8/16/16

Ndege za ATCL zatarajiwa kuingia nchini mwezi ujao


Shirika la ndege la ndege Tanzania (ATCL) linatarajia kuingiza nchini ndege zake mpya mbili mwishoni mwa mwezi ujao.
ndege-atcl_478_316
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, ujio wa ndege hizo utaleta mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa kampuni hiyo. Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa ATCL Patrick Itule, alisema Dar es Salaam kuwa ujio wa ndege hizo utairejesha kampuni hiyo kwenye biashara ya ushindani dhidi ya kampuni nyingine za ndege hapa nchini.
Ndege hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Bombardier ya nchini Canada zinatarajiwa kuingia nchini wiki ya tatu na ya nne ya Septemba, mwaka huu na zitakuwa zikipishana kwa wiki moja.
“Baada ya ujio wa ndege hizi hatuoni tena sababu ya sisi kukwama, tutakuwa tumeingia rasmi kwenye biashara ya ushindani kwa kuwa changamoto kubwa ya uhaba wa ndege ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa itakuwa imeanza kutatuliwa,’’ alibainisha Itule.
Alisema ATCL tayari imeunda kikosi kazi kinachosimamia masuala mbalimbali, likiwemo la mafunzo ya watendaji wake mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwa sasa.
Naye Ofisa Biashara wa ATCL, Josephat Kagirwa alizungumza uwezo wa ndege hizo kuwa zina uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na kwamba ujio wake utaongeza njia za kusafiri kwa kampuni hiyo kutoka njia mbili za sasa hadi kufikia njia zaidi ya kumi.
“Tutakuwa na madaraja mawili, yaani daraja la uchumi litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege,” alisisitiza.
Kampuni hiyo ilitoa shukrani zaidi zikielekezwa kwa Rais Dkt John Magufuli kwa jitihada zake za kufufua rasmi ATCL.
CHANZO: HABARI LEO
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts