Uhakiki mkubwa wa namba za TIN waja | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/15/16

Uhakiki mkubwa wa namba za TIN waja


MAMLAKA ya Mapato (TRA) inakusudia kufanya uhakiki wa kina wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) nchi nzima, lakini kwa kuanzia na Mkoa wa Dar es Salaam leo.
Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Alphayo Kidata.
TRA imelazimika kufanya uhakiki huo mkubwa imesema: "Baada ya kubadili mfumo wake wa sasa wa kuhifadhi kumbukumbu za walipa kodi na kuweka mfumo wa kisasa uneoendana na ukuaji wa teknolojia."
Kwa mujibu wa tangazo la TRA kwenye gazeti la Nipashe la jana, zoezi linaanza rasmi leo kwa mikoa ya kodi ya Dar es Salaam ambayo ni Ilala, Kinondoni na Temeke, katika awamu ya kwanza kabla ya kusambaa nchi nzima.
"Wale wote watakaoshindwa kuhakiki au kuboresha taarifa zao, TIN zao zitafungwa au kuondolewa kwenye mfumo, hivyo hawataweza tena kutumia namba hizo," tangazo hilo lilionya.
Kila mlipa kodi atatakiwa kufika mwenyewe kwenye zoezi hilo ili kuhakiki pia alama za vidole zilizo kwenye mfumo wa TRA, imeelezwa.
Taarifa ya TRA ilisema zaidi kuwa wenye TIN za biashara watatakiwa kuboresha au kuhakiki taarifa katika ofisi za mikoa ya kodi ziliposajiliwa biashara zao, lakini wenye TIN zisizo za biashara wanaweza kufanya hivyo katika ofisi yoyote ya TRA ya mkoa au wilaya iliyo karibu.
Katika zoezi hili, vyeti vipya vya TIN vitatolewa, ilisema taarifa hiyo ya TRA.
Tangu kuingia madarakani Rais wa tano, John Magufuli Novemba 5, mwaka jana, mapato ya TRA yameongezeka kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 mpaka Sh. trilioni moja kwa mwezi.
MAKUSANYO
Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja wiki iliyopita, kwa mfano, ilionyesha TRA ilikusanya Sh. trilioni 1.055, sawa na asilimia 95.6 ya lengo la kukusanya Sh. trilioni 1.103 iliyopangiwa na Serikali kwa mwezi Julai 2016.
Makusanyo hayo ya Julai, hata hivyo, yanazidi kwa asilimia 15.43 ikilinganishwa na makusanyo ya mwezi kama huo mwaka jana, ambapo TRA ilikusanya Sh. bilioni 914.
Aidha, katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, TRA imewekewa lengo la kukusanya Sh. trilioni 15.1
ikilinganishwa na lengo la Sh. trilioni 13.32 la mwaka wa fedha uliotangulia wa 2015/16, taarifa ya Mwaipaja ilisema.
Ili kufikia azma hiyo, taarifa ilisema Mamlaka imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwamo kusajili
walipa kodi wapya pamoja na kuhuisha taarifa za walipakodi kwa kuziondoa katika mfumo wa TRA namba za TIN zisizotumika.
"Maandalizi ya kuhuisha taarifa za walipakodi yako katika hatua za mwisho yakihusisha kupigaji picha, kuchukua alama za vidole pamoja na vielelezo muhimu vya mlipa kodi ili kila biashara iwe na TIN moja tu na taarifa sahihi na za uhakika," taarifa ya Wizara ilisema.

google+

linkedin