8/30/16

Walimu wakuu mkoani Simiyu wawekwa 'kikaangoni'


“Tukitaka kufanikiwa katika elimu ni lazima tukubaliane na mabadiliko yatakayotokea...
.....nashangaa pia kuona walimu wakuu, waratibu elimu wameanza kuwa na hofu ya kuondolewa katika nyadhifa zao…na bila kuficha ni lazima kuwe na mabadiliko ya wakuu wa shule watakaoendana na kasi ya utendaji kazi wa sasa …" Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, anaanza kuzungumzia mwenendo wa elimu mkoani humo.
Mtaka anasema, kumekuwa na gumzo na sintofahamu kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, baada ya kusikia taarifa zilizopotoshwa na baadhi ya vyombo vya habari hivi karibuni kuwa wataondolewa katika nyadhifa zao.
Hali hiyo kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, imewafanya walimu wakuu hao kwa kushirikiana na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) ngazi ya Wilaya na Mkoa wasikubaliane na uamuzi huo hata kumlazimu mkuu huyo kuitisha kikao cha makatibu na wenyeviti wa CWT na maofisa elimu wilaya ili kuliweka jambo hilo sawa.
Katika kikao hicho Mtaka amewathibitishia viongozi wa CWT wilaya, mkoa sambamba na maofisa elimu kuwa, kamwe hawezi kubadili msimamo wake wa kufanya mabadiliko kwa wakuu hao, na kwamba kwa kufanya hivyo itasaidia kuboresha utekelezaji wa shughuli za elimu mkoani hapo.
Amesema ili mkoa wa Simiyu uweze kuwa na mabadiliko katika elimu, ni lazima kutokee mabadiliko ya wakuu wa shule na waratibu elimu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea toka miaka ya 90 iliyopita.
“Hatuwezi kuwa na walimu wakuu ambao wanafanya kazi kwa mazoea…ni walimu wakuu toka miaka ya 90 … na wengi wao ni wale ambao kielimu wapo chini…ifikie wakati wa kufanya mabadiliko ya wakuu wa shule za msingi na sekondari," aliwaambia.
Kutokana na udanganyifu wa takwimu ulioambatana na uwepo wa idadi kubwa ya wanafunzi hewa waliowekwa katika mpango wa elimu bure, mkuu huyo amewataka walimu hao kuacha hofu kwa kuwa mabadiliko hayo yatafanywa kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Anaeleza kuwa, haoni haja kwa wakuu kuendelea kuwa na hofu na kung’ang’ania madaraka, kwa kuwa hawajazaliwa na madaraka hivyo wakae tayari kuyapokea mabadiliko, na kwamba katika upembuzi huo wa kuteua wengine utazingatia sheria na taratibu bila kumuonea mwalimu yoyote yule.
Sambamba na hilo, Mtaka ameeleza kuwa licha ya kufanya mabadiliko hayo, ambayo yanasababishwa na udanganyifu na ongezeko la wanafunzi hewa, ni vema sasa viongozi wa Mkoa kuangalia uwezekano wa kuwapata walimu wengine wenye sifa nao washike nafasi hizo, kwani inaonekana wakuu wa shule wanafanya kazi zao kwa mazoea yasiyo na tija kwa elimu ya mkoa .
“Haiwezekani Mwalimu amejiendeleza tena kwa ngazi ya uzamili, halafu hapewi kipaumbele chochote katika ongezeko la mishahara, kupanda madaraja na kupanda vyeo, kwasababu ukuu wa shule unaonekana ni wa baadhi wa watu wachache tu, " alifafanua.
Anabainisha kuwa, ili kuondoa tabaka la ubaguzi katika kugawa madaraja na vyeo, ni lazima tuwakumbuke na wale walimu waliokwisha jiendeleza nao wajisikie kuwa na imani na serikali yao, tena hawawezi kuhonga ili wapate nafasi hizo kama wanavyofanya wengine kwa kutoa magunia ya mpunga.
Mtaka amesema mabadiliko hayo yataanza na upembuzi rasmi kuanzia sasa, ili kuwabaini wale wote watakaofaa kuendelea na ukuu wa shule, huku wakiangaliwa kwa vigezo vya kufaulisha shule zao, elimu na ufanisi wa kazi ili kufikia mwezi Desemba wawe tayari wamepata majina rasmi ya wakuu hao.
Naye Joyce Mahisa kutoka Chama cha Walimu (CWT) Bariadi amesema, wanamuunga mkono mkuu wa mkoa kufanya mabadiliko ya wakuu wa shule ambao hawafanyi kazi zao kiufanisi na endapo mabadiliko hayo yatafanyika bila kuvunja sheria na taratibu, yataleta matokeo mazuri katika sekta ya elimu mkoani Simiyu.
Anabaini kuwa, walimu wakuu wengi ni wa muda mrefu madarakani hali ambayo inawafanya baadhi yao wafanye kazi kwa mazoea kuliko kuendana na kasi ya karne hii.
“Walimu wakuu wengi wanafanya kazi kwa mazoea…na wengi wao hata elimu zao zipo chini, kiasi kwamba wanapitwa hata na walimu wa kawaida katika shule zao …hivyo wanaombwa waone mabadiliko hayo kuwa ni jambo la kawaida," alisema.
Alifafanua kuwa, katika karne hii kuna walimu wengi ambao wapo vijijini na wamejiendeleza kielimu wakiwa na uzamili na stashahada, lakini hawana mtu wa kuwasaidia kupanda mishahara, madaraja na kupata vyeo badala yake shule zimekuwa zikiongozwa na wakuu wa shule wenye uzoefu wa tokea miaka ya 90.
Aidha Mahisa ameeleza kuwa, ni matumaini yake kuwa mabadiliko hayo ya wakuu wa shule yatasaidia hata ongezeko la walimu wengi wakuu kujiunga na vyuo vikuu kupitia Chuo Kikuu Huria.
“Ninavyosema hivyo ninaongea nikimaanisha…namaanisha kuwa walimu wengi wakuu wamekuwa na elimu za chini na kuzidiwa na walimu wa kawaida anaowaongoza hali inayosababisha wakati mwingine kuwa na changamoto katika kuongoza…" alisema.
Kwa kuliona hilo, baadhi ya viongozi wa serikali na Chama cha Walimu wameunga mkono dhamira ya serikali ya mkoa kufanya mabadiliko uteuzi huo utakaozingatia taratibu, huku baadhi ya maofisa elimu wakikiri kufanyika udanganyifu wa takwimu za shule unaofanywa na baadhi ya walimu wasio waaminifu.
Katibu wa CWT mkoa wa Simiyu, Said Mselema amesema wao kama chama hawatetei maovu ya walimu na kwamba wanatetea pale panapostahili na si vinginevyo, ikiwa ni sambamba na kurudisha heshima ya walimu wanaofanya kazi zao katika mstari unaostahili.
Pia amepongeza jitihada za Mkuu wa mkoa wa Simiyu Antony Mtaka, katika kuhakikisha kuwa anainua na kuboresha mazingira ya walimu na elimu kwa ujumla.
“Kwetu sisi ni faraja sana kuona, mkuu wa mkoa anatusaidia kuondoa kero za walimu…kwa kuwad ifikie wakati sasa walimu wa mkoa wa Simiyu wanafurahia kuishi mkoani hapo…" Alisema.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Abdallah Malela amewataka walimu na wakuu wa shule kuwa na amani katika utendaji wa kazi zao, kwa kuwa mabadiliko hayo yatafanyika kwa kadri ya ufanisi wa kazi zao.
Aidha amewataka walimu kuona jambo hilo kuwa ni fursa ya kuanza kujiendeleza ili wakae na kusimama katika mstari sahihi.
Kwa upande wao, wananchi wa mji wa Bariadi wamesema, kufanya mabadiliko ni jambo la busara sana katika ustawi wa elimu kwa mkoa wa Simiyu, ambao bado hauko vizuri.
Magreth Kayanda mkazi wa Sima anabainisha kuwa, kwa kufanya mabadiliko hayo kutasaidia kuchochea ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi, kwasababu watakaoteuliwa watafanya kazi kwa bidii, ili waendane na kasi ya uongozi wa awamu ya tano kwa kuhofia na wao kuondolewa.
“Sio siri, baadhi ya walimu wakuu wengi wa shule zetu za mkoa wa Simiyu wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea ...na hiyo imesababisha hata kutokuwadpo na ongezeko la ufaulu na mkoa kuendelea kusuasua kielimu," alisema.
Amedai ni vema walimu hao waone kuwa, kila changamoto ya kazi, wageuze kuwa fursa ya maendeleo katika maisha yao ya utendaji wa kazi.
Nao baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari Bariadi, wamesikitishwa sana kusikia taarifa za kuvuliwa madaraka kupitia vyombo vya habari huku wakiamini utendaji wao wa kazi uko sahihi.
Walimu hao wamebainisha kuwa, endapo kama kuna baadhi ya walimu wamefanya udanganyifu katika idadi ya wanafunzi hewa ni vema kuundwe Tume ya kuchunguza na kila atakayebainika hatua dhidi yake zichukuliwe kuliko kujumuisha walimu wote.

Nipashe
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts