WAMILIKI wa hospitali binafsi nchini wametakiwa kuajiri madaktari na wauguzi wenye sifa.


Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya.

Agizo hilo lilitolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya afya uliofanyika jijini Dar es Salaam juzi.
Dk. Ulisubisya alisema kama ilivyo katika sekta ya umma inavyohakikisha wafanyakazi wake ni wale sahihi, vivyo hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa katika sekta binafsi.
Alisema sekta ya afya ni muhimu katika uhai wa binadamu, hivyo ni lazima watu wanaofanya kazi nao wawe sahihi, wenye utaalamu na wanaotambulika na mamlaka husika.
Alisema serikali haitamvumilia mmiliki yeyote wa hospitali atakayebainika kuajiri watu wasio na sifa.
"Serikalini imetangaza kuwaondoa wafanyakazi hewa wote na hata wale wasio na sifa hawakubaliki katika sekta ya umma, na tunaamini sekta binafsi hususan katika sekta ya afya, watalizingatia hilo, niseme tu kwamba kumuajiri mtu kwenyƩ kituo cha afya asiye na sifa, ni kosa la jinai na ninaamini watakuwa waaminifu kupitia mamlaka zinazowasimamia, " alisema Dk. Ulisubisya.
Pia alisema kabla ya kuajiri watumishi hao, wanapaswa kuhakiki kwanza vyeti vya taaluma zao kama wamesajiliwa na mamlaka zinazowasimamia.