Vipanya marufuku kuingia katikati ya mji Dodoma | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/31/16

Vipanya marufuku kuingia katikati ya mji Dodoma
Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchini Kavu (Sumatra) imesema haitatoa leseni mpya za usafirishaji kwa daladala zenye uwezo wa kuchukua abiria chini ya 41 kuingia katikati ya mji wa Dodoma ikiwa ni hatua ya kuepuka msongamano wa magari kama ule wa Jiji la Dar es Salaam.


Kwa sasa magari yanayotoa huduma za usafiri katikati ya mji ni ‘hiace’ maarufu kama ‘vipanya’ lakini katika mpango huo ni wazi sasa magari hayo itabidi kwenda kufanya shughuli zake nje kidogo ya mji wa Dodoma.


Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka hiyo, Conrad Shio alisema jana kuwa kwa sasa daladala zilizopo mjini hapa haziwezi kubeba abiria wengi lakini tayari wameshaanza mipango ya kuwezesha wadau kuwekeza kwenye usafiri huo.


Alisema mipango hiyo inafanyika ikiwa ni utekelezaji wa majukumu waliyopewa ya kuboresha usafiri mjini hapa katika Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana.


Alisema wataitisha mkutano wa wadau wa sekta ya usafirishaji ambao watendaji wa Kampuni ya Mabasi ya Mwendo Kasi ya jijini Dar es Salaam (Udart) ndiyo watakaotoa mada.


Shio alisema Manispaa ya Dodoma walikuwa wameandaa vibao kwa ajili ya alama ya vituo vya bodaboda na bajaji lakini kutokana na utaratibu huo waliwaambia wasimamishe kwa sababu hakutakuwa na vituo hivyo katikati ya mji.


Aidha alisema hakutakuwa tena vituo vya kuegesha daladala katikati ya mji na badala yake vituo vya kushushia na kupakia abiria vitapanuliwa.


Alitoa wito kwa wamiliki wa daladala kuanza kuwekeza kwenye mabasi yenye uwezo mkubwa wa kubeba abiria.


Alipoulizwa iwapo wameshapokea maombi ya daladala hizo, Shio alisema hakuna biashara inayolipa kama ya usafirishaji.


“Hata Dar es Salaam watu walisema zinaondolewa ‘hiace’ katikati ya mji watu watapata shida ya usafiri lakini baada ya kuziondoa tu, magari makubwa yalijaa,” alisema.


Kwa mujibu wa ofisa huyo, mji wa Dodoma una daladala zipatazo 1,300 kati ya hizo 980 ni vipanya ambavyo vina uwezo wa kubeba abiria kati ya 15 na 16 wakati gari zenye uwezo wa kubeba abiria 26 hadi 29 ni 390.


“Haya 390 mengi ni ya zamani, yamechakaa utakuta machache tu yapo barabarani mengine gereji,” alisema.


Alisema kwa kuzipa daladala kubwa fursa ya kutoa huduma ya usafiri kutasaidia kupunguza wingi wa mabasi barabarani kwa sababu gari moja lenye uwezo wa kubeba abiria 41 linachukua nafasi ya vipanya vinne.


Alipoulizwa iwapo daladala kubwa zinaruhusiwa kusimamisha abiria, Shio alisema utaratibu wa kusimamisha abiria siyo wa kisheria ila ni wa hekima.


“Yakija yale magari makubwa ambayo yanawekwa kamba za kushikilia abiria ndiyo yanayoruhusiwa kisheria kwa sababu hata zile kamba zinahesabika kama uwezo wa kubeba abiria,” alisema.


Alisema ni vyema wadau wa usafirishaji wakajiunga na kuunda kampuni ya usafirishaji ili kuweka urahisi kwenye ufuatiliaji, usimamizi na ushauri.


Shio alisema mipango hiyo tayari imeingizwa kwenye mipango mikakati na kukubaliwa na sasa kinachofuata ni utekelezaji.


Alisema magari yatakayokuja kufanya biashara ya usafirishaji mjini hapa yatakaguliwa kwa umakini mkubwa na polisi kwa kushirikiana na Sumatra ili kuzuia magari mabovu.


“Hatutaki magari mabovu katika mji wetu yaje kutusumbua, tutahakikisha tunafanya ukaguzi ipasavyo,” alisema.


Hata hivyo, alisema wakati wakiendelea na utekelezaji wa mpango mkakati huo, Sumatra itaongeza urefu wa ruti katika baadhi ya maeneo yasiyofikiwa na huduma hiyo ili kuwapunguzia mzigo wa kukodisha bajaji na bodaboda wakazi wa mji huo.


“Ruti nyingi ni za kilometa 4, nyingine 3.5 hadi kilometa 2. Sasa tumeishauri Sumatra iongeze ukubwa wa ruti hadi kilometa 13.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti madereva wa daladala mjini hapa walisema wanafurahia ujio wa makao makuu na kuishauri Serikali kuondoa changamoto zilizoko kwenye sekta hiyo.


Dereva wa daladala zinazofanya safari zake kati ya Jamatini na Udom, Aikael Kweka alishauri kuongezwa kwa ukubwa wa stendi ya daladala ya Jamatini ili kuondoa msongamano wa daladala kwenye kituo hicho.
 
chanzo: Mwananchi

google+

linkedin