8/15/16

Reli ya kisasa kuchukua miaka 3


SERIKALI imesema reli ya kisasa (Standard Gauge) itajengwa kwa miaka mitatu kuanzia Desemba mwaka huu na ujenzi wake umegawanywa kwa awamu nne ili kuharakisha kumalizika kwake.
Kiasi cha Sh. trilioni 16 kinatarajiwa kutumika kukamilisha ujenzi huo huku serikali ikitenga Sh. trilioni moja kwa ajili ya mradi huo katika mwaka huu wa fedha ili kuwavutia wazabuni kujenga reli hiyo ya kisasa yenye urefu wa kilomita 2,561.
Taarifa iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilino, ilieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano wa sita uliowakutanisha Mawaziri wa Sekta ya Uchukuzi wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi, uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuangalia namna bora ya kupunguza vikwazo kwenye sekta hiyo baina ya nchi hizo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa ushirikiano baina ya nchi za Afrika Mashariki katika ujenzi wa reli hiyo utachochea kasi ya usafirishaji wa mizigo na shughuli za kibiashara na hivyo kuinua uchumi wa nchi hizo.
Katika taarifa hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alikaririwa akisema: “Kama mnavyojua serikali imetenga kiasi cha Sh. trilioni moja kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo na wenzetu nao watatafuta fedha katika nchi zao ili kukamilisha ujenzi wake."
Aidha, waziri huyo alibainisha kuwa kila nchi itatekeleza mradi wa kujenga reli ya kisasa kwa sehemu yake hivyo ni wajibu wa kila nchi kukamilisha mradi huo ili kuchochea maendeleo yanayotokana na sekta ya uchukuzi.
Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania, reli hiyo itaanza kujengwa kuanzia Dar es Salaam ikipitia Tabora, Isaka (Shinyanga) hadi Mwanza na itakuwa na urefu wa kilomita 1,219 ambao ndio uti wa mgongo wa reli yenyewe na sehemu nyingine ni kutoka Tabora hadi Kigoma kupitia Mpanda, Kalemela, Tabora na Uvinza.
Ili kuunganishwa na nchi za Rwanda na Burundi, Profesa Mbarawa alisema ujenzi wa reli hiyo itajengwa kuanzia Isaka na kuiunganisha na miji ya Rusumo, Kigali, Keza na Musongati.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Waziri wa Uchukuzi wa Burundi, Mhandisi Jeon Ntunzwenidana, alifurahishwa na Serikali ya Tanzania katika jitihada zake za kuharakisha ujenzi wa reli hiyo na kusema kuwa Serikali ya Burundi itakamilisha ujenzi huo haraka ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na huduma za kibiashara baina ya nchi hizo.
Katika mkutano huo, Profesa Mbarawa pia alisaini makubaliano ya uboreshwaji wa sekta ya mawasiliano, reli na barabara baina ya nchi za Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts