8/5/16

Wabunge Chadema waiona damu kumwagikaWABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Kaskazini, wamewaomba viongozi wa dini, kumshauri Rais John Magufuli kuviachia uhuru wa mikutano vyama vya siasa, ili kuepusha damu kumwagika Septemba Mosi, mwaka huu, katika operesheni Ukuta.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, alisema kama chama hawatamjaribu Rais Magufuli kama alivyoonya, bali wanamwarifu kuwa watafanya maandamano siku hiyo kudai uhuru wao kama vyama vya siasa wa kufanya mikutano na maandamano kwa ajili ya kujenga demokrasia.

“Lakini wakati tunasuguana tunawaomba maaskofu, mashehe na wachungaji wamshauri Rais wetu ili atuachie uhuru huu ambao umo ndani ya Katiba aliyoapa kuilinda, ambayo inatambua kila mtu ana uhuru wa kuabudu na kufanya chochote,” alisema.

Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, alisema hivi sasa kuna kuminywa demokrasia kwa kiwango kikubwa, hivyo watafanya maandamano kudai uhuru wa kikatiba ambao serikali imeupokonya.

Alisema suala la kuruhusu mtu aliyeshinda kufanya mikutano eneo lake hilo pia wanalipinga sababu kufanya hivyo ni kuua demokrasia, kwa kuwa inamaanisha chama hakina mwakilishi au hawana wao wenye uakilishi baadhi ya maeneo hawataweza kufanya mkutano, hivyo chama hakiwezi kukua.

“Lakini tumeshuhudia wakati rais anasema haya, tumemwona Christopher Sendeka ambaye si Mbunge, alifanya mkutano Longido hivi karibuni, hivyo hili la kutubana sisi wapinzani tu hatukubaliani nalo,” alisema.

Lema alisema pia anajiandaa kuandika barua kuomba mkutano wa hadhara ambao ataeleza sababu ya kuomba ni kutaka kukosoa bajeti kandamizi.

Naye Mwenyekiti wa Wabunge wa Kanda ya Kaskazini, Joseph Selasini, alisema wanaunga mkono maazimio ya kamati kuu ya kufanya mikutano na maandamano isiyo na ukomo ili kupinga kile alichodai udikteta unaofanywa na Rais John Magufuli.

Alisema Rais anaendesha nchi kwa kuua demokrasia iliyoasisiwa na waliomtangulia, jambo ambalo wao hawakubaliani nalo.

“Hali hii lazima tuipinge kwa nguvu, maana madhara yake ni makubwa na matokeo yake Tanzania haiwezi kuwa na maendeleo maana Rais hataki kukosolewa,”alisema.

Pia alisema wanataka Mbunge mwenzao Tundu Lissu, aachiwe huru au apelekwe mahakamani, kuliko kuendelea kumzuia polisi, kwa kuwa itaamsha chuki na hasira ya kusababisha vurugu.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alisema anamshauri Rais Magufuli afanye kazi kama kaulimbiu yake inavyosema ili ajihakikishie ushindi mwaka 2020 na si kutaka kurudi Ikulu kwa kuminya demokrasia.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts