9/10/16

Hoteli za kitalii zauzwa ArushaHoteli mbili za kitalii za Mount Meru na Snow Crest za mkoani hapa zimetangazwa kuuzwa kutokana na kuongezeka gharama za uendeshaji huku moja ikielezwa kushindwa kulipa stahili za wafanyakazi.


Pia, kuuzwa kwa hoteli hizo kunaelezwa kuchangiwa na kudorora kwa uchumi na kukosa wateja huku nyingine kadhaa mkoani hapa zikipunguza wafanyakazi.


Awali Mount Meru ilikuwa ikimilikiwa na Serikali kabla ya kubinafsishwa na kufanyiwa ukarabati mkubwa. Hoteli hiyo na Snow Crest, zilizinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.


Mount Meru imetangazwa kuuzwa na Dalali wa Kimataifa Mark Danford, ambaye anaishi nchini Marekani kwenye mitandao mbalimbali.


Msemaji wa Mount Meru, Queen Joseph aliliambia gazeti hili kwamba hoteli hiyo inauzwa kwa taratibu za kawaida huku akiwataka watumishi na wananchi kutokuwa na hofu.


“Ni kweli hoteli hii inauzwa na tayari imetangazwa, lakini hatua hii haitokani na kukosa wageni,” alisema Queen.


Queen alisema historia ya hoteli hiyo ni ndefu na fedha za kuifufua baada ya kubinafsishwa zilitolewa na mifuko ya wafadhili mbalimbali, hivyo inatakiwa kuuzwa ili kuzirejesha.


Hoteli ya Snow Crest iliyopo eneo la Ngulelo nayo ipo kwenye mchakato wa kupigwa mnada kutokana na deni la zaidi ya Sh400 milioni, inazodaiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).


Tangazo la kuuzwa kwake linasema kwamba asilimia 25 italipwa baada ya mnada na asilimia 75, ndani ya siku 14 za kazi baada ya mnada huo.


Kufuatia hali hiyo, gazeti hili lilifika hotelini hapo na kukutana na walinzi, ambao walikataa kuzungumza chochote kwa madai kuwa siyo wasemaji.


Meneja wa NSSF mkoani Arusha, Dk Frank Maduga alithibitisha shirika lake kuidai hoteli hiyo malimbikizo ya mafao ya waliokuwa wafanyakazi wake.


Dk Maduga amesema Bodi ya Wadhamini ya NSSF kwa niaba ya wateja wao (wafanyakazi) ilifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Arusha mwaka 2016 kudai fedha hizo na kushinda, hivyo kinachofanyika ni utekelezaji wa hukumu hiyo.


“Tulifungua kesi mahakamani ambako tulishinda na ikaamriwa mali na jengo viuzwe kufidia fedha hizo, sasa tunatekeleza hukumu ya Mahakama,” alisema Dk Maduga.
Weka Maoni Yako Hapa
Share:

Advertisment

Habari Mpya

Follow us on Facebook

Popular Posts

Blog Archive

Copyright © Yuvinusm | Powered by Blogger Design by Yuvinusm