Watu 12 Wanusurika Kuuawa na Tembo | Yuvinusm

The Global News and Education

Breaking News
Loading...

8/5/16

Watu 12 Wanusurika Kuuawa na Tembo
WATU 12 akiwemo mtoto wa umri wa miaka mitatu, wamenusurika kuuawa, baada ya kundi kubwa la wanyama aina ya tembo kutoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuvamia makazi yao na kubomoa nyumba tatu walimokuwa wamelala katika kijiji cha Makundusi, kata ya Natta wilayani Serengeti mkoani Mara.

Diwani wa Kata ya Natta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Hamashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini, alisema kuwa tukio ni la usiku wa kuamkia Agosti Mosi mwaka huu, saa 3 usiku kijijini hapo, baada ya wanyama hao kuvamia makazi ya watu na kubomoa nyumba hizo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika katika eneo la tukio, wananchi walionusurika walisema kuwa siku hiyo wanyama hao, walivamia makazi yao na kuanza kubomoa nyumba zao wakiwa wamelala.

Walisema kuwa walinusurika baada ya kukimbilia nje huku mtoto mdogo, Sarah Wesiko (3) akibaki ndani ya nyumba moja. Walisema kuwa walifanikiwa kuwafukuza wanyama hao baada ya kupiga yowe na madebe. Pia, walifanikiwa kumuokoa mtoto huyo, aliyekuwa amejibanza sehemu moja ya ukuta wa nyumba hiyo huku akilia akiomba msaada.

Baadhi ya wananchi hao akiwemo Nyamhanga Wesiko na Madete Karabu, walisema kuwa pia wanyama hao wameharibu samani zote za ndani, kikiwemo chakula na wanaiomba serikali kuwaona kwa jicho la huruma, ikiwa ni pamoja na kufanya doria za mara kwa mara kwa ajili ya kuwadhibiti wanyama hao.

Wananchi wa kijiji hicho, walilalamikia viongozi wao, akiwemo mwekezaji mmoja aliyewekeza katika eneo hilo kwa ajili ya uwindaji wa kitalii, kwa kile walichosema ni chanzo cha wanyama hao kuingia hadi kwenye makazi yao.

Walisema pia kuna kiongozi mmoja amekuwa akijinufaisha na mwekezaji huyo, kwa kuchukua mapato ya kijiji hicho yanayolipwa na mwekezaji huyo.

Walisema kuwa pia wanyama hao wanapoingia kwenye makazi yao, wanapotoa taarifa kwa Askari wa Wanyamapori na viongozi wa halmashauri, wamekuwa hawafiki mapema kwenye eneo la tukio.

"Kwa mfano tukio hili la juzi tulipiga simu kila sehemu lakini hakuna askari au kiongozi aliyefika mapema mpaka wanyama hao tulipofanikiwa kuwafukuza majira ya saa 9 usiku. Kwa hiyo kuanzia muda huo wa saa 3 hadi saa 9 hakuna mtu yeyote aliyefika licha ya kuwapatia taarifa mapema," alisema Wesiko.

Aliongeza kuwa mifugo yao inapoingia hifadhini kwa bahati mbaya askari wa mwekezaji huyo, wamekuwa wakiikamata na kuwapiga faini kubwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Porini alisema kuwa wanyama hao wakiwemo pia simba na chui, wamekuwa wakiingia katika makazi ya watu mara kwa mara na kushambulia mazao ya wakulima ikiwa ni pamoja na kuua mifugo.

Alisema kuwa tayari Idara ya Wanyamapori wilayani, inafanya tathmini ya uharibifu uliofanywa na wanyama hao, ili kuona namna ya kuwafidia wananchi walioathirika.

google+

linkedin