Serikali yashikilia msimamo kupinga ndoa za jinsia moja. | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/31/16

Serikali yashikilia msimamo kupinga ndoa za jinsia moja.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kushikilia msimamo wake wa kupinga ndoa za jinsia moja,kuongeza uwigo wa uhalalishaji  wa utoaji mimba,adhabu ya kifo,kuweka sera ya kutonyonga wanaokutwa na adhabu ya kifo na uridhiwaji wa mikataba ya Kimataifa inayozuia masuala ya utesaji kwa kuwa masuala hayo yanaonekana kutoendana na Katiba na Sheria za nchi, Sera,mila desturi na tamaduni za watanzania ikiwa ni sehemu ya mapendekezo  72 yaliyokataliwa na Serikali  wakati wa mapitio ya taarifa ya nchi ya ukuzaji na usimamizi wa haki za binadamu.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ndugu Gerson Mdemu ameyasema hay oleo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga kikao maalumu cha siku mbili cha wadau  mbalimbali wa masuala ya haki za binadamu ambapo ameeleza  kuwa Serikali ilipokea jumla ya mapendekezo 227 yaliyotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mwezi Mei 2016 chini ya mfumo wa mapitio kwa kipindi maalum (The Universal Periodic Review).
Mdemu ameongeza kuwa  mapendekezo hayo kwa ujumla yalijikita katika  majukumu ya Tanzania kwenye mikataba ya kimataifa ,Mifumo ya kikatiba na kisheria,miundombinu ya kitaasisi ya haki za binadamu ,masula ya kisera,ushirikiano na vyombo vya kikanda na kimataifa,utawala wa sheria,uendeshaji haki,masuala ya kulinda haki za msingi za binadamu kama vile haki ya kuishi,haki ya afya,haki za walemavu,watoto,haki ya habari na kujieleza,afya elimu mazingira haki za watu asilia na wakimbizi.
Hata hivyo, Tanzania ilikubali kutekeleza mapendekezo 130 tu kati ya 227 yaliyokuwa yanahusu mchakato wa Katiba,kuijengea uwezo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kuhuisha Sera za nchi ili ziendane na malengo endelevu ya Dunia ,kuandaa taarifa za nchi za utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu na kuziwasilisha kwenye vyombo vya vya umoja wa mataifa kwa wakati.
Vilevile  Serikali iliahirisha jumla ya mapendekezo 25 ambayo yalijikita katika marekebisho ya sheria ya Takwimu, 2015, Sheria ya makosa ya mtandao, 2015,ukamilishaji wa Sheria ya Habari, Sheria ya vyombo vya Habari,uandaaji wa mikakati na mipangokazi ya utekelezaji wa msuala ya kuzuia ndoa za utotoni na za kulazimishwa ,upitishaji wa sera mpya mbalimbali ikiwemo ya kutoa vyeti vya kuzaliwa na usajili wake kuwa bure na masuala ya uchaguzi Zanzibar,  kwa lengo la kuyapitia tena kwa kina na kushirikisha zaidi wadau ili hatimaye kuweka msimamo stahiki kabla mapendekezo hayo hayajawasilishwa tena Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa hatua za mwisho za kupitisha rasmi taarifa ya nchi katika kukuza na kulinda haki za Binadamu.
Aidha, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametumia  fursa hiyo kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda na kukuza haki za bindamu ikiwa ni pamoja na kupokea hoja na maoni ya wadau ili kuboresha taarifa ya nchi itakayowasilishwa katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja wa mataifa kabla au ifikapo tarehe 9 Septemba, 2016 na kuwataka watanzania wote kushiriki ipasavyo katika dhana nzima ya kukuza na kulinda haki za bindamu  nchini.
Utaratibu wa Mapitio kwa kipindi maalum (The Universal Periodic Review) wa masuala ya haki za binadamu ulianzishwa na Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 2006 kwa lengo la kuzifanyia mapitio nchi 192 ambazo ni wanachama wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ikiwa miongoni, kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa masuala ya kulinda na kukuza haki za binadamu nchini mwao.

google+

linkedin