8/6/16

Show bila Singeli, Haikamiliki Siku hizi, Singeli kila kona

Msanii wa muziki wa singeli, Mc MakabilaUnachukua umaarufu mkubwa katika majukwaa ya sanaa kwa sasa nchini, kwani bila muziki wa ‘Singeli’ shoo haijakamilika. Licha ya hivyo mashabiki wanaona ni moja ya burudani muhimu kwa kila shoo inayoandaliwa hivi sasa.

Licha ya kujichukulia umaarufu mkubwa, bado kuna maswali kuhusu muziki huu hasa asili yake huku wengi wakihisi unatokana na kabila fulani.

Amani Hamisi ,24, maarufu kwa jina la Man Fongo, ndiye aliyeanza kutamba na muziki huu, kupitia nyimbo mbalimbali kabla hajatoka rasmi kimuziki.

“Mwaka 2010 nilianza kuimba muziki wa Singeli lakini Tanzania wamenielewa mwaka 2016, singeli ilikuwa inapigwa mtaani tu, uswahilini watu walikuwa wanakodisha muziki na Man Fongo kwenda kuimba kwa hiyo nikienda nalipwa Sh100,000 au Sh200,000 na sikuanzia hapo nilianza kulipwa fedha ndogo sana,” anasema Man Fongo.

Akielezea asili ya muziki huo, anasema yeye alianzisha staili hiyo uswahilini na malengo yake uwe wa kuchezeka na mtu ambaye hajielewi yaani ilikuwa wa kuburudika tu na kwamba hata jina la muziki huo alitunga.

“Singeli ni muziki wa Tanzania, uliitwa hivyo kwa sababu ni kama mchezo fulani wa kucheza kama hauna akili, yaani unajichetua kama katuni ilimradi watu wawe wanafurahi kukutazama,” anasema.

Anasema muziki wake ni tofauti na ule unaoimbwa na Msaga Sumu, kwani yeye anarap huku singeli inaimbwa kwa uharaka kama Bongo Fleva

Hata hivyo, anasema ana mipango ya kuuboresha muziki huo kwani vijana wengi wamekuwa wakiimba ndivyo sivyo na kuegemea masuala ya uhusiano wa kimapenzi pekee.

Ikiwa tamasha la Fiesta mwaka huu linatimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, mashabiki na wadau wa burudani nchini kwa mara ya kwanza wanaweza kupata ladha ya miondoko ya muziki ya singeli. Mashabiki waliozungumza na gazeti hili kuhusiana na tamasha hilo wameeleza matumaini yao ya kupata ladha ya muziki huo kutokana na kuwa ndiyo habari ya Mjini.

Awadh Kilabu anasema anasubiri kwa hamu kuona ama kuhudhuria shoo ya tamasha hilo ikiwa imekusanya waimbaji mahiri wa singeli kwa sababu ni miondoko anayoipenda.


Anasema hata wakipanda jukwaani kutumbuiza mapema au usiku sana atasubiri kwa sababu siku zote amekuwa anahudhuria shoo zao kwenye vurugu lakini katika tamasha hilo itakuwa ni eneo sahihi la kujiachia.


Akizungumzia tamasha hilo ambalo mwaka huu linadhaminiwa na kampuni ya Tigo , Nicolaus Sikole anasema tofauti na miaka mingine wasanii wa bongofleva walikuwa wanafunika mwaka huu wasanii wa singeli watavutia zaidi mashabiki.


“Unajua hivi sasa kila mtu anapenda miondoko hiyo, wa kishua hawawezi kujichanganya uswahilini kuicheza, lakini katika fiesta tutajichanganya pamoja, ”anasema Sikole.


Sikole anasema mwaka juzi alikuwa na safari siku ambayo tamasha hilo lingefanyia Dar hivyo alilazimika kulifuata Morogoro kutokana na kutotamani kulikosa.


Nae Magdalena John Mkazi wa Kimbiji jijini Dar es Salaam anasema tamasha hilo mwaka huu litamlaza hotelini kwa mara ya kwanza ili ahudhurie bila kupata usumbufu wa usafiri wa kwenda na kurudi usiku wa manane.


Anasema angekuwa na uwezo angewaomba waandaaji pamoja na burudani nyingine singeli isikose laivu jukwaani hasa mwimbaji Man Fongo kwa sababu anamzimia sana.


“Unajua kwa ubize wa mji huu ni ngumu kujichanganya kwenye midundo hiyo ninayoipenda, lakini naamini katika tamasha patachimbika nitajiachiaje, ”anasema John.


John anasema ni katika tamasha hilo pekee ndiyo atakakokata kiu ya muziki huo ambao bado unadhaniwa ni wa vurugu.


Naye mkazi wa Kimara Temboni, Ruth Michael anasema pamoja na kupenda burudani mbalimbali zinazotolewa katika tamasha hilo, wakiwamo wasanii wa ndani na nje ya nchi kama ilivyo ada anatamani kuona wasanii wa miondoko hiyo laivu.


Anasema kwanza haamini kama wanacheza bila vurugu, haamini kama wataimba kama anavyosikia kwenye redio na kuwaona kwenye televisheni, hivyo ni nafasi ya pekee kwake kupata majibu ya maswali hayo.


Anasema katika mikoa 15 ambayo tamasha hilo litazunguka kuonyesha burudani atakwenda mikoa miwili bila kukosa Dar ambako huwa funika bovu, “Weeeee Dar lazima niwepo hata kama nikiwa nina homa nitajikaza vivyo hivyo, ”anasema.


Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo Prime Time Promotions, litaanzia rasmi mkoani Mwanza na kufuatiwa na mikoa ya Kahama, Bukoba, Musoma, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara, Iringa, Mbeya na Dar es Salaam.


Akizungumzia udhamini wa tamasha hilo Ofisa Mkuu wa Biashara wa tigo Shavkat Berdiev anasema, “Ikiwa ni kampuni iliyojikita katika kukuza sekta ya muziki wa ndani, tunayo furaha kuwa wadhamini wakuu wa tamasha hili kubwa la muziki nchini Tanzania.


Anasema lengo lao kila mara limekuwa ni kunyanyua wasanii wa ndani kupitia majukwaa ambayo yatawawezesha kuonyesha vipaji vyao ikiwamo jukwaa la fiesta.


Mkurugenzi Mtendaji wa Prime Time Promotions Joseph Kusaga anasema wataendelea na harakati za kuendeleza vipaji vya wasanii wapya na wanaoibukia katika muziki hususani wa vijana.


Anasema ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 15 ya kuwapo kwa tamasha hilo “Mwaka huu tutaendesha kampeni maalum inayojulikana kama ‘Kipepeo’ kwa ajili ya kuwatambua na kuwasaidia wasichana wenye mahitaji maalumu katika mikoa 15 ambako tamasha hili litafanyika.”


Mwanahip Hop mkongwe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Joseph Haule maarufu Profesa J anasema kuwa muziki huo unaweza kuwa na nguvu kuliko mwingine kwa sasa hapa nchini.


Anasema alipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita ndiyo kwa mara ya kwanza alibaini nguvu ya miondoko hiyo kutokana na kukonga nyoyo za watu.


“Tatizo moja tu la miondoko hii ya muziki yenye mchanganyiko na ladha ya chakacha, mchiriku, vanga, mdumange ni jinsi waimbaji wa nyimbo hizo walivyojiweka kisela sana,” anasema Profesa J.


Anashauri kuwa iwapo waimbaji wa muziki huo wakiungwa mkono kama alivyofanya yeye kwa kumshirikisha msanii Sholo Mwamba katika wimbo wake mpya uitwao “Kazi Kazi”, wanaweza kubadilika na kufanya kitu tofauti.


Anasema ni ngumu hivi sasa wasichana warembo, kina mama na kina kaka wanaojipenda na wastaarabu kwenda unakochezwa muziki huo kwa sababu kuna hatari wakaibiwa kila kitu kutokana na wasanii, mashabiki wa muziki huo kuwa na mchanganyiko wa wezi, wakabaji, wavuta unga na walevi.

“Katika mchanganyiko huo wa watu kitu chochote kinaweza kutokea, zaidi ikiwa ni uhalifu, nimejitokeza kuwaunga mkono ili kuufanyia promo ikiwamo kuvutia wawekezaji watakaoona umuhimu wa kuuinua, ” anasema.

Anasema kuna namna ambayo inaweza kutumika kubadili upepo wa waimbaji wa muziki huo kwa kuwatumia wao kwa wao kutunga mashairi ya kukataza matumizi ya silaha na vitendo viovu katika mashairi yao badala ya sasa wanavyotunga ya kuhamasishana kutenda maovu.

Naye mwimbaji Sholo Mwamba anasema kuwa mipango ya kubadili uchezaji, uvaaji wa wasanii wa singeli ipo isipokuwa kinachohitajika ni nguvu na elimu kabla ya kufanya mabadiliko.

Anasema wasanii wengi wa muziki huo walianza kama masihara na sasa imekuwa ajira yao, hivyo wanahitaji kuelimishwa na kupewa nafasi ili waone faida.

ya kuubadili muziki huo na kuwa ajira kwao.

“Siamini kama mtu anapata mafanikio katika kitu fulani anaweza kukiharibu, kama watapata elimu, wakapata nafasi ya kufanya shoo mbalimbali zikawalipa naamini watabadilika, ”anasema Mwamba.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts