8/22/16

Vigogo Chadema kufafanua dhana ya Ukuta kila kanda


Viongozi wa ngazi ya juu wa Chadema wameanza kutawanyika mikoani kutoa elimu ya kuhusiana na Ukuta.

Wakati mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akiwa Kanda ya Kaskazini, aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alikuwa mkoani Mbeya na jana alishiriki ibada kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Forest kabla ya kuanza vikao vya mkakati huo.

Mbowe jana alikutana na viongozi wa kanda hiyo na kuunda kamati zitakazokwenda katika majimbo yote 35 ya uchaguzi ya mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kutoa elimu.

Alisema katika kikao hicho ambacho ni mfululizo wa vikao vinavyoendelea kanda zote nchini, wamekubaliana kutoa elimu ya dhana ya Ukuta.

Hata hivyo, alisema bado chama hicho kimetoa fursa ya mazungumzo kwa taasisi yoyote ili kuhakikisha mgogoro uliosababisha Kamati Kuu kuunda Ukuta, unapatiwa ufumbuzi.

“Tutashiriki mazungumzo yoyote ya kusaka muafaka na kama matamko ya Rais John Magufuli yatabadilishwa. Tutawaeleza wanachama kusitisha mikutano ya Septemba Mosi na kuendelea na mikutano ya kawaida,” alisema Mbowe.

Wakati Mbowe akisema hayo, Lowassa alitua katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ambayo inajulikana kama Kanda ya Nyasa akihimiza mambo makubwa matatu.

Katibu wa Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe aliyataja mambo hayo kuwa aliwahimiza wanachama wote kuimarisha umoja na kufuta mipasuko iliyotokea wakati wa uchaguzi. Pili, aliwasihi wana Chadema wote kuwa jasiri kwa kupigania haki na kujitambua na la tatu ni kujiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Mwaisumbe alisema baada ya kikao cha jana, leo Lowassa anaanza kutembelea majimbo ambako atakuwa na vikao vya ndani.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts