9/4/16

Jecha ageukwa ghafla

LICHA ya kufanikiwa kuongoza vyema uchaguzi mkuu wa marudio uliomrejesha madarakani Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, ameshukiwa akidaiwa kuwa yeye na wenzake waliendesha uchaguzi mbovu.
Na sasa kuna kila sababu ya kufumuliwa kwa tume yao. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume, ndiye aliyetoa mtazamo huo wakati akizungumza katika mahojiano maalumu na Nipashe mjini Zanzibar wiki iliyopita.

Balozi Ali Abeid Karume, amesema sasa kuna sababu ya kuifumua na kuiunda upya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inayoongozwa na Jecha Salim Jecha kwa sababu iliendesha uchaguzi mbovu uliosababisha uchaguzi wa marudio visiwani humo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Nipashe mjini Zanzibar juzi, Balozi Karume alisema kwa mtazamo wake, Jecha na timu yake ndani ya ZEC walijitahidi kuwa makini wakati wa kuandaa uchaguzi mkuu wa awali visiwani humo uliofanyika Oktoba 25, 2015, lakini matokeo ya kazi yao hiyo ikawa ni kufanyika kwa ‘uchaguzi mbovu’ na ndiyo maana wenyewe (ZEC) wakalazimika kuufuta na kutangaza uchaguzi mwingine uliofanyika Machi 20, 2016.

Balozi Karume alieleza hayo wakati akifafanua kuhusiana na swali juu ya nini kifanyike ili kuondokana na mvutano wa kisiasa utokanao na matokeo ya uchaguzi mkuu na kuepukana na athari hasi kwa kila Mzanzibari na pia maoni yake kuhusiana na imani aliyo nayo kwa ZEC.

“Tume ya uchaguzi ilikuwa na usimamizi mkali lakini ni mbovu, uliokuwa ukipendelea chama kimoja,” alisema Balozi Karume kuuzungumzia uchaguzi wa awali ambao ulikuwa na ushindani mkali baina ya chama chake (Chama Cha Mapinduzi – CCM) na mahasimu wao, Chama Cha Wananchi (CUF).

“Baadhi ya wajumbe wa tume (ZEC) kutoka upinzani walikuwa wakifanya kazi ya kuhakikisha kuwa chama chao kinashinda…wakachagua viongozi wa kusimamia vituo vya uchaguzi kutokana na mrengo wa chama fulani,” aliongeza Karume bila ya kuitaja CUF moja kwa moja.

Hata hivyo, akizungumzia maoni hayo ya Balozi Karume anayeamini kuwa sasa ipo sababu ya ZEC kufumuliwa na kuundwa upya ili kuwa na uchaguzi usiokuwa mbovu, Afisa Habari wa ZEC, Idrisa Jecha, alisema siyo kweli kwamba ZEC ilikuwa na usimamizi mbovu bali ilifanya kadri ilivyoweza kusimamia vyema uchaguzi wa awali lakini uliharibika kwa sababu ambazo tayari zilishaelezwa na mwenyekiti wao, Jecha.

Wakati akitangaza kuufuta uchaguzi wa awali Oktoba 28, 2015, Jecha alitaja sababu kadhaa za kufikia uamuzi huo, kubwa ikiwa ni kuwapo kasoro nyingi zikiwamo za baadhi ya maafisa wa ZEC kuegemea maslahi ya baadhi ya vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo.

Katika muundo wa sasa wa ZEC, vyama vya siasa huwa na wawakilishi wake na kwa sasa baadhi ya wajumbe hao hutoka CCM na wengine ni wa kutoka CUF.

Mvutano mkali wa kisiasa uliibuka visiwani Zanzibar baada ya Jecha kuufuta uchaguzi mkuu wa awali uliofanyika Oktoba 25.

CUF ilipinga uamuzi wa Jecha na kuitaka ZEC iendelee na mchakato wa majumuisho ya kura huku mgombea wake, Maalim Seif Shariff Hamad, akiwaambia wandishi wa habari (kabla ya tangazo la Jecha) kwamba alikuwa akielekea kushinda kwa asilimia zaidi ya 50 zitokanazo na taarifa walizokuwa nazo za matokeo yaliyobandikwa kwenye vituo vya uchaguzi na kwamba, kilichokuwa kikifanywa na ZEC ni hila za kutaka kumbeba aliyekuwa mgombea wa CCM, Rais Ali Mohamed Shein.

Jecha aliendelea na msimamo wa ZEC wa kufuta uchaguzi wa awali licha ya kupingwa na wapinzani na pia waangalizi mbalimbali wa uchaguzi huo kutoka ndani na nje ya nchi.

Hatimaye ukaitishwa uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ambao Dk. Shein alitangazwa mshindi baada ya kupata zaidi ya asilimia 90 ya kura zilizopigwa huku CUF wakisusia kwa madai kwamba haukuwa halali.

Akifafanua kuhusu nini cha kufanya ili kumaliza mvutano wa kisiasa utokanao na masuala ya uchaguzi visiwani Zanzibar, Balozi Karume ambaye ni mmoja wa watoto wa Rais wa Kwanza wa visiwa hivyo, Abeid Amani Karume, alisema muhimu ni kwa kila mmoja miongoni mwa wanasiasa kujipanga mapema kwa ajili ya uchaguzi ujao wa 2020 na pia kuifumua ZEC ya kina Jecha.

“Cha kufanyika tujipange kwa uchaguzi ujao wa mwaka 2020. Usimamizi uwe mzuri kujua idadi ya waliojiandisha na idadi ya wapiga kura… siyo idadi ya waliojiandikisha kutofautiana na kura zilizopigwa na haki kila mmoja mwenye haki ya kupiga kura apige kura,” alisema na kuongeza: “Usimamizi wa tume uwe mzuri na itengenezwe katiba nzuri ya kidemokrasia.

Ikifika 2020 kuwe na katiba mpya, tume mpya ya uchaguzi …tume iliyopo sasa, mwenyekiti wa tume (Jecha) alilalamikiwa. Atafutwe mwenyekiti ambaye hatokani na chama cha siasa na wajumbe wa tume wawe hawatokani na vyama vya siasa kama ilivyo tume ya uchaguzi ya sasa.

” Aidha, akieleza zaidi, Karume alidai kuwa baadhi ya wajumbe wa ZEC kutoka upinzani walikuwa wameshaandaa sherehe wakijua kuwa kiongozi wao (Maalim Seif) atashinda kwa sababu walikuwa wameshaandaa mipango ya kukiwezesha chama chao kushinda kutokana na mbinu walizokuwa wameshaziandaa.

“Hadithi ya kusubiri Dk. Shein aondoke madarakani kabla ya 2020 ni za alinacha… tusubiri 2020 katika uchaguzi mkuu… hivi sasa hakuna uchaguzi mwingine,” alisema Balozi Karume.

CHANZO: Nipashe
Share:

Habari Mpya

Follow us Facebook

Popular Posts