8/29/16

Serikali kubadili mtaala wa elimu wa darasa la tatu na la nne

Wahitimu wa darasa la saba Shule ya Awali na Msingi ya Genius Kings ya jijini Dar es Salaam, wakiwa kwenye picha ya pamoja. Picha na Hussein Makame-MAELEZO.

SERIKALI inajianda kufanya mabadiliko ya mtaala wa elimu wa darasa la tatu na la nne ili kukidhi mahitaji ya elimu nchini ambayo yanabadilika kulingana na muda.

Akizungumza kwenye mahafali ya tano ya Shule ya Awali na Msingi ya Genius Kings mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Elimu wa manispaa ya Ilala Asha Mapunda, alisema tayari mitaala ya darasa la kwanza na la pili imeshabadilishwa.

Mapunda aliwataka wamiliki na waendeshaji wote wa shule binafsi katika manispaa ya Ilala kuzingatia kwa ukamilifu taratibu na sheria za nchi katika uendeshaji wa shule binafsi.

“Zingatieni pia mitaala inayotolewa na Serikali.Hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko katika mtaala ya madarasa ya kwanza na pili, kutakuwa pia na mabadiliko ya mtaala katika madarasa mengine la tatu na la nne” alisema Mapunda na kuongeza kuwa: “Hivi ninavyosema kuna baadhi ya walimu wetu wa darasa la tatu na la nne wako kwenye mafunzo.Lakini nina hakika kabisa hata shule za binafsi zitapata mafunzo hayo, kwa hiyo wala msijali.”

Aliwataka wamiliki na waendeshaji wa shule binafsi wasisite kuwasiliana ofisi ya elimu ya manispaa ya Ilala pindi wanapotaka ufafanuzi au maelekezo kutoka serikalini yanahitajika na Serikali itakuwa tayari kutoa msaada wowote utakaohitajika.

Alisema Serikali kwa ujumla na Manispaa yake inatambua mchango wa shule za binafsi katika kuendeleza elimu na inasisitiza na kutia moyo uwekezaji wa sekta binafsi katika nyanja ya elimu, kwani imedhihirika kwamba shule binafsi zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya elimu nchini.

“Serikali kwa upande wake itaendelea kusaidia jitihada hizi kwa sera na miongozi ambayo imetolewa ili kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya elimu” alisema Mapunda na kuongeza kuwa:

Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo Machage Kisyeri alisema mafanikio ya shule hiyo yametokana na filosofia yao ya kuamini katika kujenga uwezo wa mtoto kimaadili, kinidhamu na umahiri wa kitaaluma.

“Genius pia tunaamini kuwa kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa yote, hivyo shule yetu imeweka utaratibu mzuri unaowapa watoto wote wa dini tofauti fursa ya kufanya ibada pamoja na viongozi wa dini ambao tunafanya kazi nao kwa karibu sana” alisema Kisyeri.

Naye Mkuu wa shule hiyo Aloyce Siyame alisema katika mahafali hayo wanafunzi 65 wanatarajiwa kuhitimu mwaka huu ambapo kati yao 23 ni wanawake na 42 ni wanaume.

Takwimu zinaonesha ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu mitahani ya darasa la saba kutoka katika shule hiyo umekuwa ukiimarika kila mwaka ambapo mwaka 2013 wanafunzi wanne kati ya wahitimu 32 walipata daraja A na mwaka 2015 wanafunzi 40 kati ya walihitimu 57 walipata daraja A.

Aidha udahili wa wanafunzi wa shule hiyo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2013 wanafunzi 32 walihitimu na mwaka jana wanafunzi 57 walihitimi huku kukiwa na mwanafunzi mmoja tu aliyefaulu kwa wastani wa daraja C.

Akizungumzia nafasi ya shule hiyo katika shule bora kwenye mitihani ya kitaifa, Mkurugenzi Kisyeri alisema shule hiyo ilishika nafasi ya saba katika mithani ya mwaka 2013 hadi nafasi ya tano katika mitihani ya mwaka jana katika manispaa ya Ilala.

Akizungumzia umuhimu wa michezo, Mkuu wa shule Siyame alisema Watanzania wengi hawana mwamko wa michezo, huku wazazi na wadau wa elimu bado wakiiona michezo kama chanzo cha mmomonyoko wa maadili na kupunguza morali ya kusoma shuleni.

“Kwa upande wangu ninaona wakati umefika kwa Watanzania kubadilika kifikra kwani michezo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, pia inasemekana sasa hivi michezo ni ajira yenye malipo makubwa sana kwa hiyo tuwape fursa na tuwawezeshe watoto wetu kushiriki katika michezo.

Shule ya Genius Kings ilianzishwa mwaka 2008 ambapo baadhi ya wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kumaliza elimu msingi hupatiwa udhamini wa masomo yao ambapo kwa mwaka huu ni wanafunzi watato watasomeshwa hadi kidato cha nne.
 
-Michuzi Matukio
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts