu au ukosefu wa fedha.
Anasema ili kukabiliana na changamoto hizo, hospitali sasa inapunguza gharama za uendeshaji na kuongeza mapato ikiwamo kupunguza matumizi ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma kwa ufanisi kwa wagonjwa.
Katika kuongeza mapato, anasema uongozi umeweka mikakati kadhaa ambayo ni kutumia benki katika ukusanyaji mapato ili kudhibiti upotevu na wizi.
Pia anataja mikakati inayoanza mwezi ujao wa kuanzisha huduma za malipo kwa kadi maalumu, kadi za benki na mitandao ya simu ambazo wanaamini zitapunguza au kumaliza tatizo la upotevu wa fedha kupitia mikononi mwa watumishi wasio waaminifu.
“Kuboresha wodi za kulaza wagonjwa wanaohitaji huduma na malazi binafsi, kuhakikisha kila mgonjwa anayetakiwa kuchangia huduma anachangia, kadhalika kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaotumia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) na wa bima nyingine na wateja binafsi," anasema.
"Kuimarisha mfumo wa kuandaa hati za madai ya huduma kwa kampuni na NHIF.Tutaharakisha uandaaji wa ankara za wagonjwa hao tayari kwa kupelekwa NHIF na hospitali ili kulipwa kwa wakati. Itasaidia kupunguza makato yasiyojazwa kikamilifu ama yaliyokataliwa ambazo hospitali imekuwa ikizipata baada ya kuhudumia wagonjwa hao na hata wengine kuonekana siyo wachangiaji hai wa mfuko huo," anasema.
Pia anasema hospitali imesaidia mfuko wa bima kuunganisha na mfumo wa hospitali kutambua wanachama ambao siyo hai lakini bado wanaendelea kupata huduma.
Kadhalika anataja nyingine ni kutoa motisha na kuwahamasisha madaktari kuwaona kwa wingi wagonjwa wanaolipa ili kuwavutia kutibiwa MNH.
"Kutoa motisha kwa wafanyakazi wengine wanaohudumia wagonjwa ili kuongeza ari ya ufanyaji kazi, mipango hii imekwisha anza kutekelezwa na kwamba kutokana na hilo, mapato ya hospitali yameongezeka maradufu. Kwani mwezi Desemba mwaka jana ilikuwa bilioni 2.3 lakini sasa tunazungumzia Shilingi bilioni 4.8 zilizokusanywa mwezi Mei mwaka huu," anasema.
Kuhusu upunguzaji wa matumizi Aligaesha anasema hospitali imejiwekea mikakati wa kupunguza gharama za manunuzi pale inapowezekana na moja ya mikakati hiyo ni kununua dawa na vifaa tiba kutoka viwandani au moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts