9/20/16

CWT Mwanza Chakanusha Kauli ya Waziri wa Elimu Kuhusu Madai ya Walimu.
Chama cha walimu mkoa wa Mwanza,kimekanusha kauli ya Waziri wa Elimu,Sayansi na teknolojia Prof.Joyce Ndalichako kwamba serikali haidaiwi madeni na walimu,jambo ambalo chama hicho kimedai kuwa Waziri huyo ameupotosha umma kwa kutoa taarifa zisizo na ukweli,huku walimu mkoani humo wakisema wanaidai serikali zaidi ya shilingi Bilioni tatu za mapunjo ya mishahara na madai mengine mbalimbali.
Mwenyekiti wa chama cha walimu mkoa wa Mwanza Sibora Kisheri,akizungumza na ITV amesema,walimu wa shule za msingi mkoani hapa wanaidai serikali deni la shilingi bilioni moja na milioni hamsini na tatu za matibabu,likizo,usimamizi wa mitihani, nauli,uhamisho,kujikimu na masomo, huku wa shule za sekondari wakidai zaidi ya shilingi milioni mia mbili na wale wa vyuo vya ualimu na taasisi wakidai jumla ya shilingi milioni 33.

Baadhi ya wenyeviti wa Chama cha Walimu katika wilaya za mkoa wa Mwanza,waliokutana katika ofisi za chama hicho zilizopo Kirumba jijini Mwanza wametoa takwimu za madai mbalimbali ya walimu wa shule za msingi,sekondari,vyuo na taasisi katika wilaya zao.

Kwa upande wake,Katibu wa Chama cha Walimu mkoa wa Mwanza Fatuma Bakari akaeleza jitihada zilizofanywa na CWT mkoani hapa katika kuhakikisha serikali inawalipa zaidi ya walimu elfu kumi na tano madai yao ya kuanzia mwaka 2013 hadi kufikia Agosti 31 mwaka huu.

chanzo: ITV
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm