8/23/16

Walimu Washauriwa wafanye uhakiki kubaini wanafunzi hewa
AHADI iliyotolewa na Rais John Magufuli ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, imeanza kutekelezwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Hatua hiyo inatoa ahueni kwa wazazi na walezi katika kulipia wanafunzi na hivyo kufanya mambo mengine ya kuwaletea maendeleo.

Katika mfumo huo wa elimu bure, kila shule inapewa fedha kulingana na idadi halisi ya wanafunzi waliopo shuleni, ikitarajiwa kutokuwapo kwa taarifa za uongo juu ya takwimu za wanafunzi ili fedha zinazopelekwa ziendane na idadi ya wanafunzi.

Mbali na matarajio hayo ya kuwepo kwa idadi halisi za wanafunzi, katika wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, mkuu wa wilaya hiyo, Sophia Mjema amebaini kuwepo kwa wanafunzi hewa 599 kutoka katika shule za msingi sita tu, idadi ambayo inaweza kuongezeka.

Idadi hiyo ya wanafunzi hewa katika shule sita si ya kufurahisha ama ya kunyamazia kwa wilaya hiyo ama kwa shule nyingine nchini, bali iwe ni changamoto kwa walimu kufanya uhakiki wa wanafunzi ili wasiokuwemo waondolewe katika orodha hiyo.

Yumkini walimu wa wilaya hiyo, walijisahau kutoondoa orodha ya wanafunzi hewa, kwa upande mwingine haileti picha nzuri kwa kuwa fedha za wanafunzi wasiokuwamo katika orodha haijulikani kama zinarudi ama zinatumika.

Ikumbukwe kuwa fedha zinazopelekwa katika shule kwa ajili ya wanafunzi, ni za walipo kodi, hivyo kwa walimu kutoondoa majina ya wanafunzi hewa inadhihirisha kwamba kitendo hicho ni cha kujinufaisha wao binafsi na si taifa.

Hata hivyo, ni vyema wakakumbuka kuwa, wanaochukua jukumu la kufanya uhakiki wa idadi ya wanafunzi shuleni, wanawajibika kula kiapo, pindi itakapobainika kama idadi waliyoitoa itakuwa si sahihi, wachukuliwe hatua.

Fedha zinazotolewa kwenda shuleni ni kwa ajili ya kuboresha elimu, ili wanafunzi wapate elimu inayotakiwa kinyume na malengo hayo, ieleweke kuwa nia njema ya serikali ya kutoa elimu bure haitatekelezeka. Walimu wana wajibu wa kuhakikisha kuwa suala la elimu bure lisiwe la kutoa elimu isiyo bora kwa kupokea fedha za wanafunzi hewa waliokuwapo kwenye orodha.

Kwa kuthamini hatua ya elimu bure iliyoahidiwa na kiongozi wa nchi, ifike wakati kila anayehusika awajibike kwa kuhakikisha kuwa wanufaika wa fedha hizo, ambazo ni kodi za Watanzania ni wanafunzi waliopo shuleni ili wapate elimu bora.

Isiwe kutolewa elimu bure, ikawa ndio fursa ya wengine kujinufaisha kwa kuwa na orodha ‘feki’ ambayo imeongeza idadi ya wanafunzi waliopo shuleni tofauti na hali halisi ilivyo.

Kwa kuangalia mfano wa wanafunzi hewa katika wilaya ya Ilala, Dar es Salaam ni vyema kwa shule zote nchini kuhakiki idadi ya wanafunzi waliopo katika shule zao ili kujiridhisha kama wapo na fedha wanazopokea kwa ajili ya kuendesha shule zao ni halali ama zinaishia kwenye mifuko ya wanjanja wachache.

Umakini huo wa kuorodhesha idadi sahihi ya wanafunzi waliopo shuleni, usambae katika maeneo mengine nchini, ili kama kuna mianya inayotumiwa na wajanja wachache ya kuwepo wanafunzi hewa, izibwe na kwa wale wanaotumia mianya hiyo, wachukuliwe hatua za kisheria.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts