9/22/16

Chuo Kikuu Ardhi kujenga DodomaWAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kutekeleza azma ya kuhamia Dodoma, serikali itatumia Chuo Kikuu cha Ardhi(ARU), kufanikisha ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu za makazi kwa ajili ya watumishi wake.

Hatua hiyo inatokana na chuo hicho, kudhihirisha uwezo wake kupitia ujenzi wa jengo mojawapo la mahakama mjini Kibaha mkoani Pwani.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Waziri Majaliwa wakati akizindua Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015-2020) na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama ya Tanzania kwenye eneo llilipojengwa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi, Pwani na Mahakama ya Wilaya ya Kibaha.

Akizungumzia ujenzi huo, uliofanywa na ARU na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), Majaliwa alisema chuo hicho kimeonesha uwezo wa hali ya juu wa usanifu na kudhibiti ubora sambamba na kujenga majengo ya gharama nafuu.

Chuo hicho kimejenga jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kibaha kwa kutumia teknolojia ya Moladi Chem kwa gharama ya Sh milioni 520, kwa muda wa miezi mitatu, tofauti na bei ya wazabuni iliyokuwa kati ya Sh bilioni 1.73 na Sh bilioni 1.3.

“Chuo chetu cha Ardhi kimeonesha kina uwezo wa usanifu, kudhibiti ubora kujenga majengo ya gharana nafuu, na taarifa nilizo nazo chuo kina uwezo wa ujenzi wa miundombinu yoyote na kwenye azma ya kuhamia Dodoma, tutawatumia watujengee nyumba za gharama nafuu za watumishi wetu”,alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akizungumza kwa kutumia mifano halisi jinsi ARU walivyofanikisha ujenzi bora na wa gharama nafuu uliookoa mamilioni ya fedha, Majaliwa alisema kabla ya kuanza ujenzi wa jengo hilo la Mahakama, wazabuni watatu walioomba zabuni ya ujenzi huo walikuwa na gharama mara mbili na nusu ya gharama hiyo.

“Mfano tu, Katibu Mtendaji wetu wa Mahakama alifanya jaribio kwa kutangaza zabuni ya ujenzi wa jengo hilo, mzabuni wa kwanza alisema atajenga kwa B 1.73 wa pili B 1.43 wa tatu B 1.3 na kwa sheria za manunuzi mzabuni wa chini ndiye mshindi, ila kupitia ardhi wametujengea kwa Sh milioni 520, tumeokoa zaidi ya nusu ya fedha”, alisema Waziri Majaliwa.

Alisema kama ARU, wameweza kujenga jengo bora na la kisasa kwa muda wa miezi mitatu, tu kwa nini wasijivunie uwepo wa chuo hicho na teknolojia hiyo mpya ya kutumia dawa rafiki wa mazingira ya Moladi kujenga majengo bora na yenye kudumu zaidi.

Majaliwa alisema ARU ni miongoni mwa wataalamu washauri walioishauri serikali jinsi ya kuhamia Dodoma na waliitaka serikali ihamie kwa kubadilika na kuwa ya kisasa, na kujenga majengo bora ya gharama nafuu.

“ARU ni miongoni mwa wataalamu washauri waliotushauri jinsi ya kuhamia Dodoma, na kwa hakika kwa ujenzi wa jengo hili la Mahakama ya Hakimu Mkazi walilojenga, wametuthibitishia uwezo wao na ndio maana serikali imeweka Benki ya Rasilimali (TIB Corporate na TIB Development), itawapa mkopo muanze kazi mjenge nyumba nyingi za watumishi wetu waweze kupanga kwa nafuu”, alisema Waziri Majaliwa.

Hata hivyo aliwataka ARU kuimarisha kitengo chao cha ujenzi kwa sababu hivi sasa ndio kilipio la serikali katika ujenzi wa majengo nafuu na kwamba changamoto zilizopo kama vile uhaba wa nyumba za walimu na zahanati zinaweza kumalizwa kwa kutumia chuo hicho kujenga majengo hayo kwa bei nafuu.

Aidha, aliwataka ARU kuangalia jinsi ya kujenga nyumba za wananchi wa kawaida za gharama nafuu kwa sababu gharama zao ni nafuu na jengo moja hujengwa kwa siku tatu hadi nne kukamilika, tofauti na ujenzi wa kawaida.

“Fahari yangu ni kuona mradi huu umebuniwa wa ubora na gharama nafuu, leo tumejenga jengo bora lenye kumbi mbili wala haziingiliani, kila hakimu anaendesha mashauri kwa utulivu na huu ndio mwendo tunaoutaka,” alisema Waziri Majaliwa.

Awali akizungumzia mpango huo, Jaji Mkuu Othmani Chande alisema una malengo makuu matatu ambayo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali, utuaji haki wa wakati na kuimarisha imani ya jami na ushirikishaji wa wadau katika shughuli za mahakama.
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts